Madai ya kujiua baada ya mke kukataa kumpikia kuku yachunguzwa

Muktasari:
- Mwananume mmoja nchini Kenya anadaiwa kufariki dunia kwa kujiunguzaua kwa kujichoma baada ya mke wake kukataa kumpikia kuku.
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi nchini Kenya linachunguza madai kwamba mwanamume mmoja amejitoa uhai baada ya mkewe kuripotiwa kukataa kumpikia kuku nyumbani kwao Uriri, Kaunti ya Migori nchini Kenya.
Maafisa wamesema mwananume huyo wa miaka 45 alijifungia ndani ya nyumba yao kabla ya kujichoma moto mwanzoni mwa wiki hii.
Walioshuhudia waliambia Polisi kuwa mtu huyo aliyejulikana kwa jina la John Rugala, alijifungia ndani ya nyumba hiyo kabla ya kuiteketeza.
Hii ni baada ya mke kukataa kumpikia kuku hali ambayo ilileta ugomvi wa nyumbani katika familia hiyo.
Inasemekana mwanamke huyo alimwambia mumewe kabla hajachukua uamzi mgumu wa kujiondoa uhai kuwa, kuku huyo ni mali ya binti yao na kwamba isingekuwa busara kumchinja kwaajili ya kitoweo nyumbani humo.
Wenyeji walikimbilia eneo la tukio kwa nia ya kuzima moto huo lakini juhudi zao hazikuweza kuokoa uhai wa mwanaume.
Polisi walisema mwili wa marehemu umehamishiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Migori kusubiri uchunguzi wa polisi.