Hekalu la maovu la kiongozi wa Wagner

Kikulacho ki nguoni mwako, ndivyo unavyoweza kusema juu ya kilichomtokea kiongozi wa kundi la Wagner, Yevgeny Prigozhin alikwama kumpindua Rais wa Russia, Vladimir Putin wiki mbili zilizopita.

Kundi hilo lililojipambanua kulinda masilahi ya Russia limekuwa likisaidiwa na Serikali ya nchi hiyo kukabiliana na watu wanaoipinga, ikiwemo nchi ya Ukraine inayopigana vita, sasa lina hali ngumu ya kufanya shughuli zake baada ya jaribio la kumng’oa Rais Putin kugonga mwamba.

Kasri la Prigozhin, lililopo katika jiji la St Petersburg ambalo ni la nne kwa kuwa na watu wengi barani Ulaya, limevamiwa na maofisa wa polisi wanaodaiwa kuagizwa na Rais Putin.

Gazeti la ‘Izvestia’ jana lilichapisha picha na video za maofisa wa usalama wa Russia wenye silaha wakipekua kasri la kifahari la Prigozhin alipokuwa uhamishoni nchini Belarus, Juni 24.

Maofisa hao walikuta silaha nyingi za kivita, hazina ya dhahabu, mamba aliyekaushwa, fremu yenye picha za vichwa vilivyokatwa inavyodaiwa ni vya maadui wa kiongozi huyo wa kijeshi.

Picha zilizoonyesha kwenye uvamizi huo ni pamoja na kabati kubwa lililo na nywele nyingi tofauti za bandia (wigi) za mitindo na rangi tofauti, kuanzia rangi ya kijivu hadi hudhurungi.

Picha nyingi zilizoonekana zinadaiwa kumwonyesha Prigozhin akiwa amevalia wigi kama sehemu ya mavazi tofauti zilivuja kwenye mitandao ya kijamii ya Russia.

Ubora wa baadhi ya mavazi ya kujificha ni wa kuchekesha na hivyo kuzua uvumi kuwa inawezekana zimechezewa ili kumvunjia heshima kiongozi huyo wa Wagner.

Hata hivyo, wafuasi wa Prigozhin walisema kuvuja kwa picha hizo kunaweza kuwa kumekiuka sheria kali za usalama wa Taifa za Russia, wakisema kiongozi wao alikuwa akifanya kazi ya uwakala wa serikali, kutokana na uhusiano wa Wagner na idara ya ujasusi ya kijeshi ya Russia, GRU.

Hali hii imekuja ndani ya wiki mbili baada ya mbabe huyo wa kivita kuanzisha kile kilichoonekana kuwa uasi wa kutumia silaha dhidi ya Putin ambao ulisitishwa punde baada ya Rais Alexander Lukashenko wa Belarus kusimamia makubaliano ya kumaliza mzozo huo.

Rais Lukashenko jana alidai kuwa kuwa Prigozhin amerejea St. Petersburg, ingawa haijulikani yuko eneo gani la huku wapiganaji wake wengi wakiwa wamepiga kambi katika ardhi ya Belarus.

Inadaiwa bilionea Prigozhin alitumia mbinu za kujificha barani Afrika na Mashariki ya Kati alipokuwa akiendeleza masilahi ya Putin na kupeleka huko vikosi vya Wagner.

Nyundo kubwa yenye maandishi "Kwa ajili ya matumizi katika mazungumzo muhimu" ilipigwa picha katika chumba cha mapokezi cha kasri hilo karibu na meza ya snuka (mchezo wa kugonga tufe mezani).

Idadi kubwa ya masanduku yenye noti za Russia zenye thamani ya Rubble 10 bilion (Sh268 bilioni za Tanzania) pia yalikamatwa katika uvamizi wa mali ya Prigozhin, ambayo ni pamoja na jengo la ofisi yake.

Vyombo vya habari vya Russia vinaripoti kuwa fedha na vifaa hivyo vimerudishwa Kituo cha Wagner.

Prigozhin aliwahi kusema kuwa Wagner inashughulika na fedha taslimu pekee kulipa gharama za shughuli zake. Putin, kwa upande mwingine, aliwahi kusema serikali ilimfadhili Wagner.

Miongoni mwa mali muhimu za kiongozi huyo wa kijeshi zilizopigwa picha katika kasri lake la kifahari ni sare ya kijeshi ya Russia iliyopambwa kwa medali karibu dazeni mbili.

Pia kwenye onyesho la nyumba yake ya kifahari ni kile kinachoonekana kuwa mamba aliyekaushwa kwenye meza ya mavazi.

Hati kadhaa za kusafiria pia zilipatikana na kupigwa picha ndani ya jumba hilo.

Hati hizo zina majina tofauti na sura tofauti za mtu yule yule mmoja ambaye alijigeuza sura kwa kuvaa mawigi na wakati mwingine ndevu za bandia.

"Mtu wa kawaida hawezi kuwa na pasipoti nyingi," Eduard Petrov alisema, ambaye ni mwandishi wa habari aliyeshuhudia uvamizi huo.

"Kwa nini mtu huyu alikuwa na nguvu za ajabu kama kiongozi makini wa aina fulani ya kundi la uhalifu?" aliuliza.

"Tunahitaji kupata undani wa nani alikuwa upande wa nani (katika uasi). Tunahitaji kuwaadhibu na kuwafungulia mashtaka."

Video iliyowekwa mitandaoni inaonyesha maofisa waliojihami kwa bunduki wakipekua nyumba na ofisi zake.

Picha pia zinaonyesha nyumba kubwa ya kifahari ambayo Prigozhin anaishi ina bwawa binafsi la kuogelea, helikopta, bafu la mvuke, ukumbi wa michezo na chumba cha matibabu.

Nyumba hiyo pia inaonekana kuwa na chumba binafsi cha kufanyia sala kilichojaa picha zinazohusu mambo ya dini.

Katika maoni yake ya kwanza tangu uhamisho wake, mapema wiki hii Prigozhin aliapa kuwa wapiganaji wake hivi karibuni watapata "ushindi mpya", huku picha zikiibuka za kambi mpya ya mamluki hao huko Belarus.

Prigozhin alisema katika ujumbe mfupi wa sauti uliotumwa Jumanne iliyopita kwenye chaneli ya Telegram ya Greyzone inayohusishwa na Wagner:

"Na nadhani tulifanikiwa katika mengi ya haya. Katika siku za usoni, nina hakika kwamba utaona ushindi wetu ujao mbele".

Katika video hiyo, Prigozhin hakutoa kidokezo kuhusu sehemu aliyopo, huku video hiyo ikiwa ni rekodi ya sauti tofauti na ujumbe wake wa kawaida anaotoa mara kwa mara kwa njia ya video.

Ni jambo lililozoeleka kwa kiongozi huyo kuhutubia vikosi vyake kwa njia ya video kabla ya jaribio lao la uasi lililoshindwa Juni 24.

Vyombo vya habari vya Serikali ya Russia viliwahi kumsifu kiongozi huyo na wapiganaji wake kwa kampeni yao kali nchini Ukraine, lakini vilimkosoa kwa hisia zake za usaliti kwa Rais Putin alipojaribu kumpindua.

Tangu jaribio hilo lishindwe, vyombo hivyo vimeacha kutangaza habari za kundi la Wagner na hali ya Prigozhin.


Tuhuma za Putin

Juni 24, mwaka huu, Rais Putin aliingia katika kile kilichoonekana kuwa ni mzozo kati ya serikali yake na jeshi binafsi la Wagner akilituhumu kwa usaliti na uhaini baada Prigozhin kuanzisha kile kilichoitwa uasi dhidi ya serikali na kutuma wapiganaji wake kuelekea Moscow.

Lakini kabla siku hiyo haijamalizika, wakiwa umbali mfupi kufika Moscow, Prigozhin alibadilisha mwelekeo huo na kuwaamuru wapiganaji wake kurejea kambini.

Baadaye siku hiyo Prigozhin alisisitiza kuwa hayo yalikuwa "maandamano ya haki" na si mapinduzi. Lakini vyovyote ilivyokuwa, yaliisha haraka sana kama yalivyoanza.

Zilikuwa ni saa 24 za taharuki kwa serikali ya Russia. Ndani ya muda wa siku moja tu, matukio yaliongezeka na yakapungua haraka kama yalivyoanza. Ndani ya siku hiyohiyo Wagner walikomesha uasi waliouanzisha wao wenyewe.


Uhusiano na Rais Putin

Kwa muda mrefu Prigozhin amekuwa mshirika wa karibu sana wa Rais Putin na kundi lake limestawi sana chini ya utawala Putin. Wapiganaji wa Wagner wamekufa kwa wingi katika mapambano makali ya kuiteka Bakhmut mashariki mwa Ukraine, ambayo yalidumu kwa miezi kadhaa na hayakufanikiwa.

Uhusiano wa wawili hao inaaminika ndio uliochagiza Prigozhin kupelekwa uhamishoni huko Belarus ikiwa ni sehemu ya makubaliano waliyofikia chini ya usimamizi wa Rais Lukashenko wa Belarus.

Katika makubaliano hayo, kiongozi huyo wa Wagner alikubali kwenda Belarus ili asishtakiwe kwa uhaini.


NATO kujiandaa

Viongozi kutoka wanachama 31 wa muungano wa kijeshi wa NATO watakutana katika mji mkuu wa Lithuania Julai 11-12 mwaka huu kujadili mabadiliko yanayoendelea ya NATO na kukubaliana kuhusu mipango mipya ya kikanda ya kuimarisha ushirikiano miongoni mwa wanachama na ulinzi ili kukabiliana na vitisho vipya vya kundi la Wagner.

Siku moja baada ya kushindwa kwa uasi, Lord Dannatt, mkuu wa zamani wa Jeshi la Uingereza, alielezea wasiwasi wake kuwa huenda Prigozhin anajiandaa tena kuongoza shambulio dhidi ya Kyiv kutokea Belarus.

Akiongea na kipindi cha 'Sophy Ridge On Sunday' cha kituo cha runinga cha 'Sky News', alisema: 'Inaonekana ameondoka kwenda Belarus lakini je, huo ndio mwisho wa Prigozhin na Wagner Group? Ukweli kwamba amekwenda Belarus nadhani linanipa wasiwasi fulani ... Tusichokijua, tutakachogundua katika saa na siku zijazo ni ... wapiganaji wangapi wamekwenda naye..."

Aliendelea kusema; “Ingawa inaweza kuonekana kuwa suala hili limeisha, nadhani halijaisha, na mitetemeko ya baadaye itarejea na itachukua kwa muda mrefu. Wao (Ukraine) wanahitaji kuwa waangalifu sana kuhusu mashambulizi mapya kutoka upande wa Belarus."

Vyovyote vile itakavyokuwa, si tu kwamba uhusiano wa Wagner na jeshi la Russia hautakuwa tena kama ulivyokuwa awali, bali pia hata uhusiano wa Rais Putin na Yevgeny Prigozhin hautakuwa imara kama ulivyokuwa kabla ya jaribio la mapinduzi kukwama.