Kilichowakuta zimamoto Septemba 11 - sehemu (2)

Muktasari:
- Katika toleo lililopita tulisimulia mwanzo na mwisho wa majengo ya World Trade Centre (WTC). Mmoja wa watu waliotoa maoni yao juu ya kugongwa na ndege hadi kuanguka kwa majengo pacha ya WTC ni Van Romero ambaye ni Makamu wa Rais wa Utafiti katika Taasisi ya Mabomu na Teknolojia ya New Mexico inayojulikana tu kwa kifupi chake kama ‘Tech’.
Katika toleo lililopita tulisimulia mwanzo na mwisho wa majengo ya World Trade Centre (WTC). Mmoja wa watu waliotoa maoni yao juu ya kugongwa na ndege hadi kuanguka kwa majengo pacha ya WTC ni Van Romero ambaye ni Makamu wa Rais wa Utafiti katika Taasisi ya Mabomu na Teknolojia ya New Mexico inayojulikana tu kwa kifupi chake kama ‘Tech’.
Yeye ni mmoja wa wanaodai walisikia milipuko katika minara ya majengo ya WTC mara baada ya kugongwa na kabla hayajaanguka. Romeo alisema baruti kidogo ingetosha kuliporomosha jengo hilo ikiwa tu ingekuwa imewekwa sehemu sahihi. Kwa mujibu wa vyombo vingi vya habari, walioshuhudia majengo hayo yakianguka walisema walisikia milipuko kadhaa kabla hayajaanguka. Louie Cacchioli (51), ambaye ni zimamoto aliyekuwa na gari la zimamoto ‘Engine 47’ kutoka kituo cha Harlem, New York, alisema:
“Tulikuwa wa kwanza kuingia katika mnara wa pili mara baada ya kugongwa. Nilikuwa nawapeleka zimamoto kwenye lifti kuelekea ghorofa ya 24 ili kujiweka katika hali ya kuwaokoa wafanyakazi katika jengo hilo.
“Nilipokuwa naelekea juu nikasikia mlipuko (kama) wa bomu. Tukafikiri kuwa kuna mabomu yaliyokuwa yametegwa kwenye jengo. Nilikuwa nimemwambia zimamoto mwingine abaki nami, jambo ambalo lilikuwa zuri kwa sababu tulipokwama kwenye lifti alikuwa na vifaa vya kutusaidia kujikwamua. Kulikuwa na zaidi ya watu 500 waliokuwa wamekwama.
“Ilikuwa ni vurumai kubwa. Umeme ukakatika. Ilikuwa ni giza. Kila mtu alikuwa akipiga yowe. Baadhi yetu tuliweza kutoka lakini baadhi ya wengine hawakuweza. Najua kiasi cha zimamoto 30 ambao hawakuokoka.”
Jumatatu ya Machi 11, 2002, ikiwa ni miezi sita baada ya mashambulizi hayo, kituo cha televisheni cha CBS kilionesha filamu ya mambo halisi kuhusu kile kilichowatokea zimamoto Septemba 11, 2001, kikitumia kipande cha picha za video zilizopigwa na ndugu wawili wa Ufaransa, Jules Clement Naudet na Thomas Naudet.
Ndugu hao ni wakazi wa Marekani tangu mwaka 1989. Walikuwa jijini New York wakati tukio la Septemba 11, 2001 likitukia. Jules aliipiga picha ndege ‘Flight 11’ wakati ilipokuwa ikienda kugonga mnara wa Kaskazini wa WTC.
Ndugu hao walikuwa wakipiga picha hizo kwa ajili ya filamu karibu na majengo ya WTC iliyohusu gari ‘Engine 7’ la zimamoto wa Idara ya Moto ya New York ambayo ilikuwa umbali mfupi kutoka yalipokuwa majengo ya WTC.
Ghafla ndugu hao wakajikuta wako katika kazi nyingine ambayo hawakuitarajia awali na ndio hao hao ambao walifanikiwa kupiga picha ndege ya kwanza iliyogonga mnara wa kaskazini, ambayo Rais George Bush alidai kuwa aliiona moja kwa moja. Kwa kuwa ndugu hao walikuwa na kikosi cha zimamoto wakati wakiwapiga picha kwenye kituo chao, walifanikiwa kuondoka nao kwenda eneo la tukio. Wakati kikosi cha zimamoto kutoka Idara ya Zimamoto ya New York kilipowasili eneo hilo kikiwa na mpigapicha Jules Naudet, walishangazwa walipokuta kuwa ukumbi uliokuwa chini ya ghorofa ya 96 ya mnara wa kaskazini ambao ulikuwa chini ya sehemu ambayo jengo liligongwa na ndege, ulikuwa umeharibika vibaya. Ingawa eneo la ukumbi huo halikugongwa na ndege, baadaye ilielezwa kuwa mafuta ya ndege yaliyomwagika yalimiminika kuelekea chini na hivyo kulipuka na kuharibu kabisa ukumbi huo.
“Ilionekana kana kwamba ndege iligonga ukumbi,” alisema zimamoto mmoja katika filamu hiyo iliyooneshwa na CBS Machi 11, 2002. Hivyo ndivyo ilivyoonekana ingawa ndege haikugonga eneo hilo.
Wataalamu mbalimbali wa moto katika majengo marefu walikataa uwezekano wa majengo ya WTC kuanguka kwa sababu ya moto. Wengi walisema hakuna jengo hata moja lililowahi kuanguka kwa sababu hiyo na wala WTC lisingeweza kuwa la kwanza.
Mara baada ya ndege kugonga, kituo kikuu cha kuendeshea shughuli za zimamoto katika majengo ya WTC kiliwekwa katika mnara wa kaskazini. Ikiwa mnara huo ungeanza kuanguka kabla ya ule wa kusini, zimamoto wengi zaidi wangekufa.
Lakini, waliokoka kwa sababu baada ya mnara wa kusini kuanguka, ndipo wataalamu wakaona kuwa hata mnara wa kaskazini nao utaanguka pia. Kwa hiyo wengi walianza kuondoka haraka kutoka katika mnara huo, na waliokuwa na bahati zaidi walipona lakini wakajeruhiwa vibaya.
Mamia ya wafanyakazi wa zimamoto walifia katika ngazi za majengo hayo kwa sababu haikufikiriwa kwa vyovyote kama majengo hayo yangeporomoka.Kisha kuna ile habari ya ofisa usalama katika majengo ya WTC aliyoambiwa na aliyekuwa mwandishi wa habari wa televisheni ya ABC, Peter Charles Archibald Ewart Jennings. Ofisa huyo, ambaye hakutajwa jina, alisema baada ya kuanguka kwa mnara wa kusini alipigiwa simu kutoka Kituo cha Mamlaka ya Bandari ya New York katika ghorofa ya 22 ya WTC ikimwomba afanye mpango wa uokozi haraka katika mnara wa kaskazini.
Yeye mwenyewe aliamua kwenda na kikosi cha zimamoto na, alisema, walikuta eneo hilo katika ghorofa hiyo likiwa limeharibika sana. Kwa bahati mbaya, Peter Jennings alifariki dunia Jumapili ya Agosti 7, 2005 kwa maradhi ya mapafu. Tazama, ndege iligonga jengo hilo katika ghorofa ya 96, lakini zimamoto hao katika ghorofa ya 22 walisema wafanyakazi hao wa Mamlaka ya Bandari ya New York walisema walikuwa wamekwama kwa sababu ukumbi ulikuwa umeharibiwa vibaya kiasi kwamba ofisa huyo na kikosi chake walilazimika kupakua kifusi ili waweze kupita kuwaokoa wafanyakazi hao wa mamlaka ya bandari.
Kamishna Msaidizi wa Zimamoto katika Jiji la New York, Stephen Gregory, alisema alichoona ni mwanga na kisha akasikia milipuko sehemu ya chini ya mnara wa pili, kisha mnara huo ukaporomoka.
Mashuhuda wengi waliamini kuwa walisikia milipuko ya mabomu ndipo majengo hayo yalipoanza kuanguka. Lakini ikiwa hivyo ndivyo ilivyokuwa kama wataalamu hao wanavyodai, basi ndiyo sababu mnara wa kwanza kugongwa ulikuwa wa mwisho kuanguka na mnara wa mwisho kugongwa ukawa ndio wa kwanza kuanguka kwa sababu mabomu yatakuwa yalianza kulipuka katika mnara wa pili kugongwa na ndege badala ya ule mnara wa kwanza.
Afisa mmoja wa zima moto wa huko Arlington, Virginia, Derek Spector, anaeleza kuwa hana tatizo kukumbuka mahali alipokuwa September 11, 2001.
“Kwa kweli tulipelekwa Rosslyn ambako kulikuwa na moto, na wakati tukijitayarisha kuondoka huko, tulisikia ndege imeanguka huko Pentagon. Na tulipokuwa tunaingia kwenye kituo cha zima moto tuliusikia mlipuko huo”.
Spector alikuwa miongoni mwa wazima moto wa kwanza kufika Makao Makuu ya Jeshi la Marekani, Pentagon. Hivi karibuni alishiriki katika kumbukumbu ya kuendesha pikipiki kuwakumbuka wale waliopoteza maisha yao katika mashambulizi hayo na wakijumuika na polisi na zima moto ambao waliwajibika siku hiyo.
Specter alisaidia kupandisha kile kinachoelezewa bendera ya uzalendo, bendera kubwa ya Marekani ambayo inapeperushwa katika mataifa yote 50 kuwakumbuka wale ambao wamepoteza maisha yao Septemba 11 na wanajeshi ambao wamepigana vita nchini Afghanistan na Iraq.
“Nadhani inaashiria kila kitu ambacho ni kizuri katika nchi hii. Ukiweka siasa kando, ukaondoa vyama, bado sisi ni Wamarekani, na bado tunaithamini nchi hii bila kujali tunachosema au tunachofanya. Ndani ya mioyo yetu bado tunaiamini nchi hii na tunaithamini sana nchi yetu”, anasema.
Je, alitekeleza? Tukutane kesho kuona zaidi.