Uvuvi haramu, tozo na mabadiliko ya soko vyavuruga uchumi wa samaki
Baadhi ya wavuvi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa wametaja uvuvi haramu, mrundikano wa tozo na matumizi ya taa za betri kuwa ni chanzo cha upungufu wa samaki unaosababisha mauzo yake kushuka ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Tanzania (BoT) iangaziayo ufanisi wa uchumi wa kanda iliyotolewa Oktoba 5 mwaka huu, licha ya uuzaji wa samaki Kanda ya Ziwa kuongoza nchini, lakini umepungua ikilinganishwa na miaka minne iliyopita.
Ripoti hiyo inaonyesha mauzo ya samaki kwa ujumla nchini yameongezeka kufikia tani 94,544.8 maAAwaka 2022/2023 ikichangiwa na ongezeko la kanda ya Kusini MashaaaAriki, lakini kanda ya ziwa yamepungua kutoka tani 34,863.9 mwaka 2019/20 kufikia tani 27,548.6 mwaka 2022/23.
Mapato yatokanayo na mauzo ya samaki mwaka 2022/2023 yalifikia Sh506.8 bilioni, yakipungua kutoka Sh526.5 bilioni mwaka 2021/2022, lakini yakionagezeka kutoka Sh393.2 bilioni ikilinganishwa na mwaka 2019/2020.
Katibu wa Chama cha Wavuvi Tanzania (Tafu), Jephta Machandalo anasema pamoja na kuwepo uvuvi haramu unaochangia samaki kupungua, kuna uvuvi haramu ambao umehalalishwa na sheria akiitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuchukua hatua.
“Samaki wamepungua Ziwa Victoria sababu ya uvuvi haramu unaoendelea, lakini kuna uvuvi ambao umehalalishwa kisheria ambao ni uvuvi wa dagaa.
“Uvuvi wa dagaa umegeuka kuwa uvuvi haramu kutokana na kwamba wavu wa dagaa ni mkubwa sana hauna mipaka, sheria haitamki kwamba wavu wa dagaa unapaswa kuwa na urefu wala upana kiasi,” anasema Machandalo na kuongeza:
“Wakati huohuo kuna aina ya nyavu zinazotumika sasa hivi, zile za Japan ambazo matundu yake ni ya pembe nne badala ya matundu ya pembe sita kama ilivyo nyavu ya kawaida, unakuwa kama kitambaa. Ni kuchuja maji tu lakini kila kitu kinapitiwa ziwani wakati wa uvuvi iwe sangara wa kilo 50, 100, awe wa kawaida, wawe watoto wa sangara au dagaa wenyewe.
“Sasa wavu wa namna hiyo huwezi kutegemea uvuvi endelevu hata kama samaki wanazaana, wao wazaane kwa miujiza gani?”
Mwenyekiti wa Muungano wa Wavuvi nchini (Fuo), Juvenary Matagili yeye anasema taa zinazotumika wakati wa uvuvi ni aina nyingine ya uvuvi haramu, akidai zinachangia kupungua kwa mazao ya samaki.
“Uvuvi haramu ndio unasababisha hayo mambo yote, kwa mfano sasa hivi kuna hizi taa ambazo wavuvi wa dagaa wanazitumia. Asilimia zaidi ya 95 ni uvuvi wa kutumia taa za kienyeji ambazo ni za betri, Serikali inasema watumie mwanga usiozidi wati 10, lakini taa zinazotumika sasa hivi ni zaidi ya wati 20… Serikali inajua kabisa kuna taa za kienyeji lakini haichukui hatua,” anasema.
Anashauri ili kuondokana na uvuvi haramu suala la kuangalia shughuli za uvuvi libinafsishwe kwenye kampuni binafsi kwa kuwa hakuna watu zaidi ambao wamejizatiti kwenye kazi hiyo.
“Kuanzia ngazi ya chini hadi za juu wote wanajua, lakini sheria hazifuatwi… Uvuvi haramu kuuzungumzia ni ngumu kwa sababu karibu maofisa wote wa uvuvi waliopo wanapendelea rushwa, labda sasa suala la udhibiti wa uvuvi haramu litekelezwe na kampuni binafsi kwa kuwa Serikali hatuna wa kujitoa kwa hilo,” anasema Juvenary.
Kiongozi wa wavuvi mkoani Kigoma, Francis John anasema mauzo yameshuka kutokana na kupungua kwa samaki, akidai Ziwa Tanganyika upungufu unatokana na uvuvi haramu na mabadiliko ya tabianchi.
“Uvuvi haramu huku upo wa aina ya filimayaa (wavuvi wanatumia nyavu zinazodaiwa kuwa na sumu ili wapate samaki na dagaa wengi) unaosababisha samaki kuoza masaa machache baada ya kuvuliwa kutokana na kutumia nyavu zenye sumu. Hilo linasababisha samaki kupungua sana ziwa Tanganyika kwa sababu kila wakienda kuvua likipita saa moja samaki wanakutwa wameoza wote,” anasema.
Anaiomba Serikali iangalie aina zote za uvuvi haramu na kuwachukulia hatua za kisheria wahusika watakaokamatwa wakijihusisha na uvuvi huo, ikiwemo kufikishwa kwenye vyombo vya sheria pamoja na kuchomwa moto nyavu wanazozitumia.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wavuvi Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, Onesmo Langi anasema Serikali imeshindwa kuchukua hatua madhubuti za kuzuia uvuvi haramu ambao bado upo kwa kiasi kikubwa pamoja na kuzuia wavuvi kuvua kwenye mazalia ya samaki, hali inayosababisha samaki na mauzo kupungua.
“Kingine kilichosababisha hali hiyo ni mabadiliko ya hali ya hewa, zamani kulikuwa na miti ambayo imeota kandokando ya ziwa, lakini saizi hivyo vitu havipo, hivyo unakuta samaki anapotoka kwenye kina kirefu anakuja pembezoni ya ziwa ili azaliane anakutana na mazingira mabaya yaliyoathiriwa na shughuli za binadamu.
“Serikali ilitenga maeneo ya mazalia ya samaki, inapaswa kuyasimamia ikiwa ni pamoja kuyawekea alama ambayo kila mtu atajua kuwa maeneo hayo shughuli za uvuvi hazipaswi kufanyika.
“Kuhusu uvuvi haramu naamini Serikali ikiamua jambo haiwezi kushindwa kwa kurudisha jambo hilo katika Serikali za Mitaa, lakini pia Serikali iunde bodi maalumu kwa ajili ya kusimamia suala la uvuvi.”
Naye Mwenyekiti wa Wavuvi Mkoa wa Mara, Matete Mgongo anaiomba Serikali itilie mkazo uvuvi haramu, akitolea mfano kama inaweza kuzuia na kudhibiti madini yasitoroshwe kwa nini inashindwa kuwekeza nguvu ya kulinda ziwa.
“Ukiangalia miaka mitano kurudi nyuma tulikuwa tukisomesha watoto wetu kwenye shule binafsi za gharama, lakini sasa wavuvi wengi wamewatoa watoto wao huko, wamerudi kwenye shule za umma sababu kipato chao kimeathiriwa na kukosekana kwa samaki,” anasema.
Vilevile anasema uwepo wa tozo nyingi nao unachangia mauzo kuporomoka, kwa kuwa baadhi ya wavuvi ili waweze kujiendesha wanalazimika kutorosha mazao ya samaki nje ya nchi.
Mabadiliko ya soko na tozo
Mwenyekiti wa Tafu, Bakari Kadabi anasema sababu nyingine ya mauzo kuonekana kushuka kulinganisha na miaka ya nyuma ni wavuvi kuamua kuuza mazao yao ya samaki kwenye masoko ya ndani, akidai wanakwepa kuuza viwandani kulingana na malipo kuwa chini, hivyo kusababisha Serikali isipate takwimu sahihi za mauzo ya kitoweo hicho.
“Kuongezeka kwa masoko ya ndani ambayo yanapokea samaki kwa wingi badala ya viwandani. Hii inatokana na bei halisi ya viwandani haiendani na uendeshaji kazi wa wavuvi, kwa hiyo wavuvi wanaona kuliko kuuza kwa kilo moja hadi nne kuanzia Sh11,000 ni bora wapasue samaki zao watoe mabondo, wauze mabondo alafu wauze minofu ambapo wanapata faida na kuendelea kukidhi uendeshaji wa kazi zao,” anasema.
Machandalo anasema tozo ni sababu nyingine iliyopelekea uuzwaji wa samaki kushuka, akidai wavuvi wanatozwa tozo nyingi zaidi ya 13, hali inayowalazimu baadhi yao kutorosha samaki nchi jirani.
“Yaani samaki mmoja sangara anaweza kuwa na zaidi ya tozo 13 na bado zimeongezwa tozo nyingine. Sasa uendeshaji unakuwa ni mgumu, matokeo yake tuna samaki wengi wanatoroshwa. Samaki wenyewe ni haba, lakini na wale wanaopatikana kidogo wanatoroshwa juu kwa juu,” anasema.
Mtafiti wa uvuvi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania mkoani Mwanza (Tafiri), Philemon Nsinda anasema matumizi ya zana haramu, mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la uvuvi haramu ni sababu ya samaki kupungua na kusababisha mauzo ya kitoweo hicho kushuka.
Hatua za kudhibiti
Kufuatia kuendelea kwa vitendo vya uvuvi haramu, Novemba 28, 2023 Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alimuagiza Mkurugenzi wa Uvuvi, Profesa Mohamed Sheikh kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja wanakomesha.
"Wapo viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama nimeshazungumza navyo, tunataka tumalize hili tatizo, hatuwezi kila siku kutoa maelekezo wakati hayatekelezwi," alisema.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu kuhusu mikakati ya kuzuia uvuvi haramu, aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa uvuvi, Stephen Lukanga alisema Serikali inafanyia kazi suala hilo, huku akidai wizara hiyo ina mpango wa kuanzisha mamlaka itakayodhibiti suala hilo.
“Kuna mikakati fulani tumeweka ambayo hatuwezi kuiweka wazi kwa sababu hizi ni kazi za kiintelijensia ambazo baada ya kufanya uchunguzi na kubaini maeneo na watu wote wanaohusika na uvuvi haramu tutaweka wazi,” alisema Lukanga, aliyekuwa akikaimu nafasi hiyo hadi Oktoba mwishoni.
Aliongeza: “Mpango mkakati wa muda mrefu wizara inajipanga kuanzisha mamlaka, tumeona mbinu nyingi zikitumika huwa hazizai matunda, unadhibiti leo uvuvi haramu halafu kesho unarudi tena, hivyo tunataka tufanye kama wenzetu wa Maliasili na Utalii, wamefanikiwa kupambana na ujangili".