Petroli, dizeli bei juu

Petroli, dizeli bei juu

Muktasari:

  • Watumiaji wa mafuta ya petroli, dizeli na ya taa watatakiwa kuongeza kiasi cha pesa zaidi kila watakapohitaji bidhaa hizo baada ya  Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kutangaza ongezeko la bei.

Dar es Salaam. Watumiaji wa mafuta ya petroli, dizeli na ya taa watatakiwa kuongeza kiasi cha pesa zaidi kila watakapohitaji bidhaa hizo baada ya  Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kutangaza ongezeko la bei.

Kwa mujibu wa taarifa mamlaka hiyo, mabadiliko ya bei ya mafuta katika Februari, 2021 yanayoingizwa kupitia bandari ya Dar es Salaam imeongezeka kwa viwango tofauti huku ikitajwa kuchangiwa na mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la dunia na gharama za usafirishaji.

Sasa wanunuzi wa rejareja wa mafuta ya petroli watatakiwa kuongezeka Sh53 zaidi kwa kila lita watakayonunua, kuongeza Sh134 zaidi kwa kila lita ya dizeli huku watumiaji wa mafuta ya taa wakitakiwa kuongeza Sh119 kwa lita ikilinganishwa na bei ya mwezi Januari, 2021.

Katika Jiji la Dar es Salaam wanunuzi wa rejareja watanunua petroli kwa Sh1,887, dizeli kwa Sh1,829 na mafuta ya taa kwa Sh1,769.

Pia wanunuzi wa mafuta kwa jumla watatakiwa kuongeza  Sh52.90 sawa na asilimia 3.10 kwa kila lita ya petroli,  Sh133.36 sawa na asilimia 8.51 kwa kila lita ya dizeli na Sh118.31 sawa na asilimia 7.77 kwa kila lita ya mafuta ya taa.

Kwa mujibu wa Ewura pia bei ya jumla na rejareja za petroli na dizeli katika mikoa ya kaskazini yaani Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara nayo imebadilika ikilinganishwa na toleo la mwezi Januari.

Bei ya rejareja ya petroli na dizeli katika mikoa hiyo imeongezeka kwa Sh91 kwa lita na Sh80 kwa lita katika mtiririko wa awali huku bei ya jumla ya mafuta ya petroli na dizeli ikiongezeka kwa Sh90.92 kwa lita na Sh79.48 kwa lita katika mtiririko wa awali.

Hata hivyo, bei ya mafuta ya taa katika mikoa hiyo itaendelea kubaki kama ilivyokuwa mwezi Januari kwa sababu hakukuwa na shehena ya mafuta hayo iliyopokelewa katika bandari ya Tanga Januari 2021.

Hiyo ikiwa na maana kuwa sasa wakazi wa Tanga watanunua petroli na dizeli kwa Sh1,919 na Sh1,834, Kilimanjaro - Moshi (Sh1,966 na Sh1,880), Arusha (Sh1,976 na Sh1,890), huku wakazi wa Manyara – Babati wakinunua mafuta kwa (Sh2,010 na Sh1,924).

Hali ya kuongezeka kwa bei pia imeonekana pia katika mikoa ya kusini ambapo bei ya rejareja ya petroli na dizeli zitapaa kwa Sh71 kwa lita sawa na Sh76 kwa lita katika mtiririko wa awali.

Sasa wakazi wa Mtwara watalipa Sh1903 kwa kila lita ya petroli na Sh1829 kwa kila lita ya dizeli, wakazi wa Lindi watanunua kwa Sh1,917 na Sh1,842 huku wakazi wa Ruvuma- Songea wakilipa Sh1,989 kwa lita na Sh1,914 katika mtiririko uleule

Bei za mafuta pia katika mikoa mingine kama Mwanza itakuwa Sh2,037 kwa petroli na Sh1,979 kwa dizeli, Mbeya itakuwa Sh1,994 na Sh1,936, Dodoma Sh1,935 na Sh1,888 huku Geita ikiwa ni Sh2,054 na Sh1,995 kwa dizeli

Katika taarifa yake Ewura imesema kampuni  za mafuta ziko huru kuuza petroli kwa kuzingatia bei kikomo kama ilivyokokotolewa na kanuni iliyopitishwa. 

“Pia vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana na yakionesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika,” inaeleza taarifa hiyo

“Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza mafuta kwa bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani. Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja,”