Visa yaipa tano BoT malipo kwa kadi

Dar es Salaam. Makamu rais na Meneja Mkuu wa kampuni ya miamala ya Visa Afrika Mashariki Chad Pollock amepongeza uamuzi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kukataza makato ya ziada kwa miamala ya malipo kwa kutumia kadi za benki, akisema ni hatua muhimu ya kufanikisha uchumi wa kidijitali.
Itakumbukwa kuwa, Julai 16, 2024, BoT ilitoa tangazo la kukataza ada au gharama za ziada katika miamala inayofanywa kwa kutumia mashine za malipo ya wafanyabiashara (POS), huku ikiwataka wananchi kutoa taarifa watakapokutana na hali hiyo.
Katika mahojiano na Mwananchi, Pollack alisema ukiachilia mbali suala la uelewa, miamala kidijitali inakabiliwa na changamoto ya usalama ambayo ni muhimu kwa kuwa watu wanataka uhakika wa usalama wa pesa zao.
“Tanzania ni soko kubwa, ukiangalia idadi ya watu na shughuli za kiuchumi zinatoa matumaini ya kuwa na uchumi wa kidijitali imara,” alisema na kuongeza kuwa kutumia pesa taslimu kuna gharama nyingi, ikiwemo za ulinzi na usalama.
Pollock alirejea utafiti wa kampuni yake uliofanywa hivi karibuni, akisema ili kuachana na gharama za ulinzi na usalama wa fedha, huduma za kidijitali ndiyo suluhisho na hilo linawezekana kwa Serikali kushirikiana na wengine.
Utafiti huo unaoitwa ‘Thamani ya upokeaji: Kuelewa mazingira ya malipo ya kidijitali Tanzania,’ unaeleza kuwa asilimia 84 ya wajasiriamali hao waliohojiwa walieleza kuwa ndani ya miaka miwili iliyopita walianza utaratibu wa kupokea fedha kidijitali.
Ripoti ya utafiti huo inaeleza kuwa asilimia 64 ya wafanyabiashara hao wanaamini kupokea malipo kwa kadi ni uwekezaji wa kimkakati unaoweza kuchangia maendeleo ya baadaye ya biashara zao.
Aidha, ripoti inasisitiza kuwa zaidi ya asilimia 50 ya biashara ndogo na za kati zilizoko kwenye majukwaa ya masoko mtandaoni tayari zinatumia malipo ya kidijitali, ikidhihirisha ukuaji wa mfumo wa malipo wa kidijitali.
“Matokeo ya utafiti yanaonyesha taswira yenye matumaini kuhusu ukuaji wa malipo ya kidijitali Tanzania,” alisema Pullock.
Pullock alisema faida zinazopatikana kwa wafanyabiashara, watumiaji, na uchumi kwa ujumla zinatoa fursa kubwa ya maendeleo. Visa imejizatiti kufanya kazi na wadau wote katika mfumo huu ili kufanikisha upatikanaji wa malipo ya kidijitali kwa wote nchini Tanzania.”
Kadhalika, ripoti hiyo inaangazia fursa muhimu za kuanzisha suluhisho za malipo ya kidijitali zinazotoa urahisi sawa na fedha taslimu, kama vile urahisi wa kurejesha malipo pamoja na usalama wa hali ya juu.
Hata hivyo, pamoja na maendeleo yanayotajwa katika ripoti hiyo, ni asilimia 30 tu ya biashara zinazotegemea fedha taslimu zilikosa mauzo au miamala kwa sababu wateja hawakuwa na pesa taslimu za kutosha.
Hata hivyo, utafiti umebaini changamoto kadhaa zinazoathiri kupanuka kwa matumizi ya malipo ya kidijitali Tanzania ikieleza kuwa watumiaji wengi wamekutana na changamoto kama kushindwa kwa malipo kutokana na matatizo ya kiufundi na gharama kubwa ya kupata mashine za POS.