Israel yatajwa kukwama misaada ya Gaza

Muktasari:

  • Mapigano mapya yaliyozuka baina ya Israel na wanamgambo wa Hamas, imetajwa kuwa kikwazo kikubwa kwa ufikikaji wa misaada ya kibinadamu huko Gaza.

Gaza. Umoja wa Mataifa (UN) umeilalamikia Israel kusababisha kukwama kuingia kwa misaada ya kibinadamu Gaza katika kivuko cha Rafah mpakani mwa na Misri, huku ukaguzi ukitajwa kuwa ndio kikwazo kikubwa.

Katika chapisho lake kwenye mtandao wa X, Umoja huo umesema Israel imepanua uwezo wake wa kukagua misaada inayotolewa kupitia kivuko cha mpaka cha Rafah kinachodhibitiwa na Misri.

Pia, Umoja wa Mataifa umesema usambazaji wa misaada umesimama kwa kiasi kikubwa nje ya eneo la Rafah katika siku chache zilizopita kutokana na mapigano makali na vikwazo vya kutembea kwenye barabara kuu, hasa ndani na karibu na mji wa karibu wa Khan Younis.


Katika taarifa yake ya hivi karibuni, ofisi ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya kibinadamu, imesema uwezo wa wafanyakazi wake huko Gaza kupokea misaada inayokuja umepungua kwa kiasi kikubwa.

“Uhaba wa malori Gaza, kukatika kwa mawasiliano ya simu na kuongezeka kwa idadi ya wafanyakazi ambao hawakuweza kusafiri kwenda kwenye kivuko cha Rafah kutokana na mapigano makali, ni miongoni mwa changamoto zinazotukabili,” imesema taarifa hiyo.

Bodi ya wizara ya ulinzi ya Israel inayosimamia sera katika maeneo ya Palestina, Cogat, imesema Umoja wa Mataifa unapaswa kuongeza nguvu zaidi katika kupeleka misaada kwa watu huko Gaza.


Imeandaliwa na Victor Tullo