Changamoto mbili zinazomkabili Rais mpya Nigeria

Rais mpya wa Nigeria, Bola Tinubu.

What you need to know:

  • Bola Tinubu alitangazwa kuwa mshindi katika Uchaguzi Mkuu wa Februari 25, 2023 kwa kupata kura milioni 8.8 na kutimiza idadi ya kura inayohitajika kisheria ya theluthi mbili katika majimbo yote ya Nigeria.

Abuja. Mwanasiasa mkongwe, Bola Tinubu ameapishwa leo Mei 29, 2023 kuwa Rais mpya wa Nigeria wakati Taifa hilo lenye watu wengi zaidi barani Afrika likipita kwenye changamoto za kiuchumi na kuzorota kwa usalama nchini humo.

Raia huyo anatoka eneo la kusini, akiwa na umri wa miaka 71, na pia anatoka chama kimoja na Rais aliyemaliza muda wake wa mihula miwili, Muhammadu Buhari (80) ambaye anatoka eneo la kaskazini na ni jenerali wa zamani wa jeshi.

Hafla ya kuapishwa kwa Tinubu imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Afrika wakiwemo Rais Samia Suluhu Hassan (Tanzania), Paul Kagame (Rwanda), George Weah (Liberia) pamoja na wawakilishi wa mataifa mengine kutoka nchi tofauti duniani.

Tinubu alitangazwa mshindi wa uchaguzi mkuu wa Februari 25, 2023 kwa kura milioni 8.8 na kutimiza idadi ya kura inayohitajika ya theluthi mbili katika majimbo ya Nigeria.

Kiongozi mkuu wa upinzani, Atiku Abubakar, aliyeshika nafasi ya pili na Peter Obi, aliyekuwa wa tatu, wanapinga matokeo hayo mahakamani, wakidai udanganyifu.

Tume ya uchaguzi ilikubali makosa wakati wa kura lakini ikapuuza madai kwamba mchakato huo haukuwa huru na wa haki.

Tinubu anayejulikana kama “godfather” wa siasa za Nigeria aliendesha kampeni zake akisema “Ni zamu yangu” kutawala nchi yenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika, akijivunia uzoefu wake kama Gavana wa Lagos kuanzia mwaka 1999 hadi 2007.

Wengi wanasema mwanasiasa huyo mahiri amesaidia kulifanya Jiji la Lagos kuwa la kisasa na wanatumaini kuwa atakuwa na mchango mkubwa kwa taifa zima.

Hata hivyo, Rais huyo aliyeingia madarakani anakabiliwa na tuhuma za ufisadi, ingawa amekuwa akikanusha kila wakati, pamoja na maswali kuhusu afya yake.

Buhari aliahidi kukabiliana na ufisadi na kudorora kwa usalama lakini aliwakatisha tamaa wengi, kwa mujibu wa wachambuzi, akiacha madeni yakiwa yameongezeka, mfumuko wa bei na kukithiri kwa ukosefu wa usalama.

Urais wake ulionyesha kwamba “inawezekana kwa mtu anayeaminika na wengi kuwa hawezi kuhongwa, kuongoza taifa ambalo linatambulika kwa rushwa na kukosekana kwa weledi kazini,” alisema Ebenezer Obadare wa Baraza la Uhusiano wa Kimataifa, taasisi ya wasomi yenye makao yake mjini Washington.

“Pamoja na serikali inayokuja ya Bola Tinubu,” Obadare aliandika kwenye blogu, “Wanigeria hivi karibuni watajua kama kiongozi anayeonekana kama fisadi anaweza kuongoza taifa na kumaliza ufisa ma kuongeza ufanisi wa kutosha.”

Wanaume hao wawili wanaweza kuwa tofauti kimtindo na sifa, lakini pia wana mambo yanayofanana, kama vile kushikamana kwao na Uislamu katika nchi iliyogawanyika kati ya Wakristo na Waislamu na pia umri wao mkubwa.

Buhari alifanya safari za matibabu mara kwa mara nchini Uingereza alipokuwa Rais, wakati Tinubu naye alitumia muda wake nje ya nchi wakati wa kampeni na kati ya uchaguzi na kuapishwa.

Kwa uvumi kuhusu afya yake, macho yamegeukia kwa Makamu wa Rais mpya, Kashim Shettima, ambaye ni gavana wa zamani wa jimbo la Borno kaskazini, mwenye umri wa miaka 56.

Baada ya uapisho huo, Serikali mpya itakuwa na kazi nyingi za haraka, kuanzia na uchumi.

Moja ya changamoto kuu kwa Nigeria yenye utajiri wa mafuta ni kwamba inabadilisha mafuta ghafi yenye thamani ya mabilioni ya dola kwa petroli ambayo inatoa ruzuku kwa soko lake la ndani.

Hii imesababisha upungufu mkubwa wa mapato yaa fedha za kigeni na kuchangia katika kuongezeka kwa deni.

Zaidi ya watu milioni 80 kati ya watu milioni 210 nchini humo wanaishi chini ya mstari wa umaskini, kwa mujibu wa Benki ya Dunia, na Umoja wa Mataifa umeonya kwamba zaidi ya robo ya watu hao wanakabiliwa na njaa kali mwaka huu.

Licha ya sekta zinazostawi za teknolojia na burudani, Wanigeria wengi wa tabaka la kati wanakimbilia ng'ambo wakitarajia kupata maisha mzuri zaidi.