Aliyeua watu 10 naye akutwa amefariki

What you need to know:

  • Mwanaume mmoja aliyetekeleza mauaji ya watu 10 usiku wa kuamkia Jumapili Januari 22, amekutwa amejiua kwa kujipiga risasi kwenye gari aliokuwa akikimbia nayo.

California. Mwanaume mmoja mwenye umri wa miaka 72 nchini Marekani, amejiua kwa kujipiga risasi ndani ya gari wakati akiwakimbia polisi baada ya kutekeleza mauaji ya watu 10.

Mwanaume huyo alietambulika kwa jina la Huu Tran alitekeleza mauaji ya watu 10 na kujeruhi wengine 10 waliokuwa wanasherehekea sikukuu ya Lunar ambayo husherehekewa na watu wa China.

Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa mwanaume huyo alijaribu kufyatua risasi nyingine kwenye klabu tofauti dakika chache baada ya shambulizi la kwanza siku ya Jumamosi usiku.

Polisi walisema muuaji huyo ambaye alikuwa ni daktari wa kusafisha miili, alitumia bastola yenye uwezo wa juu kufyatua risasi kwenye ukumbi wa densi maarufu wa Monterey Park.

"Tran alijipiga risasi siku ya Jumapili polisi walipokaribia gari jeupe alilokuwa akiendesha huko Torrance, takriban maili 20 kutoka eneo la tukio huko Monterey Park," Polisi wamesema.

Maofisa walisikia mlio wa risasi kutoka ndani ya gari hilo walipokuwa wakikaribia, kisha wakarudi nyuma kumbe alikuwa anajiua.

Kati ya watu 10 waliojeruhiwa, saba walisalia hospitalini Jumapili usiku, na mmoja wao alikua katika hali mbaya.