Bunge la Nigeria lagoma kununua boti ya kifahari ya Rais

Muktasari:

  • Baraza la Wawakilishi nchini Nigeria, limebatilisha maombi ya manunuzi ya boti ya kisasa kwa ajili ya Rais wa nchi hiyo, na badala yake fedha hizo zimeelekezwa katika kuongezwa mikopo kwa ajili ya wanafunzi, na kuuwezesha mfuko huo, kuongezeka mara mbili.

Dar es Salaam. Baraza la Wawakilishi nchini Nigeria, limeugomea mpango wa Serikali kununua boti ya kifahari (Yatch), kwa ajili ya matumizi ya Rais wa nchi hiyo, yenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 6, sawa na makadilio ya Sh15 bilioni.

Hayo yamebainishwa jana Alhamisi 2, 2023; na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Matumizi, Abubakar Bichi, alipokuwa akizungumza na wanahabari baada ya kupitishwa kwa Muswada wa Matumizi ya Fedha wa 2023.

Bichi, ambaye ni mwanachama wa chama tawala cha Rais Tinubu, amesema wabunge hawakuwa tayari kupitisha bajeti kwa ajili ya boti hiyo na badala yake, wamehamisha fedha hizo (dola milioni 6) na kuziongeza katika bajeti ya mikopo ya wanafunzi.

“Hakuna bajeti kwa ajili ya manunuzi ya Yacht ya Rais, kwa sababu fedha hizo zimeongezwa kwenye bajeti ya mikopo kwa nafunzi ambao umeongezeka kutoka N5 bilioni hadi N10 bilioni,” amesema Mbunge Bichi.

Kwa mujibu wa viwango vya ubadilishaji fedha, Naila 5 bilioni, inakadiriwa kuwa kama Sh15.8 bilioni.

BBC imeripoti kuwa Wanigeria wameutaja mpango huo kama ni “Matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi” kwa kile walichokiita “mambo ya anasa,” hasa katika kipindi hiki ambapo kuna mgogoro wa kiuchumi.

Wakati anaingia madarakani mwezi Mei mwaka huu, Rais wa nchi hiyo Bola Tinubu alikuja na ahadi ya kuondoa ufisadi na kuboresha hali ya maisha ya watu wake kwa kuweka mazingira mazuri ya uchumi wa Wanigeria.

Hata hivyo mzozo huu unakuja wakati ambapo Rais huyo anakabiliwa na shinikizo kubwa kutokana na kupanda kwa gharama za maisha, huku sarafu ya nchi ikiporomoka dhidi ya dola ya Marekani.

Malalamiko yalianza kusikika baada ya Serikali kuliomba bunge kuidhinisha bajeti ya ziada, huku mununuzi ya boti hiyo yakiorodheshwa kama sehemu ya bajeti ya matumizi ya Jeshi la Wanamaji, yenye kufikia dola za Kimarekani milioni 53 (karibu Sh132 trillioni).

Mwanaharakati wa haki za binadamu na aliyekuwa Mbunge Shehu Sani ambaye amesema "Maskini hawawezi kupambana kwa kuishi kwenye mashua wakati kiongozi wao anaendesha Yacht."

Hata hivyo, Temitope Ajayi ambaye ni Msemaji wa Rais Tinubu, amemtenga bosi wake na mipango hiyo akisema: “Kulingana na kile ninachokifahamu, maombi ya ununuzi wa Yacht, yaliyotajwa kwenye bajeti, yanatokana Jeshi la Wanamaji, hivyo ni lazima sababu za kwa nini inahitajika."

Aidha, bajeti hiyo ziada, pia inametenga dola milioni 36 kwa matumizi ya Ikulu, ikiwa ni pamoja na ununuzi wa magari ya kisasa na ujenzi wa jengo la ofisi la Rais. Serikali pia imepanga kutumia dola milioni 15 (karibu Sh37.4 trilioni) kwa ajili ya ndege ya Rais.

Hata hivyo, Ajayi amesema Rais na makamu wake, hawana nia ya kuongeza magari mapya kwenye misafara yao na kwamba wanatumia magari yaliyoachiwa na utawala uliopita.

Taasisi inayosimamia mradi wa haki za kijamii na kiuchumi na uwajibikaji (Serap), imesema manunuzi ya boti hayawezi kuhalalishwa wakati kuna Wanigeria milioni 137 wanaishi katika umaskini mkubwa.

Wachambuzi wa siasa nchini humo, wameeleza kuwa uzito wa hali mbaya ya maisha ya Wanigeria, umeongezeka baada ya Serikali ya Tinubu kuondoa ruzuku ya mafuta, jambo ambalo lililosababisha bei ya bidhaa hiyo na nyingine za msingi kupanda.

Mwanaharakati Omoyele Sowore ameilamu, Serikali kwa kutumia pesa kwa anasa wakati inaendelea "kudumisha mateso ya wananchi wa Nigeria."


Imeandaliwa na Mwandishi wetu kwa msaada wa mashirika.