Wagner inavyotishia usalama barani Ulaya

Katika toleo lililopita tuliona uhusiano uliopo kati ya kundi la jeshi la mamluki la Wagner linaloongozwa na Yevgeny Prigozhin na namna linavyoshirikiana na jeshi la Russia.

Lakini Juni 24 mwaka huu, baada ya Prigozhin kutangaza kuandamana kutoka Ukraine kuelekea jiji la Russia la Rostov-on-Don, idara ya usalama ya Taifa ya nchi hiyo, FSB ilisema imefungua mashtaka ya jinai dhidi yake na kuamua kumkamata.

Inadaiwa kuwa mazungumzo na Rais wa Belarus, Alexander Lukashenko yalipunguza kasi ya mapinduzi hayo na Prigozhin alipaswa kuondoka Russia kwenda Belarus kwa sharti la kufutwa kwa mashtaka dhidi yake.

Je, Prigozhin alikwenda Belarus? Aliondokaje Russia? Mashtaka dhidi yake yalifutwa? Nini kiliendelea baada ya hapo?

Juni 28 Rais Lukashenko alithibitisha kuwa ni kweli Prigozhin na watu wake aliwasili nchini humo na akasema amewapa eneo la kijeshi lililotelekezwa ambapo wangeweza kuweka mahema yao huku wakifikiria nini cha kufanya, na kwamba yeyote ambaye anataka kujiunga nao anaweza kufanya hivyo, lakini akitambua ‘hatari ya kifo’ kwa kazi hiyo.

Akizungumzia sababu za maasi hayo, kiongozi huyo wa Belarus alisema ni mgogoro kati ya Waziri wa Ulinzi wa Russia, Sergei Shoigu na Prigozhin ulioongezeka na kuwa mbaya zaidi.

Kwa mujibu wa vyombo mbalimbali vya habari, Rais Lukashenko amewaalika mamluki wa Wagner kutoa mafunzo ya kijeshi nchini mwake.

Kulingana na shirika la habari la serikali, Belta, Lukashenko alidokeza mwaliko huo katika hotuba aliyoitoa siku ya uhuru wa Belarus iliyoadhimishwa Ijumaa ya juzi.

"Kwa bahati mbaya, wao (mamluki wa Wagner) hawapo,” Lukashenko alisema. “Na ikiwa wakufunzi wao, kama nilivyowaambia tayari, watakuja na kutupa uzoefu wa mapigano, tutakubali.”

Wagner wamepokea tuzo mbalimbali za Serikali katika mfumo wa nishani za kijeshi na vyeti vilivyotiwa saini na Rais Vladimir Putin wa Russia.

Makamanda wa Wagner, Andrey Bogatov na Andrei Troshev walipewa tuzo ya shujaa wa Shirikisho la Russia kwa kusaidia kuliteka jiji la Palmyra nchini Syria kwa mara ya kwanza Machi 2016.

Bogatov alijeruhiwa vibaya katika vita hivyo. Wakati huo huo, Alexander Kuznetsov na Dmitry Utkin waliripotiwa kushinda tuzo ya ujasiri mara nne.

Utkin ni mwanzilishi mwenza wa kundi la Wagner, akishirikiana na Prigozhin.

Wanafamilia wa kundi hilo waliouawa pia walituzwa medali na Wagner mwenyewe, huku mama wa mpiganaji mmoja aliyeuawa akipewa medali mbili, moja ya ‘ujasiri na ushujaa’ na nyingine ya ‘damu na ushujaa’.

Wagner pia walipewa nishani ya kufanya operesheni nchini Syria.

Mwishoni mwa Januari 2018, Syria kulijengwa mnara kwa heshima ya wapiganaji wa Russia waliojitolea.

Maandishi kwenye mnara huo yameandikwa kwa maneno ya Kiarabu yanayosomeka: "Kwa watu wa kujitolea wa Russia, waliokufa kishujaa katika ukombozi wa maeneo ya mafuta ya Syria kutoka kwa ISIL". Mnara huo ulijengwa katika kiwanda cha Haiyan, takribani kilomita 50 kutoka Palmyra, ambapo Wagner walikuwa wakifanya shughuli zao za kivita. Mnara mwingine kama huo pia ulijengwa huko Luhansk Februari 2018.

Pia kuna mnara mwingine ulijengwa mbele ya kanisa lililo karibu na Goryachy Klyuch, Krasnodar Krai, nchini Russia, ambalo liko kilomita chache kutoka kituo cha mafunzo cha Wagner huko Molkin.

Uongozi wa Kikundi cha Wagner na wakufunzi wake wa kijeshi waliripotiwa kualikwa kuhudhuria gwaride la kijeshi Mei 9, 2018, kwenye maadhimisho ya ‘Siku ya Ushindi’. Hofu iliyoko sasa katika maeneo kadhaa ya Ulaya ni kwamba kundi la Wagner, ambalo limehamia Belarus, linaweza kutumia watu kutoka Afrika na maeneo mengine kuvuruga Ulaya ya Kati na Mashariki.

Juzi Alhamisi, nchi za Umoja wa Ulaya (EU), zinazopakana na Belarus ziliomba mshikamano zaidi kutoka kwa jumuiya hiyo na Jumuiya ya Kujihami ya Mataifa ya Magharibi (Nato), dhidi ya kundi la Wagner na hatari ya "kujipenyeza" katika nchi zao.

"Tunaangalia kila kitu kinachoendelea Belarus na Prigozhin na idadi isiyojulikana ya wapiganaji waliofunzwa sana na wenye ujuzi ambao labda watajiunga naye," Waziri Mkuu wa Latvia, Arturs Krisjanis Karins aliwaambia waandishi wa habari baada ya kuwasili kwenye kilele cha mkutano wa siku mbili wa viongozi wa EU mjini Brussels.

"Hilo linaweza kuwa tishio. Tishio hilo pengine lisiwe la makabiliano ya moja kwa moja ya kijeshi, lakini la jaribio la kujipenyeza Ulaya kwa madhumuni yasiyojulikana. Kwa hiyo tunahitaji kuongeza ufahamu wetu wa mpaka na kuhakikisha kwamba tunaweza kudhibiti hilo," alisema.

Inasemekana kuwa Prigozhin alikubali kwenda Belarus ili aepushwe na mashtaka ya uhalifu, ingawa Wizara ya Ulinzi ya Russia pia imetoa wito kwa wapiganaji wa Wagner kujiunga na jeshi la Russia.

Baadhi ya vifaa vyao vya kijeshi vilikamatwa na jeshi la Russia.

Viongozi kutoka wanachama 31 wa muungano wa kijeshi wa Nato watakutana katika mji mkuu wa Lithuania Julai 11-12 mwaka huu, kujadili mabadiliko yanayoendelea ya Nato.

Pia kukubaliana kuhusu mipango mipya ya kikanda ya kuimarisha ushirikiano miongoni mwa wanachama na ulinzi ili kukabiliana na vitisho vipya.

Lakini kwa nini Wagner wanaonekana kuwa tishio? Ziko sababu nyingi, lakini mbili ni kubwa.

Kwanza, katika muda wa saa chache tu Juni 24 mwaka huu, Wagner waliudhibiti mji mzima wa Rostov-on-Don nchini Russia.

 Kisha walituma msafara wenye silaha nzito kuelekea Kaskazini, ukisimama umbali wa kilomita 200 tu kutoka Moscow na kudaiwa kuangusha ndege za kijeshi za Russia.

Hii ilikuwa changamoto kubwa kwa utawala wa Rais Putin.

Kwa kifupi, ilikaribia kuanzisha vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vingeweza kuwa janga katika nchi yenye silaha kubwa zaidi, zikiwamo za nyuklia.

Pili, Wagner imekuwa kikosi cha kijeshi chenye ufanisi zaidi cha Russia nchini Ukraine.

Wanajeshi wake, wanaojumuisha maveterani wa kazi na wafungwa, mara nyingi wanalipwa vizuri na wana ari kuliko jeshi la kawaida. Kwa maana hii, Ulaya lazima iwe na hofu.

Tangu kilipofanyika kile kilichoonekana kama uasi dhidi ya Serikali ya Putin na hatimaye Rais Lukashenko wa Belarus kuingilia kati, na baadaye Prigozhin kukubali kwenda uhamishoni Belarus Jumanne iliyopita. Si tu kwamba uhusiano wa Wagner na jeshi la Russia hautakuwa tena kama ulivyokuwa awali, bali pia hata uhusiano wa Rais Putin na Yevgeny Prigozhin hautakuwa kama ulivyokuwa awali.