Malawi yafunga shule kukwepa Kimbunga Freddy

Muktasari:

  • Kufuatia athari za kimbunga Freddy, mamlaka nchini Malawi imezifunga shule kufuatia mvua kubwa zinazonyesha kusini mwa nchi hiyo.

Dar es Salaam. Mamlaka ya elimu nchini Malawi imezifunga shule katika wilaya 10 kutokana na wasiwasi wa usalama baada ya Kimbunga Freddy kusababisha uharibifu katika nchi jirani ya Msumbiji.

 Kwa mujibu wa BBC, mvua kubwa inayonyesha kusini mwa Malawi imeharibu barabara na kusitisha uzalishaji wa umeme, huku mvua zaidi zikitarajiwa kunyesha katika siku chache zijazo.

Masomo yamesimamishwa kuanzia leo Machi 13, 2023 Jumatatu na Jumanne katika taasisi zote za masomo katika eneo hilo.

Wizara ya Elimu nchini humo imeelekeza kwamba walimu na wanafunzi watumie majukwaa yanayopatikana mtandaoni na masomo ya redioni katika kipindi ambacho shule zimefungwa.

 “Wakati madarasa yatakaporejea walimu wanahimizwa kuongeza muda wa masomo ili kufidia muda uliopotea,” iliongeza.

Nchi jirani ya Msumbiji imepokea mvua ya zaidi ya mwaka mmoja katika wiki nne zilizopita, huku Kimbunga Freddy kikitua Jumapili kwa mara ya pili katika mwezi mmoja.

Idadi ya vifo nchini Msumbiji ni imefikia 28 tangu dhoruba hiyo ilikumbe taifa hilo kwa mara ya kwanza.