Ajali ya basi yakatisha maisha wanachuo, wahadhiri 14

Muktasari:

  • Watu wasiopungua 14 wamfariki baada ya basi la Chuo Kikuu cha Pwani kugonga daladala katika eneo la Kayole Barabara ya Naivasha-Nakuru.

Dar es Salaam. Takribani watu 14 wakiwemo wanafunzi na wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Pwani kilichopo nchini Kenya wamefariki dunia baada ya basi walilokuwa wakisafiria kugonga daladala katika eneo la Kayole barabara ya Naivasha-Nakuru.

Ripoti zinasema basi hilo lilikuwa na takriban watu 30 ambao walikuwa wakielekea Eldoret katika chuo kingine kwa ajili ya kuhudhuria michezo.

Chanzo cha ajali inasadikiwa ni kufeli kwa breki, Mashuhuda wa ajali hiyo wamesema waliona basi hilo likigonga daladala maarufu kama ‘Matatu’ kisha kutumbukia mtaroni.

Ruth Wambui ambaye ni mmoja wa mashuhuda amesema basi lilipoteza mwelekeo baada ya kugonga basi abiria ‘matatu’ iliyokuwa ikiingia barabara kuu baada ya kuchukua abiria pembeni ya barabara.

“Dereva wa basi alipiga honi mara kadhaa huku likiwa linakaribia kwa kasi,” amesema Wambui.

Kwa mujibu wa Tovuti ya Taifa Leo ya nchini Kenya, Naibu Kamishna Kisilu Mutua amethibitisha tukio hilo.

“Hii ndiyo idadi ya hivi punde lakini ninaendelea kupata habari zaidi kutoka kwa maofisa wa polisi na vitengo mbalimbali vya hospitali zilizoko katika eneo hili,” amesema afisa huyo wa utawala.

Magari hayo mawili ambayo ni basi la chuo na matatu yalikuwa yakielekea upande mmoja wa barabara ya kwenda Nakuru.

Shughuli za uokoaji zinazoongozwa na Polisi na maofisa wa Kikosi cha Zimamoto cha Naivasha, kwa ushirikiano wa wananchi.