Serikali yavuna Sh1.8 trilioni sekta ya uziduaji
Muktasari:
- Ripoti imeweka wazi taarifa za uzalishaji na usafirishaji wa madini, mafuta na gesi asilia, takwimu za ajira katika sekta ya uziduaji, michango ya kampuni kwa jamii (CSR) na ushiriki wa wazawa katika sekta ya uziduaji ikijumuisha kutoa huduma kwenye kampuni za uziduaji.
Dar es Salaam. Serikali imevuna jumla ya Sh1.877 trilioni kutoka kwa kampuni 44 zilizohusishwa katika sekta ya madini, mafuta, na gesi, huku tofauti kati ya malipo na mapato ikiwa ni Sh402.41 milioni kwa mwaka wa fedha 2021/22.
Hayo yamebainishwa leo na Alhamisi Septemba 12, 2024 na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde alipokuwa akizindua ripoti ya 14 ya Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji Katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI) jijini Dar es Salaam.
Mavunde amesema kampuni 26 kati ya hizo ni za madini, saba ni za gesi asilia na mafuta na 11 zinazotoa huduma katika sekta ya madini, mafuta na gesi asilia.
“Kampuni hizi zimelipa serikali Sh1.878 trilioni na hivyo kupelekea kuwepo kwa tofauti ya Sh402 milioni sawa na asilimia 0.021 ya mapato yote yaliyoripotiwa na serikali,” amesema Waziri Mavunde.
Aidha, ameelekeza uchambuzi wa kina kufanyika kuhusiana na tofauti hiyo ya Sh402 milioni kwa lengo la kubaini chanzo na kutoa ushauri kwa kampuni na serikali ili kuzuia tofauti hizo kujitokeza tena kwenye ripoti zijazo.
Ripoti hiyo pia inatekeleza matakwa ya viwango vya kimataifa vya EITI pamoja na Sheria inayosimamia shughuli za TEITI nchini.
Imeweka wazi taarifa za uzalishaji na usafirishaji wa madini, mafuta na gesi asilia, takwimu za ajira katika sekta ya uziduaji, michango ya kampuni kwa jamii (CSR) na ushiriki wa wazawa katika sekta ya uziduaji ikijumuisha kutoa huduma kwenye kampuni za uziduaji.
Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya TEITI, Ludovick Utouh alisema lengo la ripoti hiyo ni kuweka wazi taarifa kwa wananchi na wadau mbalimbali ili waweze kutumia takwimu hizo kufanya mijadala ya kuboresha na kuongeza mchango wa sekta ya madini, mafuta na gesi asilia katika Pato la Taifa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dk David Mathayo ameipongeza Serikali kwa kutoa taarifa ya wazi ya ulinganisho wa mapato ya sekta ya uziduaji, na kuwataka Watanzania kuitumia taarifa hiyo kushauri na kutoa maoni yao juu ya mchango wa sekta hiyo katika kukuza uchumi wa nchi.