Wafanyabiashara nchini walia kwa utitiri wa kodi

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji (kushoto) akifurahia jambo na Mkurugenzi wa Kampuni ya Multy Mazao Limited, Riyaz Khan, (wa pili kulia) mara baada ya kufunguliwa kwa  kongamano la Kodi kitaifa lililowasjirikisha wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi, katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam jana. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Wafanyabiashara na wawekezaji jana walitema nyongo wakilalamika kuwa mfumo wa kodi uliopo nchini unaua biashara.


Dar es Salaam. Wafanyabiashara na wawekezaji walitema nyongo wakilalamika kuwa mfumo wa kodi uliopo nchini unaua biashara.

Maoni hayo yalitolewa mbele ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba kwenye kongamano la kitaifa la kodi, huku waziri huyo akisisitiza lengo la Rais Samia Suluhu Hassan ni kutowaumiza walipa kodi.

Miongoni mwa maeneo yaliyolalamikiwa ni msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye ndege za kukodi na utitiri wa kodi katika usafiri wa anga kwa ujumla, kutozingatiwa kwa Itifaki ya kodi ya Afrika Mashariki, kodi ya mwanzo kwa wamiliki wa malori na wengi kutoona umuhimu kulipa kodi.

Maoni hayo waliyatoa katika kongamano lililofanyika jijini hapa, likihudhuriwa na Waziri Mwigulu na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais wa Zanzibar (Fedha na Mipango), Saada Mkuya Salum.

Akifungua kongamano hilo, Waziri Mwigulu alisema tofauti na hali ilivyokuwa kabla na baada ya uhuru, ambapo Serikali ilikuwa ikifanya biashara, hivyo kutotaka sekta binafsi nayo ishiriki kulikuwa na ukandamizaji.

Dk Mwigulu hata hivyo alisema kadri miaka ilivyoenda, Serikali ilianza kuona umuhimu wa kuishirikisha sekta hiyo ndiyo maana mwelekeo wa sasa ni kuilinda sekta binafsi.

“Kwa mtazamo wa Rais (Samia), mtu anayeanzisha uzalishaji anatakiwa awezeshwe, aulizwe anakwama wapi kusudi asaidiwe. Serikali itaendelea kuwalinda wazalishaji kwa sababu ni washirika wakuu katika maendeleo ya nchi,” alisema.


Malalamiko ya walipa kodi

Akizungumza katika mkutano huo, mwakilishi wa wadau wa usafiri na usafirishaji wa anga, Latifa Sykes alisema hatua ya Serikali kuondoa msamaha wa VAT kwa ndege za kukodi imesababisha ndege za nchi nyingine kuvamia soko la Tanzania.

“Tangu Julai 2022, ndege za Chartered kutoka Kenya zimeongezeka sana, wanafanya biashara hasa kwenye sekta ya madini kutokana na sababu inayojulikana kwamba kufutwa kwa msamaha wa VAT kumefungua fursa kubwa kwa wenzetu na kupunguza biashara kwa Tanzania,” alisema Latifa.

Alisema biashara ya usafiri wa anga inaenda sambamba na utalii hivyo kukwama kwa usafiri huo kunakwamisha kukua kwa utalii.

“Utalii nchini una fursa na uwezo mkubwa wa kukua. Mheshimiwa Rais Samia ameitangaza filamu ya The Royal Tour ndani na nje ya nchi na matunda yake tumeanza kuyaona tangu mwaka jana. Lakini hatua ya kutangaza msamaha wa VAT kwa ndege za kukodi kumefumua jitihada za Rais kutokana na bei kupanda kwenye sekta ya anga nchini,” alisema.

Akiunga mkono hoja hiyo, mdau wa usafiri wa anga na utalii, Abdulkadir Rutta Mohamed alisema mbali na kuondolewa kwa msamaha huo, sekta hiyo ina utitiri wa kodi.

“TCAA (Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania) ina kodi karibu 55. Kila rubani kabla hajaendesha ndege anakata leseni, ndege zinakaguliwa kila mwaka na kupewa cheti unacholipia, halafu kuna cheti cha uendeshaji na ukienda kusoma unapaswa umsomeshe na mtu atakayesimamia masuala ya anga kusudi aje aelewe anachokuja kukagua na wanataka umlipie daraja la kwanza kwenye ndege wakati wewe unapanda economy, mambo ya ajabu,” alisema Mohamed.

Kwa upande wake, mwakilishi wa kiwanda cha Mufindi Paper Mills, Elly Pallangyo alisema licha ya kufuata Sheria ya Ushuru wa Afrika Mashariki, nchi za Uganda na Kenya zinazuia bidhaa zao kuingia kwenye masoko yao.

“Lakini nchi hizo hivi sasa zinazuia bidhaa zetu kuingia kwao kwa sababu wanaingiza bidhaa kutoka kwenye masoko ambayo ni rahisi,” alisema Pallangyo.

Mjumbe wa Jumuiya ya Wasafirishaji Tanzania (TAT), Focus Isango alisema Serikali imeweka kodi wanayotakiwa kuilipa mwanzo kabla hawajapata faida, jambo linalochangia kuua biashara zao. “Siku za hivi karibuni imeanzishwa kodi inaitwa advance tax (ushuru wa mapema) kwa anayeanzisha biashara. Kumbuka kwa wasafirishaji, mtu ana magari 100 au 200 na wengi wanakopa benki halafu kila gari anatakiwa alilipie ushuru wa mapema wa Sh3 milioni, kama si kuziba mwanya wa uchumi hapo ni nini?” alihoji Isango.

Hata Msemaji wa Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa), Elias Lukumay alisema licha ya umuhimu wa usafiri wao, bado wanaongezewa kodi tena wanazotakiwa kulipa kabla ya kupata faida kwenye biashara yao.

“Changamoto hii ya advance tax, ni kwamba inatuumiza na itaiumiza bandari yetu ambayo kwa asilimia 95 inategemea usafirishaji wa malori,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Vodacom, Philip Besimire alisema tozo ya miamala ya kielektroniki iliyoanzishwa hivi karibuni ilisababisha kuwapoteza wateja wao milioni moja wa Mpesa.

“Kuna haja ya kuangalia uwezekano wa kupunguza kodi na tozo zilizopo, kupoteza wateja milioni moja si jambo dogo,” alisema.Johnson Minja, mwenyekiti mstaafu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) aliulalamikia utaratibu wa forodha unaotumika kukadiria kodi ya bidhaa zinazoingizwa kutoka nje.

“Watu wanaweza kuingiza makontena yenye bidhaa za aina moja ila kila mmoja akalipa kiwango tofauti cha kodi. Wakadiriaji wamepewa mamlaka makubwa sana, tuweke mwongozo utakaoonyesha kiasi cha kodi kinachostahili ili kuondoa tofauti inayojitokeza,” alishauri.


Wananchi wapewe mamlaka

Akichangia mjadala huo, mwakilishi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Dk Camilus Kassala alisema licha ya uelewa wa kulipa kodi, kinachokosekana ni mamlaka ya wananchi kusimamia maendeleo yao.

“Wakipewa mamlaka wataelewa. Ikiwa Serikali ina mamlaka ya kuchukua kodi na tozo kutoka chini na kupeleka juu basi izigawe kwa usawa na kwa wakati,” alisema padri huyo.

Pia, alishauri kuwezeshwa kwa Serikali za Mitaa ili ziwe na mamlaka ya kukusanya na kupanga maendeleo yao kupitia kodi.

“Kama katika mkoa au jimbo fulani la upinzani hautapelekewa hela tusitarajie wananchi kuona umuhimu wa kulipa kodi. Wanachi wapewe mamlaka ya kusimamia ukusanyaji wa kodi na maendeleo yao,” alisema.

Dk Kasala ambaye pia ni mtafiti mwenza wa Tax Justice Africa Network, aliitaka Serikali kuweka wazi mikopo na mikataba hasa ya kimataifa inayosaini kwa wananchi ili wajue ina matokeo gani katika maendeleo yao.