Keki ya Rais Biya yasambaratishwa Ufaransa

Rais Paul Biya wa Cameroon

Muktasari:

Wapinzani wa Rais Paul Biya wa Cameroon wameisambaratisha keki ya kuadhimisha miaka 40 ya kiongozi huyo madarakani.

Yaounde. Wapinzani wa Rais Paul Biya wa Cameroon wameisambaratisha keki ya kuadhimisha miaka 40 ya kiongozi huyo madarakani.

Vurugu hizo zilitokea Jumapili jijini Paris nchini Ufaransa wakati wafuasi wa Rais Biya wanaoishi nchini humo walipoamua kuadhimisha sherehe hizo sambamba na zilizokuwa zikifanyika nchini Cameroon.

Hata hivyo, kundi linalompinga kiongozi huyo la ‘Brigade Anti-Sadinards’ (BAS), lilivamia ukumbi wa sherehe na kuanzisha vurugu ikiwamo kuisambaratisha keki iliyoadaliwa kuadhimisha miaka 40 ya Rais Biya madarakani.

BAS wakiwa wamejifunga bendera ya Taifa ya Cameroon walivamia ukumbini na kugeuza viti kuwa silaha ya kuwapigia wafuasi wa Rais Biya na kuna ripoti ya watu kujeruhiwa.

Taarifa zilisema baadhi ya watu walijeruhiwa katika vurugu hizo ambapo viti vilitumika kama silaha.

Kundi la BAS limekuwa likishutumiwa kwa kuanzisha mashambulizi dhidi ya wafuasi wa Biya wanaoishi nje ya nchi.

Biya ambaye Februari mwakani anatimiza umri wa miaka 90, mwishoni mwa wiki alitimiza miaka 40 madarakani na kuwa kiongozi wa pili Afrika aliyetawala muda mrefu baada ya Rais Teodoro Obiang Nguema wa Teodoro Obiang Nguema aliyeingia madarakani mwaka 1979.

Kabla kushika madaraka ya nchi, Biya alikuwa Waziri Mkuu wa Cameroon kwa miaka saba na aliingia madarakani Novemba 6, 1982 na kuwa Rais wa pili wa nchi hiyo tangu ipate uhuru kutoka kwa koloni la Ufaransa mwaka 1960.

Biya alipochukua madaraka ya nchi Rais wa 40 wa Marekani, Ronald Reagan ndio alikuwa ametimiza miaka miwili ya urais wake. Reagan alitawala kuanzia mwaka 1981 hadi 1989. Marekani sasa ina Rais wa 46, Joe Biden.

Kiongozi huyo ambaye wafuasi wake wamempa jina la utani la ‘Popol’ hajaonekana hadharani tangu Julai alipokuwa na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron aliyefanya ziara nchini humo.

Wafuasi wake walisherehekea miaka 40 ya Rais Biya kuwa madarakani kwa kutumia bango lililokuwa na picha yake kwa kuwa yeye kwenye sherehe hizo, zaidi ya kuadhimisha akiwa nyumbani kwake na familia yake.

Uchumi kuanguka

Chini ya utawala wa Rais Biya, Cameroon ilinusurika kuanguka uchumi katikati ya miaka ya 1980 hadi mwanzoni mwa miaka ya 2000, na kusababisha siasa za uhamaji kutoka chama kimoja hadi Serikali ya vyama vingi.

Hata hivyo, kama kiongozi wa chama tawala cha Cameroon People’s Democratic Movement (CPDM), anatajwa kuwa na upendo kwa wafuasi wa chama hicho.

Pia, wafuasi wake walikubali siasa za vyama vingi miaka ya 90, ingawa ameendelea kuwa mshindi wa uchaguzi wa mfululizo, huku vyama vya upinzani vikidai kuibiwa kura.

Cameroon, imekuwa na wakuu wa nchi wawili pekee tangu ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa Wafaransa mwaka 1960, Rais wa kwanza akiwa ni Ahmadou Ahidjo ambaye baadaye alimuachia utawala Waziri Mkuu, Paul Biya ambaye aliapishwa kwa mara ya kwanza kama Rais wa nchi hiyo, mwaka 1982.

Cameroon ina idadi kubwa ya vijana na zaidi ya asilimia 60 ya watu ni chini ya umri wa miaka 25.

Tuhuma za ufisadi

Biya amekuwa akikoselewa kwa utawala wake wa kimabavu na ufisadi uliokithiri katika nchi hiyo ambayo mwananchi wa kawaida anaishi chini ya dola mbili kwa siku, hali iliyosababisha manung’uniko na uasi kwa baadhi ya maeneo na wengine kujitenga na kutoa pande mbili zinazopingana za wanaozungumza lugha ya Kifaransa na Kiingereza.

Kuna wakati ripoti ya Shirika la Transparency International, iliitaja Cameroon kuwa ‘nchi fisadi zaidi duniani’ na hapo ndipo ilipo orodheshwa kama Taifa la juu zaidi lenye matukio ya kifisadi hiyo ilikuwa mwaka 1998 na 1999.

Biya, pia amekuwa na sifa mbaya kama Rais ambaye anaweza kuiongoza Cameroon akiwa nje ya nchi, akitumia pesa nyingi za walipa kodi katika hoteli za kifahari nchini Uswisi na inaelezewa huko anamiliki jengo la kifahari ambako mara kadhaa amekuwa akienda likizo huko.

Hata hivyo, wafuasi wa Biya waliielezea ripoti hiyo kama “propaganda”, ndipo ripoti nyingine ikatolewa ikisema kiongozi huyo alitumia dola milioni 182 kwa safari zake za kibinafsi tangu awe rais na kwamba pia alitumia dola 40,000 kwa siku kwa ajili ya malazi ya hoteli ya yeye na wasaidizi wake.

Kuka muda mrefu madarakani kulitokana na Bunge linaloongozwa na chama tawala kupiga kura ya kurekebisha katiba, kuondoa ukomo wa mihula ya urais.

Marais wa muda mrefu

Kwa bara la Afrika, viongozi wanaotajwa kuwa madarakani kwa muda mrefu zaidi hadi kufikia mwaka 2018 ukimuacha Rais Paul Biya ambaye hadi mwaka huu wa 2022 ametimiza miaka 40 madarakani ni pamoja na Teodoro Obiang Nguema wa Equatorial Guinea (39).

Wengine ni Denis Sassou Ngueso wa Jamhuri ya Congo (34), Idris Deby wa Chad (28) na Yoweri Kaguta Museven wa Uganda ambaye mpaka mwaka huu wa 2022 anafikisha miaka 36 madarakani.