Tanzania kuendeleza huduma za mawasiliano Burundi

Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Mhandisi Peter Ulanga (kushoto) akisaini mkataba wa kuongeza huduma ya mawasiliano na Burundi katika hafla iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam, kulia ni Mtendaji Mkuu wa BBS Jeremie Hageringwe.

Muktasari:

  • Burundi wanaongeza huduma za mawasiliano na intaneti kutoka Mkongo wa Tanzania kwa muda wa miaka mitano

Dar es Salaam. Katika kuboresha huduma ya mawasiliano ukanda wa Afrika Mashariki Serikali za Tanzania na Burundi zimeingia makubaliano ya kibishara ya kuongeza huduma kwenye mkongo wa Taifa wa mawasiliano.

Mkataba huo wenye thamani ya Sh8.3 bilioni umesainiwa kati ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL)  na Taasisi ya  Mkongo wa Taifa wa Burundi (BBS).

Burundi wanaongeza huduma za mawasiliano na intaneti kutoka Mkongo wa Tanzania kwa muda wa miaka mitano.

Akizungumza baada ya hafla ya utiaji saini iliyofanyika leo Februari 23 2024, jijini Dar es Salaam, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema hatua hiyo inaashiria umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa kibiashara na kiteknolojia kati ya Tanzania na Burundi pamoja na kufungua njia ya ushirikiano mpana zaidi katika sekta hiyo.

Akitaja manufaa ya kuongeza huduma hiyo, Nape amesema kwa Tanzania, itawezesha upatikanaji wa soko jipya la huduma za mawasiliano Burundi na kuongeza fursa za biashara na uwekezaji.

"Kwa Burundi, itaboresha miundombinu ya mawasiliano na kuimarisha uchumi wake kwa jumla. Ninaamini kwa ushirikiano huu utaimarisha uhusiano wa kindugu kati ya nchi zetu na kuchangia katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Afrika Mashariki kwa jumla," amesema Nape.

Amesema Serikali imeonesha dhamira thabiti ya kusimamia sekta ya mawasiliano kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji, kukuza matumizi ya huduma za kidijitali, kufungua fursa kwa nchi za Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa kutumia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) na Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data Kimtandao (NIDC).

Vilevile, amebanisha kuwa matokeo mazuri ya huduma za mkongo wa mawasiliano wanazopata sasa ndiyo sababu ya Serikali ya Burundi, kupitia BBS, kukubali kuongeza huduma hizo.

"Kama Taifa tunajivunia mchango wetu katika kuboresha mawasiliano Afrika Mashariki, tunaamini mkataba huu mpya utakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa Tanzania na Burundi kwa kuimarisha uchumi, biashara na ushirikiano wa kijamii," amesema Nape.

Pia, ameishukuru Serikali ya Burundi na BBS kwa kuendelea kuiamini Tanzania kuwapa fursa ya kuwahudumia.

"Tunaahidi kuendelea kutoa huduma bora za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa lengo la kukuza maendeleo ya nchi yetu na kanda ya Afrika Mashariki," amesema.

Aidha, Nape amesema Jumuiya ya Afrika Mashariki inapaswa kuwa na mipango na mikakati ya kuendeleza sekta ya mawasiliano ndani ya Jumuiya kwa kujenga mifumo ya kidijitali.

Amesema mifumo hiyo itawezesha Afya Mtandao, Elimu Mtandao, Biashara Mtandao, Kilimo Mtandao, Serikali Mtandao, na malipo kwa kutumia mifumo ya kidijitali na ni muhimu kwa kurahisisha shughuli za maendeleo kwa wananchi.

Awali, akizungumza Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Mhandisi Peter Ulanga amesema Burundi imekuwa mteja wa Tanzania kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano tangu mwaka 2019.

Amesema hatua ya Burundi kusaini tena mkataba ni baada ya matokeo mazuri ya huduma za Mkongo wa Taifa. "Shirika la Mawasiliano Tanzania liko tayari kutoa huduma bora kwa Burundi kwa kuzingatia masharti ya mkataba yaliyokubaliwa.

"Tunaamini ushirikiano huu utaimarisha uhusiano wa kindugu kati ya nchi zetu na kuchangia katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Tanzania na Burundi," amesema Ulanga.

Amesema wanafurahishwa kuona Mkongo wa Taifa ukiendelea kutumika kwa mafanikio katika ukanda wa Afrika Mashariki na SADC.

"Ubora wa huduma na gharama nafuu za Mkongo huu vimetupa motisha ya kuendelea kuwekeza katika miundombinu yake ili iweze kuleta tija zaidi na kuchochea shughuli za maendeleo katika nchi zetu za Afrika," amesema.

Ulanga amesema Mkongo wa Taifa umeunganisha nchi kadhaa kwa kuwa mwaka 2023, TTCL iliingia mkataba wa kibiashara na  Mamlaka ya Taifa ya Teknolojia ya Habari ya Uganda (NITA-U) wa kuunganisha mtandao wa nchi hizo mbili.

"Pia, tulifanikiwa kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano Tanzania na Mkongo wa Taifa wa Malawi kupitia Shirika la Umeme la Malawi (ESCOM). Hadi sasa, tumefanikiwa kuunganisha nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Malawi na Zambia.

"Mkongo umeshafika Mtambaswala katika mpaka wa Tanzania na Msumbiji, juhudi za dhati zinaendelea za kuunganisha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo  (DRC) kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano utekelezaji wake unaendelea," amebanisha Ulanga.

Mtendaji Mkuu wa BBS, Jeremie Hageringwe amesema Burundi mahitaji ya huduma za mawasiliano na intaneti yanakua kwa kasi siku hadi siku ndio maana wameamua kusaini mkataba na Tanzania ili kuongeza huduma hiyo.

"Nawashukuru TTCL kwa hatua hii tunapata huduma bora na gharama nafuu kwa jumla TTCL inaisaidia BBS tunaahidi ushirikiano zaidi," amesema Hageringwe.