Israel yashambulia kiwanda muhimu cha kemikali Iran
Muktasari:
- Israel imesema ilikilenga kiwanda cha petrokemikali cha Mahshahr, huku ofisa wa jimbo hilo akiliambia Shirika la Habari la Fars kuwa sehemu za mtambo huo ziliharibiwa.
Israel imesema imeishambulia mitambo ya kiwanda cha kemikali (petrochemical) kusini-magharibi mwa Iran pamoja na kufanya mashambulizi mengine dhidi ya malengo ya kijeshi, baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kuripotiwa kumtaka Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kujizuia kufanya mashambulizi zaidi.
Katika shambulizi la kwanza kulenga eneo la nishati ndani ya Iran tangu kusitishwa kwa mapigano Aprili 8, 2026, Israel imesema ilikilenga kiwanda cha petrokemikali cha Mahshahr, huku ofisa wa jimbo hilo akiliambia Shirika la Habari la Fars kuwa sehemu za mtambo huo ziliharibiwa.
Waasi wa Kihouthi wa Yemen wanaoungwa mkono na Iran wameapa kusitisha usafiri wa majini wa Israel katika Bahari Nyekundu, wakisema wao ndio waliohusika na shambulizi la kwanza la kombora dhidi ya Israel tangu makubaliano ya kusitisha mapigano, jambo lililifanya jeshi la Israel kuwasha mifumo yake ya ulinzi wa anga.
“Tunachukulia harakati zote za adui kuwa malengo halali ya kijeshi kwa majeshi yetu,” imeeleza taarifa ya Houthi.
Saa chache kabla ya hapo, Trump alisema mashambulizi mapya kati ya Israel na Iran hayataathiri mazungumzo ya amani yanayoendeshwa na utawala wake na Tehran, akiongeza kuwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, hafanyi uamuzi.
Trump amekuwa akiishinikiza Israel kusitisha mashambulizi yake nchini Lebanon ili kutoa nafasi kwa makubaliano ya kumaliza vita pana dhidi ya Iran, ikiwamo kumkosoa Netanyahu kwa lugha kali katika mazungumzo ya simu wiki iliyopita.
Hata hivyo, Jumapili iliyopita, Israel ilianzisha mashambulizi katika eneo la Beirut kwa mara ya kwanza tangu Marekani itangaze mpango wa usitishaji mapigano nchini Lebanon wiki iliyopita.
Iran nayo ilijibu kwa kurusha makombora kadhaa kuelekea Israel, lakini Trump alisisitiza kuwa makubaliano ya kumaliza vita hivyo bado yanaweza kufikiwa.
“Haitakuwa na athari yoyote kwa makubaliano hayo,” Trump aliliambia gazeti la Financial Times. “Mimi ndiye ninayeamua. Mimi ndiye ninayeamua kila kitu. Yeye (Netanyahu) hafanyi uamuzi.”
Saa chache baadaye, jeshi la Israel lilisema limevishambulia vituo vya kijeshi vya Iran. Walinzi wa Mapinduzi wa Iran nao walisema Israel ilitumia makombora ya masafa marefu yaliyorushwa kutoka angani katika mashambulizi yake.
Iran ilirusha makombora 11 ya balistiki kuelekea Israel, balozi wake nchini Marekani, Yechiel Leiter alisema kupitia mtandao wa X, “Kila mtu amechoshwa na utawala huu wa kichaa wa Iran.”