TRA K’njaro yajivunia mafanikio ikivuka lengo la makusanyo

Meneja wa TRA, Mkoa wa Kilimanjaro, Masawa Masatu akizungumza na wafanyabiashara mjini Moshi wakati wa uzinduzi wa wiki a shukurani kwa mlipa kodi. Picha na Janeth Joseph

Moshi. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa Kilimanjaro imekusanya Sh227.72 bilioni kwa mwaka wa fedha 2021/22 ambapo ni zaidi ya asilimia 108 ya lengo lililokusudiwa la Sh210.52 bilioni.

Akizungumza na wafanyabiashara leo Mjini  Moshi, katika  uzinduzi wa wiki ya shukrani kwa mlipa kodi, Meneja wa TRA Mkoani hapa, Masawa Masatu amesema mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano wa wafanyabaishara ambao wamekuwa ni waaminifu waliolipa kodi bila kushurutishwa.

Aidha, amesema katika mwaka wa fedha unaoendelea wa 2022/2023, TRA mkoani humo tayari imeshakusanya jumla ya 89.48bilioni kati ya Julai hadi  Oktoba 2022, ambapo  amesema  ni asilimia 109 ya lengo la kukusanya jumla ya 82.3 bilioni katika kipindi hicho.

"Makusanyo haya yamevuka lengo lililowekwa na mafanikio haya yanatokana na ushirikiano ambao TRA tumeupata kutoka kwa wafanyabiasara ambao ni wale waliolipa kodi bila kushurutishwa," amesema Masatu.

Pamoja na mambo mengine amesema, maadhimisho hayo  yamelenga kuonyesha ushirikiano uliopo baina ya  wafanyabiashara na mamlaka hiyo na kwamba mchango wa wafanyabaishara hao ni mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi na wananchi kwa ujumla.

Akizindua maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Abbas Kayanda aliwapongeza wafanyabiashara ambao wamekuwa wakilipa kodi kwa wakati na bila kushurutishwa na kusema huo ndio uzalendo unaotakiwa katika nchi.

"Tuna kila sababu ya kuwashukuru wafanyabiashara wa Mkoa wa Kilimanjaro kwa namna wanavyoitikia wito wa kulipa kodi kwa hiari na huu ndio uzalendo tunaotaka kuuona kwenye maeneo mbalimbali,"

"Katika kipindi kifupi cha Julai hadi Oktoba mmeweza kukusanya zaidi ya Sh89.48 bilioni wakati lengo lilikuwa ni kukusanya Sh82.3 bilioni, kwa mwenendo huu tunaona kabisa hata mwaka huu wa fedha 2022/23 kutakuwa na uwezekano mkubwa wa kuvuka malengo tuliyojiwekea," amesema

Kayanda amewataka wafanyabaishara kuendelea kulipa kodi kwa hiari kwa ajili ya ustawi mzima wa nchi ili kuweza kuondokana na faini zinzzoweza kuzuilika ambazo kibiashara haziwezi kuketa afya.