Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mapambano dhidi ya dawa za kulevya duniani

Muktasari:

  • Magenge ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya, mtandao wao ni mpana, kadiri vigogo wanavyokamatwa ndivyo wengine wanavyoibuka na kuongeza ugumu wa vita.
  • Ugumu wa vita dhidi ya dawa za kulevya unasababishwa na fedha. Hakuna biashara ambayo inaweza kumpatia mtu utajiri kwa haraka kama dawa hizo. Uwapo wa fedha nyingi kwenye mzunguko ni sababu ya watu wengi kung’ang’ania kuwapo huko na hata kugoma kutoka.

Biashara ya dawa za kulevya ni ngumu sana. Mataifa makubwa kama Marekani yamekuwa yakiwekeza bajeti kubwa kila mwaka lakini Taifa hilo limekuwa likipata matokeo yenye kukatisha tamaa. Kadiri wanavyoongeza nguvu ndivyo wauza dawa za kulevya wanavyodhihirisha uimara wao.
Magenge ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya, mtandao wao ni mpana, kadiri vigogo wanavyokamatwa ndivyo wengine wanavyoibuka na kuongeza ugumu wa vita.
Ugumu wa vita dhidi ya dawa za kulevya unasababishwa na fedha. Hakuna biashara ambayo inaweza kumpatia mtu utajiri kwa haraka kama dawa hizo. Uwapo wa fedha nyingi kwenye mzunguko ni sababu ya watu wengi kung’ang’ania kuwapo huko na hata kugoma kutoka.
Fedha nyingi kwenye mzunguko na utajiri mkubwa na wa haraka, husababisha wengi kuvutiwa na biashara hiyo.
Ripoti za Ofisi ya Dawa na Uhalifu ya Umoja wa Mataifa (UNODC), zinaonyesha kuwa thamani ya uhalifu wa mipango (organized crime) kwa jumla, kwa asilimia 50 unabebwa na dawa za kulevya.
Mantiki hapo ni kuwa, dawa za kulevya ndiyo uhalifu wenye thamani kubwa zaidi duniani. Ripoti ya sasa ya UNODC inaonyesha kuwa mzunguko wa kifedha wa biashara ya dawa za kulevya duniani kwa mwaka ni Dola 435 bilioni za Marekani ambazo kwa sarafu ya Tanzania ni Sh972 trilioni.
Fedha za haraka
Brian O’Dea, raia wa Uingereza, alikuwa bilionea wa unga kabla hajaacha. Katika kitabu chake kinachoitwa ‘HIGH: Confessions of a Pot Smuggler’, kilichotoka Aprili 11, 2006, anaeleza kuwa aliifanya biashara hiyo kwa mafanikio.

O’Dea ambaye aliwahi kufungwa miaka 10 nchini Marekani, anaandika kuwa wakati fulani baada ya kutoka jela hakuwa na fedha, hivyo alikwenda Colombia na kujitambulisha kwenye genge la Sinaloa linaloongozwa na Joaquin Guzman ‘El Chapo’ kuwa naye ni memba ila alikuwa jela.

Huko alipewa gramu 50 tu za cocaine ambazo alipita nazo sehemu zote za ukaguzi lakini wakaguzi hawakugundua kama alibeba unga kwa sababu walimuona ameshika pakiti ya sigara. Naye kwa kuwapoteza aliifungua kabisa na kutoa sigara moja na kuvuta.

Kwamba unaona pakiti ya sigara, unafungua unakuta sigara zenyewe lakini ndani watu wamefunga mzigo kati ya gramu 50 mpaka 100. O’Dea anasema baada ya kuuza gramu hizo 50 Marekani, aliendelea kuzungusha cocaine ambazo ndani ya miezi miwili zilimfanya atengeneze Dola 1 milioni (Sh2.23 bilioni kwa sarafu ya sasa).

Mtu anatoka jela kisha anaanzia mtaji wa gramu 50 halafu kwa haraka ndani ya miezi miwili anafikisha utajiri wa Sh2.23 bilioni, unaweza ukakisia biashara hiyo nguvu yake ni kubwa kiasi gani.

Kwa haraka O’Dea ndani ya miaka michache alifikisha Dola 200 milioni (Sh447 bilioni). Akaweka makazi yake Marekani, akanunua meli ya uvuvi ambayo aliitumia kusafiri na kuuza unga ndani ya Bahari ya Pacific. Wakaguzi walipoiona waliikagua na kukuta samaki, lakini ndani kulikuwa na cocaine.

Anasema samaki hao walipakiwa kwenye malori na kupita barabarani wakiwa wamewekewa barafu kama vile wanaenda kuuzwa, lakini walipofika sehemu husika walitoa unga ndani ya samaki kisha biashara kubwa ilifanyika.

O’Dea anasema pia kuwa, nguvu yake iliingia mpaka ndani ya kikosi cha ujasusi cha kupambana na dawa za kulevya Marekani (Dea), akawa na watu wake ambao walimpa taarifa za ndani, vilevile aliwatumia kwa mipango yake mingi, ikiwamo kuwakamatisha wauza unga wenzake kisha yeye kuvuna faida kubwa.

Jeuri ya wauza unga

Fedha nyingi ambazo wauza unga huwa nazo huwapa jeuri kuona wanaweza kuiendesha Serikali yoyote duniani. Tukumbuke sakata la Narcosobrinos nchini Venezuela. Narcosobrinos ni maneno ya Kispaniola (Spanish au Castilian) yenye maana “Wapwa Wauza Unga”. Narco ni Wapwa na Sobrinos ni Wauza Unga.

Narcosobrinos ni maneno yaliyotumiwa na vyombo vya habari kutambulisha sakata la wapwa wa Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro na mkewe, Cilia Flores, waliokamatwa na kilogramu 800 za cocaine Novemba 10, 2015.

Wapwa hao wa Rais Maduro, wanaitwa Efrain Antonio Campo Flores na Francisco Flores de Freitas, walikamatwa na maofisa wa kikosi cha ujasusi cha dawa za kulevya cha Marekani (Dea) walipokuwa Port-au-Prince, Haiti wakijaribu kuingiza mzigo huo wa cocaine nchini Marekani.

Novemba 18, 2016, wapwa hao wa Rais Maduro walikutwa na hatia. Maelezo yaliyotolewa mahakamani ni kuwa walikuwa wametumwa tu, kwamba wahusika ni Rais Maduro na mkewe Celia ambaye ni Naibu Rais wa Bunge la Venezuela.

Ilielezwa kuwa fedha hizo za cocaine zilikuwa kwa ajili ya kusaidia familia ya Rais Maduro kuendelea kubaki madarakani. Kwamba familia ya Rais Maduro inaongoza mtandao mpana wa unga ambao imeurithi na kuuendeleza kutoka kwa aliyekuwa Rais wa Venezuela, Hugo Chavez.

Mhariri wa Washington Post, Jackson Diehl, alipata kuandika habari kuhusu mtandao mpana wa dawa za kulevya kwenye Serikali za Amerika Kusini, akasema kuwa Hugo Chavez na timu yake ya Serikali ya Mapinduzi ya Bolivarian, walikuwa wanaongoza genge hatari la wauza unga.

Suala la wauza unga kuwa na nguvu nyingi kwenye Serikali, mfano wake upo kwa bilionea raia wa Mexico, Joaquin Guzman ‘El Chapo’, anayeongoza genge la Sinaloa. Kila anapokamatwa hutoroka.

Bajeti ya El Chapo kutoroka jela inatajwa kufikia mpaka Dola 500 milioni za Marekani, yaani Sh1.1 trilioni. Kwamba akishawekwa ndani, maofisa wa serikali ya Mexico na nyingine, wanamwaga fedha kama njugu, mwisho ulinzi unalegezwa halafu ‘mtu mzima’ Chapo anatoroka. Hivi sasa Marekani wamemkalia kooni, kwani alipokamatwa tu Wamarekani walikwenda kuimarisha ulinzi na Januari 19, mwaka huu alihamishiwa Marekani ambako sasa ni wazi fainali yake imewadia.

Ukichunguza mtandao wa El Chapo unaona kuwa vituo vyake vya mauzo ni Marekani, Bara la Asia, Afrika Kusini, eneo la Magharibi ya Afrika, vilevile ana kituo Brazil.

Dawa za kulevya zinafanywa na watu wenye jeuri zao. Kuna watu wamekamatwa lakini wanaishi ndani ya jela kama wapo kwenye nyumba na ofisi zao. Wapo jela lakini wanaendesha magenge ya unga. Wakiamua wanatoka kwenda kufanya harakati zao kisha wanarudi ndani.

Wauza unga wanaweza kukamatwa na mzigo kweli lakini wakiwa jela hutumia jeuri yao ya fedha kuutorosha mzigo kwenye mikono ya dola.

Hapa Tanzania limewahi kuripotiwa tukio la cocaine kubadilishwa kuwa chumvi polisi. Kwamba wauzaji walikamatwa na cocaine, baada ya siku chache ikageuka chumvi.

Mitandao ya wauza unga

Mitandao ya dawa za kulevya ina fedha nyingi. Fedha hizo zimefanya biashara yao iendeshwe kwa teknolojia ya hali ya juu. Matokeo yake unga hupitishwa bandarini, mipakani na kwenye viwanja vya ndege bila kushtukia.

Magenge ya wauza unga sasa hivi hutengenezesha magari maalum ya kusafirishia unga. Unaweza kulisimamisha na kulikagua kila mahali na usione unga.

Mfano wewe unaona gari aina ya saloon. Watu wanajua saloon zilivyo. Wewe unakagua ndani kisha huoni kitu. Wenye gari lao wakifika mahali panapohusika, bodi la nyuma linavutwa, saloon inakuwa na mwonekano wa Pickup. Katikati kunakuwa eneo lenye kubeba hata Kg 300 za cocaine.

Tukokotoe sasa. Gramu moja ya cocaine katika soko la dunia kwa bei ya kutupa ni dola 200, yaani Sh447,000. Kwa msingi huo, kg moja ya cocaine ni dola 200,000, Sh447 milioni. Kg 300, maana yake ni Sh134 bilioni.

Mtu ambaye anatengeneza Sh134 bilioni kwa mkupuo mmoja, anapoingiza magari 10 thamani yake ni kiasi gani? Magari hayo hupita mipakani na mengine hupokelewa bandarini na kulipiwa kodi na ushuru. Wakaguzi hawawezi kujua magari yamebeba kitu gani. Wakiangalia ndani yako matupu.

Magari mengine yanatengenezwa kwa aina yake. Yale maeneo yenye vioo vya madirisha (power windows) na chini ya viti yanafunguliwa kwa vitufe (batons). Sehemu moja ya ‘power window’ inaweza kuwekwa mpaka kg 20 za cocaine. Askari akiangalia, akivuta power window hazifunguki na kila eneo lipo sahihi, ila wenye magari yao wanabonyeza vitufe panaachia kisha mzigo unatolewa.

Wauza unga wanamiliki viwanda bubu na vingine halali. Unakuta makontena ya kondomu yanasafirishwa kwa sababu za kibiashara au misaada. utaikuta kondomu imefungwa vizuri kwenye pakti yake. Kumbe ndani imejazwa heroin.

Unga waweza kusafirishwa kwenye vinywaji vya makopo. Utakuta kinywaji na utafungua unywe kuhakikisha. Kumbe lile kopo limegawanywa katikati, juu kinywaji, chini unga. Hiyo ni kazi ambayo inafanyika kiwandani. Wahandisi wenye utaalamu wa hali ya juu huifanya hiyo kazi.

Mbinu mbalimbali hutumika kupambana na uhalifu wa biashara ya dawa za kulevya duniani? Matoleo yajayo tutaeleza ugumu wa vita yenyewe kisha tutaangalia kila mbinu, mafanikio na changamoto zake.

Luqman Maloto ni mwandishi wa habari, mchambuzi na mshauri wa masuala ya kijamii, siasa na sanaa. Ni mmiliki wa tovuti ya Maandishi Genius inayopatikana kwa anwani ya mtandao www.luqmanmaloto.com