Tigo na Zantel kuuzwa kwa Axian group

Monday April 19 2021
kuuzwa pc
By Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Kampuni yaMillicom International inayomiliki hisa za Tigo na Zantel, imepanga kuziuza kampuni hizo kwa ubia utakaoongozwa na Axian Group, kampuni ya mawasiliano yenye makao makuu yake jijini Antananarivo, Madagascar.

Kuuzwa kwa Tigo na Zantel, kunaifanya Millicom kukamilisha safari yake ya kujiondoa katika soko la Afrika ilikodumu kwa zaidi ya miaka 25 badala yake kuelekeza nguvu zake Amerika Kusini.

Axian Group, ni kampuni ya mawasiliano inayotoa huduma katika visiwa vilivyomo kwenye Bahari ya Hindi, Afrika na Ulaya. Huduma zake kwa sasa zinapatikana nchini Madagascar, Senegal, Togo, Visiwa vya Reunion na Mayotte pamoja na Comoro.

“Millicom inafuraha kumpata Axian ambaye ni mwekezaji wa kimkakati kuendeleza huduma za Tigo Tanzania pamoja na Zantel kupeleka huduma nafuu na za kibunifu kwa wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” imesema Millicom kwenye taarifa yake.

Mchakato wa kuhamisha umiliki utakapokamilika muda wowote ndani ya mwaka huu, Axian Group inatarajiwa kuwekeza dola 400 milioni (zaidi ya Sh920 bilioni)  ndani ya miaka mitano ijayo.

“Tunapenda kuwahakikishia wateja wetu na umma kwa ujumla kwamba huduma zetu zitaendelea kuwa kama zilivyo mpaka tutakapopata uthibitisho kutoka mamlaka za usimamizi,” inasomeka sehemu ya taarifa ya Millicom.

Advertisement

Tigo ilianza kutoa huduma zake nchini mwaka 1995 na miaka 15 baadaye ikazindua huduma za fedha, Tigopesa. Mpaka mwishoni mwa Desemba 2020, Tigo ni kampuni ya pili kwa kuhudumia wateja wengi wa mawasiliano hata wa huduma za fedha ikiwa nyuma ya Vodacom

Advertisement