Utalii; Zanzibar sasa wachangamkia fursa

Watalii wakifuatilia mashindano ya ngalawa ambayo hufanyika kila mwaka
Muktasari:
Mbali na kujivunia Muungano, Watanzania wanasherehekea mafanikio yaliyopatikana katika kipindi hiki cha miaka 50.
Zanzibar. Wakati Watanzania wakisherekea miaka 50 ya Muungano, pande zote za nchi zina sababu mbalimbali za kufurahia Muungano huu mkongwe barani Afrika.
Mbali na kujivunia Muungano, Watanzania wanasherehekea mafanikio yaliyopatikana katika kipindi hiki cha miaka 50.
Licha ya kuwa visiwa hivyo ni maskani ya utalii Afrika Mashariki, miaka ya nyuma asilimia kubwa ya wakazi wa Unguja na Pemba, walikuwa nyuma kushiriki moja kwa moja katika biashara ya utalii.
Tofauti za kiutamaduni baina ya wenyeji na watalii mbalimbali, hususan wanaotoka nchi za barani Amerika na Ulaya, zilitajwa kuwa kichocheo kikubwa cha Wazanzibari kutochangamkia fursa zilizo kwenye sekta ya utalii.
Wakazi hao sasa wameamua kuvunja misimamo hiyo na kujitosa moja kwa moja katika nyanja tofauti za maendeleo, hususan katika utalii na biashara.
Katika bustani ya Forodhani iliyopo Mji Mkongwe vijana wengi ndio wanaomiliki vijiwe mbalimbali vya kuuza vyakula na wanaonekana kuwachangamkia wageni wote wanaopita maeneo ya jirani na biashara zao.
Wanawake nao wanachangamkia fursa kwa kufanya kazi ya kusuka watalii, wakati malazi sasa yamekuwa ni chanzo cha mapato kwa kuwa sasa wananchi wamegundua kuwa watalii wanalipa vizuri tofauti na zamani wakati wenyeji walipokuwa wakitoa malazi bure.
Mwamko huo pia umeonekana katika masoko ya Mwanakwerekwe na Darajani.
Wengi huwakaribisha wageni hao kwa ukarimu na ushindani mkubwa baina yao na hujitutumua kuzungumza Kiingereza hasa kwa maneno kama “my friend, my friend (rafiki, rafiki)” kama njia ya kuwaita wazungu wasiojua Kiswahili.
“Ni kweli utalii unatupa riziki kwa kuongeza vipato vyetu,” anasema mkazi wa Nungwi, Haji Ame ambaye hata hivyo anaelekeza lawama za kufinywa kwa ajira za wazalendo kwa wamiliki wa hoteli.
“Lakini wawekezaji wanatunyima ajira. Mameneja wengi wasio wazalendo kutoka Kenya, Tanzania bara, Uganda, Burundi hawatujali,” anasema Ame.
Ame anaongeza kuwa wanakijiji huchukua zabuni ya kuuza samaki kwenye hoteli zilizo jirani na hupewa malipo yao kila mwezi. Anasema kuna wakati samaki aina ya nduwala huuzwa kwa Sh1.3 milioni au zaidi kwa wawekezaji hao.
Hata hivyo Ame bado anakwazwa na mavazi wanayoendelea kuvaa baadhi ya watalii wanapotembelea vivutio vilivyopo jirani na maeneo yao.
“Maendeleo haya yameharibu kabisa maadili ya Kinungwi. Zamani watalii wakija tulikuwa tunawavisha mashuka mara tu wanapoingia nchini, lakini sasa wanakuja na vinguo vifupi vinavyoishia mapajani,” anasema Ame huku akionyesha kukerwa na changamoto hiyo.
Sheha wa Shehia ya Kiwengwa mkoani Kaskazini Unguja, Maulid Masoud anasema uboreshaji wa miundombinu kama barabara na pia kuongezeka kwa hoteli za kitalii katika maeneo yao kumekuwa chachu ya Wazanzibari wengi kujitosa katika biashara ya utalii.
“Hapo zamani mtu akitaka ardhi ulikuwa unamkatia kipande bure kabisa bila ya wasiwasi kwa sababu hakuna mtu aliyejua thamani yake.
Hata hivyo, walipoanza kuja wawekezaji, ardhi imekuwa lulu kipande kidogo tu unaweza kuuziwa Sh50 milioni au zaidi ya Sh100 milioni,” anabainisha Masoud.
Anaongeza kuwa baada ya Barabara ya Pongwe-Matemwe, Mkwajuni-Nungwi kukamilika mwaka 2009 walianza kupokea wageni wengi wakiwemo wawekezaji ambao waliamsha ari ya kufanya biashara.
“Unajua zamani mtu alikuwa anaweza kuazimwa nyumba bure kwa kipindi fulani bila kodi. Lakini kwa sasa kila mtu kagundua vyumba ni mali, huwezi kupata chumba hapa bila Sh60,000 au Sh70,000,” anasema kiongozi.
Masoud anabainisha kuwa kuna wakati wakazi hao hukodisha nyumba zao za kawaida kwa Watalii kwa kiwango cha Dola 350 za Kimarekani (Sh560,000), hasa wakati wa msimu wa wageni wengi.
Voti Mtumwa, mkazi wa Kiwengwa wilayani Kaskazini B, Mkoa wa Kaskazini Unguja anasema wanawake pia hujihusisha na biashara ya kusuka nywele na kuuza nguo.
“Wakinamama tunanufaika sana na utalii kwa sababu huwa tunauza nguo kama batiki na kuwasuka nywele watalii wanaotembelea kijiji chetu na kupata takriban Dola 15 za Kimarekani (Sh24,000) hadi 20 (32,000) kwa kichwa,” anasema Mtumwa.
Wakati baadhi wakilalamikia ukosegfu wa ajira kwenye hoteli za kitalii kwa madai kuwa zinatolewa kwa upendeleo kwa wageni badala ya wazawa, Zakaria Juma, meneja mkuu wa hoteli ya Karafuu, anapingana na hoja hiyo.
“Kama hapa hotelini kwangu kuna jumla ya wafanyakazi 200 na kati yao, ni wageni wanne tu kutoka Kenya, waliobaki wote ni Watanzania kutoka Bara na Visiwani,” anajitetea Juma.
“Mpishi Mkuu wa hii hoteli ni mwenyeji wa hapa hapa kijiijini (Michamvi) na alianza kama mhudumu wa bustani, lakini tumempa mafunzo mpaka kawa tegemeo la hoteli yetu na zile za jirani kwa upishi bora,” anasisitiza.
Anaongeza kuwa asilimia kubwa ya wafanyakazi wa kada za chini walipewa mafunzo hotelini hapo.
Juma aliuambia msafara wa Benki ya Dunia uliomtembelea kuwa ukosefu wa maji safi na salama ni changamoto kubwa katika uendeshaji wa biashara yake.
“Kukosekana kwa maji kumetufanya tufunge mashine za kuchuja maji ya bahari ili kuwa safi kwa matumizi ya binadamu,” anasema.
Hoteli ya Karafuu ni miongoni wa hoteli za kwanza kusini mwa Unguja ambayo ilijengwa wakati eneo hilo likiwa na changamoto kubwa ya barabara.
Kwa mujibu wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, kwa sasa visiwa hivyo vina zaidi ya hoteli 370, lakini asilimia kubwa ni za kiwango cha chini ukilinganisha na idadi ya hoteli za nyota tano.
Sekta ya utalii inakuwa kwa kasi Zanzibar na ukuaji unachangia asilimia 80 ya fedha za kigeni na takriban asilimia 30 katika pato la taifa. Kilimo cha Karafuu kinachagia asilimia 45 kikifuatiwa na sekta nyingine za uvuvi na biashara.
Kwa mujibu wa tovuti ya SMZ, sekta ya utalii imekuwa ikikua kwa asilimia 9.6 na ifikapo 2020 karibu nusu ya idadi ya Wazanzibar watakuwa wakijiuhusisha na sekta hiyo.
Uchangamkiaji hu wa fursa, pia unathibitishwa na Wayne Biger, raia wa Marekani aliyeenda Zanzibar kutembelea kwa mara pili baada ya kutalii kwa mara ya kwanza mwaka 1996.
“Sikuwahi kufikiri kama siku moja ningerudi tena visiwani humu kwa ajili ya utalii kutokana miundombinu kuwa mibaya,” anasema Biger akionekana kufurahishwa na uboreshwaji wa miundo mbinu.
“Nilikuja Tanzania mwaka 1996 na nilitembelea Zanzibar ambayo ilikuwa tofauti kabisa na hii ninayoiona. Hakukuwa na hoteli nyingi kama sasa na barabara nyingi zilikuwa za vumbi na mbovu sana,” anaongeza.
“Safari hii nimerudi tena na najisikia furaha sana ukizingatia wenyeji wa siku hizi ni wachangamfu sana kuliko wa kipindi kile.” Anasema alipofika Mji Mkongwe alichukua taxi ambayo ilimpeleka mpaka Nungwi mkoani Kaskazini Unguja kwa kutumia muda usiopungua masaa sita, ndani ya takriban kilomita 60 tu. Kwa sasa kwenda eneo hilo ni mwendo wa nusu saa hadi saa moja.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Dk. Idrissa Hija anasema licha ya hatua hiyo ya maendeleo iliyofikiwa, bado kuna changamoto lukuki zinawakabili ikiwemo kuhakikisha vijana wanapata ajira za kutosha.
“Katika mkoa wangu, vijana ambao wamekuwa wakifanya kazi katika sekta ya utalii ni asilimia 35 tu; hivyo tunaendea kuboresha huduma za kijamii kama umeme, maji na barabara ili waliobaki watumie fursa ya biashara nyingine zinazohusiana na utalii,”
Katibu mkuu wa Wizara ya Fedha Zanzibar, Khamis Omar anasema ni kweli kuna mafanikio katika kupambana na umaskini, lakini bado asilimia 44 ya wananchi visiwani humo wanaishi katika umaskini wa kutupwa.
Anaongeza kuwa kwa sasa serikali inaendelea kuboresha miundombinu kama barabara na umeme ili kukuza uwekezaji hususan wa utalii na viwanda.
Kwa sasa bado idadi ya wananchi waliojiunga na huduma za umeme ni ndogo kwa asilimia 40 tu, huku wale wenye wa uwezo wa kupata nishati hiyo ni asilimia 85.
Uwanja wa ndege kukuza utalii
Omar anasema kuwa Serikali kwa ushirikiano na Benki ya Dunia inamalizia mradi wa upanuzi na ujenzi wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume kama moja ya jitihada za kukuza sekta ya utalii na biashara.
Mradi huo ulihusisha upanuzi na ujenzi wa njia za kujiandaa ndege wakati wa kuruka na kutua pamoja na sehemu ya maengesho ya ndege.
Pia kuna mradi mwingine wa ujenzi wa jengo la abiria ambalo linajengwa kwa msaada wa Benki ya Exim ya China ambao nao ukikamilika utaufanya uwanja huo kuhudumia zaidi ya abiria 1.6 milioni kwa mwaka.
Kwa mujibu wa katibu mkuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano ya Zanzibar, Dk Juma Akil kwa sasa uwanja huo unakadiriwa kuhudumia abiria kati ya abiria 700,000 hadi 800,000. Dk. Akil anasema kukamilika kwa uwanja huo kutaongeza idadi kubwa ya watalii nchini kwa sababu utakuwa na uwezo wa kupokea ndege kubwa mpaka za kiwango cha code E ambazo zinahusisha ndege kama Boeing 777.
Pamoja na maendeleo ya kasi ya sekta ya utalii visiwani humu, bado matukio machache ya kiusalama yaliyotokea kwa nyakati tofauti yametia doa mafanikio hayo.
Mapema Agosti mwaka jana, watu wasiofahamika waliwamwagia tindikali wanawake wawili raia wa Uingereza waliokuwa wakifanya kazi ya kujitolea, kitendo kilichozua hofu miongoni mwa watali.
Hata hivyo afisa utalii mwandamizi wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Dk Miraji Ussi anasema Serikali ya Mapinduzi ina mpango wa kufunga kamera za usalama (CCTV) ili kuzuia na kung’amua wahalifu.
Ni dhahiri kuwa mpango huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na matukio ya uhalifu na hivyo kuifanya Zanzibar kuwa salama na kuvutia zaidi watalii, ambao kwa kiasi kikubwa watasaidia wazawa kujikita zaidi kwenye biashara na hivyo kuongeza pato lao na kupunguza makali ya umaskini.