Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wazalishaji chumvi ghafi watikisa soko

Muktasari:

  • Wizara ya Madini na Wizara ya Viwanda na Biashara zaingilia kati.

Mkuranga. Serikali imesema uhaba wa chumvi ghafi kwenye viwanda inatokana kukosekana kwa mfumo wa kuratibu usafirishaji wa bidhaa hiyo.

Kauli hiyo imetolewa leo, Jumanne Desemba 19,2023 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk Hashil Abdallah alipofanya ziara katika kiwanda cha kuzalisha chumvi cha Neel kilichopo Mkuranga, mkoani Pwani.

Uongozi wa kiwanda hicho chini ya Kampuni ya Kneelkant Group Africa umeeleza kuishiwa malighafi na hauwezi kuendelea na uzalishaji hata kwa siku moja.

Dk Abdallah amesema baada ya majadiliano na wazalishaji na uongozi wa kiwanda hicho, wamekubaliana kuendelea kupeleka malighafi kiwandani hapo.

Ziara hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya mawaziri wa Madini na wa Viwanda na Biashara ili kupata ufumbuzi wa uhaba wa chumvi ghafi katika kiwanda hicho.

“Tumebaini kilichokosekana ni muundo wa biashara hii kwa namna ya uzalishaji na usambazaji viwandani,” amesema Dk Abdallah na kuongeza:

“Tumepeana mwezi mmoja kukaa pamoja ili kushughulikia changamoto hii, kwanza wazalishaji wa chumvi ghafi waendelee kupeleka kiwandani hapo wakati tukishughulikia muundo wa biashara hiyo.”

Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali amesisitiza wazalishaji kuuza bidhaa hiyo wakati wanashughulikia changamoto zilizopo.

Mhazini wa chama cha wazalishaji wa chumvi ghafi, Aboud Noordin Hussein ameihakikishia Serikali na kiwanda hicho kwamba wataendelea kufanya nao biashara ili kukidhi mahitaji yaliyopo.

“Tuna uwezo wa kufikia mahitaji yote ya soko, kwa mwaka tunazalisha tani 192,000 lakini mahitaji ya kiwanda hicho ni tani 84,000, kwa hiyo akiba ipo kubwa,” amesema.

Kuhusu kiwanda

Meneja mkuu wa uzalishaji wa kiwanda hicho, Ahmed Said Ahmed amesema changamoto ya makubaliano ya bei na wazalishaji wa chumvi ghafi yatapatiwa ufumbuzi ndani ya mwezi mmoja.

“Tulikuwa tumebakiza akiba ya tani 500 tu ya chumvi ghafi ambayo haitoshi hata kwa mahitaji yetu ya siku moja katika uzalishaji, kwa hiyo tunahitaji watuletee malighafi hiyo kwa wingi,” amesema.

“Mahitaji yetu kwa mwaka ni tani 180,000 lakini tumekuwa tukipata tani 84,000 pekee kwa wazalishaji wa ndani, tunatamani angalau wafikie asilimia 50 ya mahitaji yetu,” amesema.

Kiwanda hicho kilichoanza  uzalishaji mwaka 2017, kinamiliki asilimia 40 ya mahitaji ya soko la ndani, thamani ya uwekezaji wake ulikuwa Dola za Marekani 22 milioni (Sh55 bilioni).

Kiwanda hicho kimeajiri zaidi ya Watanzania 500 na bidhaa zake huuzwa nchini, Malawi na Zambia.

Kwa mujibu wa Wizara ya Viwanda, kiwanda hicho ni kikubwa miongoni mwa takribani 10 vya kuzalisha  chumvi nchini.