Biden, Xi Jinping wawekana sawa

Rais wa Marekani, Joe Biden na Xi Jinping wa China wakisalimiana walipokutana kwa mara ya kwanza tangu kila mmoja achaguliwe kushika wadhifa huo mjini Bali, Indonesia wanapohudhuria mkutano wa G-20, juzi.

Muktasari:

  • Marais Joe Biden wa Marekani na Xi Jinping wa China wamefanya mkutano wa faragha wa ana kwa ana kwa mara ya kwanza tangu Biden awe Rais wa 46 wa Marekani.

Bali. Marais Joe Biden wa Marekani na Xi Jinping wa China wamefanya mkutano wa faragha wa ana kwa ana kwa mara ya kwanza tangu Biden awe Rais wa 46 wa Marekani.

Viongozi hao wanakutana kwenye mkutano wa viongozi wa mataifa 20 tajiri duniani unaofanyika mjini Bali nchini Indonesia kuanzia leo.
Biden aliwasili Bali juzi akitokea kwenye mikutano mingine, wa tabianchi (COP27) uliofanyika Sharm El Sheikh (Misri) na mkutano wa viongozi wa Muungano wa Mataifa ya Kusini-Mashariki mwa Asia (ASEAN) uliofanyika Phnom Penh, Cambodia.

Rais Xi Jinping ambaye hakuhudhuria mkutano wa COP27 na ule wa ASEAN aliwasili jana mchana na kukutana na Biden katika mkutano uliofanyika hoteli ya Mulia, Bali.
Viongozi hao wako Bali kuhudhuria mkutano wa viongozi wa kundi la nchi tajiri duniani (G-20).

Mara mwisho kukutana ana kwa ana ni wote walipokuwa makamu wa Rais katika nchi zao.
Mkutano wa jana umefanyika wakati mataifa hayo makubwa duniani uhusiano wao ukiwa kwenye hali ya sintofahamu.
Muda mfupi kabla ya mkutano huo, Biden alizungumzia umuhimu wa kuepuka mgogoro kati ya mataifa hayo mawili.

Hata hivyo, suala la Taiwan linaelezwa kuwa miongoni mwa ajenda ya mkutano huo ambapo China inadai Taiwan ni eneo la mamlaka yake.
Pia, viongozi hao wanatarajiwa kuzungumzia usalama wa uchumi wa dunia, suala la Korea Kaskazini, uvamizi wa Russia nchini Ukraine na pia kutuliza hofu ya China kuhusu ziara ya Spika wa Bunge la Marekani, Nancy Pelosi aliyoifanya Taiwan hivi karibuni.

Ziara hiyo ilishutumiwa na Jinping akiionya Marekani kutofanya mzaha na suala la Taiwan kwamba, kunaweza kuvuruga uhusiano wao.

Kwa mujibu wa maofisa wa Ikulu ya Marekani, Biden amekuwa akiruduia kwamba hataki mgogoro na Jinping na alimwambia Marekani na China zinaweza kumaliza tofauti zao, kuzuia ushindani utakaoziingiza kwenye mgogoro na kutafuta njia ya kufanya kazi pamoja.

Kwa upande wake Jinping naye alisema hali iliyopo siyo ile inayotegemewa na jumuiya ya kimataifa waione katika mataifa hayo.
Alisema wanahitaji kuwa na uhusiano mzuri kati ya China na Marekani kwa kuwa dunia iko njia panda.

Biden alianza ziara ya kujenga uhusiano wa kimataifa kwa kuhudhuria mkutano wa COP27 kisha ASEAN.
Kwa sasa wanakutana kwa ana wote wakiwa na mamlaka ya urais katika nchi zao.
Walikutana ana kwa ana wote wakiwa makamu wa Rais mwaka 2011 nchini China.

Lakini, pia waliwahi kukutana nchini Marekani.
Xi Jingping alikuwa makamu wa Rais wa sita wa China kuanzia mwaka Machi 14, 2013 hadi Machi 17, 2018.

Wakati Biden alikuwa makamu wa Rais wa 47 wa Marekani kuanzia mwaka 2009 hadi mwaka 2017, chini ya Rais wa 44 Barack Obama.
Tangu Biden aingine madarakani Januari 2021, viongozi hao wamezungumza mara tano kwa njia simu na video.

China na Marekani ambazo ni mahasimu wa kibiashara zimekuwa na uhusiano wenye shaka wakati wa utawala wa Rais wa 45 wa Marekani, Donald Trump.

Onyo la Biden
Mara baada ya kuchukua nchi akiwa ametimiza siku 100 madarakani, Aprili 2021 Biden alihutubia Bunge la Marekani kwa mara ya kwanza na akatumia nafasi hiyo kuionya China akisema Marekani haitakaa kimya wakati kampuni za kichina yakitishia usalama wa kampuni ya kimarekakani na hata ajira za raia wake.

Biden kwenye hotuba yake hiyo, aliweka wazi kuwa katika mazungumzo yake na Jinping alimueleza msimamo wake kuwa japo Marekani haitafuti mgogoro na China, lakini pia atalinda maslahi yake ya kibiashara kwa nguvu zake zote.

Machi 2021, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken aliielezea China kama, ndiyo nchi pekee inayoweza kuipa changamoto Marekani katika anga za kimataifa kwenye nyanja za uchumi, diplomasia na teknolojia.