Takwimu rasmi kuchochea uchumi, Ridhiwani ataka uwajibikaji
Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa NBS, Daniel Masolwa, wakati wakati akizungumza katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Muktasari:
- Masolwa amesema kaulimbiu ya mwaka huu inayosema NBS inatoa takwimu rasmi katika kupanga maendeleo, kufanya maamuzi sahihi na kufuatilia utekelezaji wa mipango ya kitaifa
Dodoma. Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema takwimu rasmi ndiyo nguzo katika uchumi wa Taifa na kusaidia msukumo wa tathimini ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa NBS, Daniel Masolwa, wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
“Takwimu rasmi ni msingi wa upangaji wa maendeleo. Serikali, sekta binafsi, watafiti na wadau wengine hutegemea takwimu hizi katika kufanya maamuzi sahihi na kupima matokeo ya mipango inayotekelezwa,” amesema Masolwa.
Kwa mujibu wa Masolwa, NBS pia huzalisha takwimu zinazoonesha hali ya soko la ajira, kiwango cha ukosefu wake, idadi ya watu waliopo katika ajira na wale waliopo nje ya nguvu kazi.
Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa NBS, Daniel Masolwa, wakati wakati akizungumza katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Katika uzinduzi huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete aliagiza watumishi kujali na kuthamini kile walichokabidhiwa kukifanya ama kusimamia lakini waheshimu na kujali walio chini yao.
Ridhiwani amesema wafanyakazi ndiyo Msingi wa Maendeleo na kama watatimiza wajibu inaweza kutoa picha nzuri ya mafanikio ambapo wananchi watafanikiwa kuyafikia malengo.
"Wape nafasi na watumishi walio chini yenu ili nao wapate fursa itakayopelekea kupata morali ya utendaji, lazima tufanye kazi kwa ushirikishwaji na hasa kwenye mageuzi ya kidijitali ili tuwasaidie watu wetu," amesema Ridhiwani.
Amesema kuwa hakuna nafasi ya mtumishi mzembe ambaye anashindwa kutimiza wajibu wake kwani wananchi wanapolalamika kukosa huduma kwa mtu ambaye analipwa na Serikali haipeleki picha nzuri.