Jeshi la Israel lawaua kimakosa raia wake Gaza

Muktasari:

  • Raia watatu wa Israel waliokuwa wamechukuliwa mateka ┬áKaskazini mwa Gaza, wameuawa na Jeshi la Ulinzi la nchini humo (IDF) kimakosa ikielezwa kuwa ni katika hatua za kujilinda.

Gaza. Wanajeshi wa Israel wamewaua kwa kuwapiga risasi na kuwaua mateka watatu wa Israel Kaskazini mwa Gaza kimakosa, Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limesema.

Msemaji wa IDF, Daniel Hagari amesema wakati wa mapigano huko Shejaiya, Kaskazini mwa Gaza jana Ijumaa, Desemba 15, 2023, IDF iliwapiga risasi mateka hao wa Israel ikiwa ni katika hatua ya kuchukua tahadhari ya kujilinda.

"Wakati wa ukaguzi katika eneo ambalo tukio hilo limetokea, jeshi la Israel lilipata wasiwasi juu ya mateka hao na ndipo lilipotekeleza mauaji hayo," amesema Hagari.

Amesema miili yao ilihamishiwa eneo la Israeli kwa uchunguzi, na ikathibitishwa kuwa walikuwa ni mateka wa Israeli.

Mateka hao wametambuliwa ni Yotam Haim na Alon Shimriz, ambao walitekwa nyara kutoka Kibbutz Kfar Aza Oktoba 7,2023 na Samer Talalka, ambaye alitekwa nyara kutoka Kibbutz siku ya tukio.

Hagari amesema IDF inaamini wanaume hao watatu waliwatoroka watekaji wao kwa sababu ya mapigano katika eneo hilo.

Alipoulizwa ikiwa watu hao watatu waliinua mikono yao juu au walipiga kelele kwa Kiebrania, Hagari amesema jeshi bado linaendelea na uchunguzi na kuahidi kuwekwa wazi kwa taarifa zote pindi uchunguzi utakapokamilika.

Hagari amesema tukio hilo limetokea katika eneo ambalo IDF imekabiliana na maadui zake katika siku chache zilizopita.

Kabla ya habari za vifo vya mateka hao kutangazwa, Israel imesema inaamini mateka 132 waliobaki Gaza, 112 walidhaniwa kuwa bado wako hai.