Wakulima wachekelea bei ya mbaazi kupaa

Wakulima wa zao la Mbaazi wakifungua barua zilizoombwa na wanunuzi kwenye mnada wa mbaazi katika Kijiji cha Mtua mkoani Lindi. Picha na Bahati Mwatesa
Muktasari:
- Wakulima wa zao la mbaazi mkoani Lindi, wameishukuru Serikali kwa kukubali kuweka mfumo wa stakabadhi ghalani kama ilivyo kwenye ufuta na korosho.
Lindi. Kutokana na bei nzuri zinazojitokeza kwenye minada ya mbaazi wakulima wa zao hilo katika Kijiji cha Mtua, Amcos ya Mtua Halmashauri ya Mtama mkoani hapa, wameishukuru Serikali kwa kukubali kuweka mfumo wa stakabadhi ghalani kwa kuwa mfumo huo humnufaisha mkulima.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti leo Jumatatu Septemba 11, 2023 wakulima Japason Matteka na Fatuma Abelly wa Kijiji cha Mtua, wamesema kuwa kabla ya mfumo wa stakabadhi ghalani, walikuwa wanauza kilo Sh200 na ikashuka hadi Sh100.
"Tulikata tamaa kabisa kulima zao hili, kutokana na kukosa soko la uhakika, ikawa huwezi kuuza mbaazi kilo 200, wakulima wengi tuliamua kuachana na mbaazi tukawa tunahangaikia kilimo cha ufuta na korosho,” amesema Japason Matteka.
Mkulima Fatuma Abel amesema, "Mwaka huu wakulima wegi hawakulima mbaazi kwa kuwa kulikuwa hatuna uhakika na soko lenyewe ,ila baada ya kuweka mfumo wa stakabadhi ghalani, bei yake inaridhisha ,mwakani watu wengi tutalima mbaazi, kama zao la biashara na chakula."
"Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuona wakulima baada ya kukubali mbaazi iingizwe kwenye mfumo huu," amesema Abelly.
Mwakilishi wa Mrajisi wa Vyama Vikuu Mkoa wa Lindi, Mbaraka Malelo amesema kuwa jumla ya minada minne imeshafanyika kwa vyama vikuu viwili vya Lindi Mwambao na Chama Kikuu cha Runali na kupata jumla ya tani milioni 14 na Sh29 bilioni zilipatikana na fedha hizo zimeshalipwa kwa wakulima.
Hata hivyo, Malelo amesisitiza wananchi kulima mbaazi kwa wingi na kuwataka kuwa na sauti moja ili kuweza kuongezeka kwa bei hapo baadaye.
"Niwasisitize wakulima kujitahidi kulima kwa wingi zao la mbaazi, mkulima kwa wingi tutaongeza pato la mkoa na taifa kwa ujumla na kuwa na sauti moja ili hapo baadaye bei ziweze kuwa nzuri zaidi," amesema Malelo.
Mhasibu Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika Lindi Mwambao kinachojumuisha Wilaya tatu, Wilaya ya Kilwa, Wilaya ya Mtama pamoja na Manispaa ya Lindi Mabruk Ismail amesema kuwa hadi sasa chama chake kimeshafanya minada mitatu, ambapo wakulima kwa minada miwili wameshalipwa pesa zao zote na ziliuzwa tani 989 zenye thamani ya Sh2 bilioni.
Jumla ya kilo 436,236 zimeuzwa katika mnada wa tatu kwenye Amcos ya Mtua Halmashauri ya Mtama ambapo bei ilikuwa Sh2,252 kwa kilo moja.