Baharia aliyeuawa shambulio la bomu Hormuz azikwa Musoma
Waombolezaji wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa baharia mtanzania, Nchama Maregesi aliyefariki dunia baada ya meli aliyokuwa akifanya kazi kushambuliwa katika mfereji wa Hormuz.
Muktasari:
- Baharia huyo alifariki dunia akiwa kwenye meli iliyokuwa safarini kuelekea Oman ikitokea UAE iliposhambuliwa wakati ikivuka katika mlango wa bahari wa Hormuz katika eneo la kimkakati lililopo kati ya Iran na Oman.
Musoma. Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka ameongoza mamia ya wakazi wa mji wa Musoma na waombolezaji katika mazishi ya baharia Mtanzania, Nchama Maregesi aliyefariki dunia baada ya meli aliyokuwa akihudumu kushambuliwa na bomu katika mlango wa bahari wa Hormuz.
Maregesi alifariki dunia Mei 3,2026 baada ya meli ya kuvuta iitwayo Volans yenye namba za usajili ya Shirika la Kimataifa la Bahari (Imo) 929856 iliyokuwa ikipeperusha bendera ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) iliyokuwa safarini kuelekea Oman ikitokea UAE iliposhambuliwa wakati ikivuka katika mlango huo wa Hormuz katika eneo la kimkakati lilipo kati ya Iran na Oman.
Akizungumza katika mazishi hayo mjini Musoma leo Alhamisi Mei 21,2026 Chikoka amesema watashirikiana na familia kufuatilia stahiki za marehemu.
"Nitumie nafasi hii kutoa pole kwa familia kuhusu tukio hili baya lakini pia niwahakikishie familia kuwa Serikali ipo tayari kushirikiana nanyi mkiona kuna haja ya kuwa kiunganishi ili kupata stahiki za marehemu anazostahili,"amesema Chikoka.
Chikoka amewasihi wakazi wa Musoma kuishi kivitendo na kuyaenzi yale mazuri aliyoyafanya marehemu enzi za uhai wake kwa ajili ya familia na jamii nzima.
Mwakilishi kutoka Wakala wa Meli Nchini (Tasac), Lameck Sondo amewaomba Watanzania kutambua na kuthamini mchango wa mabaharia katika kujenga na kukuza uchumi wa jamii na Taifa kwa ujumla.
Sondo amesema kazi ya ubaharia ni ngumu lakini ina umuhimu katika uchumi wa nchi kwani pamoja na mambo mengine inasaidia kusafirisha mizigo duniani kote kwa njia ya maji, ambayo kutokana na weledi wa mabaharia imeonekana kuwa bora kwa ajili ya usafirishaji wa mizigo.
Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka akitoa heshima za mwisho wakati wa mazishi ya baharia mtanzania, Nchama Maregesi aliyefariki dunia baada ya meli aliyokuwa akifanya kazi kushambuliwa katika mfereji wa Hormuz.
"Marehemu alikuwa mfano wa uzalendo,nidhamu, mchapa kazi na jasiri katika kazi yake ya ubaharia alionyesha mchango mkubwa kwenye shughuli zake na kuhakikisha anazifanya kwa ufanisi," amesema Sondo.
Mdogo wa marehemu, Juma Maregesi ameishukuru Serikali kwa kuwezesha mwili wa ndugu yao kupelekwa nyumbani kwa ajili ya mazishi, "bila mchango wa Serikali sisi tusingeweza."
"Rais Samia alinipigia simu akanieleza nisiwe na wasiwasi mwili utafika na kweli leo umefika, Mkuu wa wilaya tunaomba ufikishe salaam zetu kwake," amesema Maregesi.