Mitaji yatajwa changamoto wafanyabiashara wanawake

Muktasari:

Kuwepo kwa mitaji kwa wafanyabiashara wanawake ni suala moja lakini kuweza kuisimamia imetajwa kuwa ni changamoto kubwa kwa kundi hilo kutokana na kukosa elimu na ujuzi katika usimamizi wa fedha.

Dar es Salaam. Mtendaji Mkuu wa Ecobank Tanzania, Charles Asiedu,  amesema licha ya kukaribia uwiano wa jinsia 50 kwa 50, changamoto kubwa inayopaswa kutatuliwa kwa wafanyabiashara wanawake ni usimamizi wa fedha.

Amesema hapa nchini asilimia 50 ya biashara zinafanywa na wanawake, lakini changamoto kubwa wanayokutana nayo ni mitaji hivyo elimu inahitajika ili waweze kuisimamia vizuri pia.

Asiedu ameyasema hayo wakati akifungua warsha 'Ellevate by Ecobank’ yenye lengo la kuwasaidia na kuwainua wanawake wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa katika masuala mbalimbali ya kifedha na kuwaongezea kipato ili waweze kumudu biashara na kuinua vipato vyao.

"Kuwepo kwa mitaji ni jambo moja lakini kuweza kusimamia huo mtaji ni jambo la pili, wanawake wanalalamika hawapati mitaji lakini changamoto tumebaini ni namna fedha hiyo inavyotumika, hivyo tumekuja na hii akaunti tunampa mtaji lakini anapata msimamizi pia," amesema.

Amesema ili kuhakikisha wafanyabiashara waliopo katika akaunti hiyo wanakua zaidi, Ecobank imeanzisha mfumo maalum wa kuwaunganisha wafanyabiashara mbalimbali barani Afrika ujulikanao kama "Trade hub" kwa lengo la kupanua wigo wa biashara zao ili kuweza kutanuka kimasoko kimataifa  na kuwakutanisha wafanyabiashara wenzao ili waweza kuuza na kununua  kupitia huo mfumo.

Pia amesema kutokana na takwimu za benki hiyo zaidi ya asilimia 95 ya wafanyabiashara wadogo na wakubwa hapa nchini,  asilimia 54 ya biashara zinamilikiwa na wanawake hivyo mpango huo utaweza kuwainua wanawake wengi ili kuweza kujitegemea kwenye mitaji na kukua kiuchumi.


Mkuu wa kitengo cha masoko na mawasiliano EcoBank Tanzania, Furaha Samalu amesema tangu kuzinduliwa kwa mpango huo maalum, Tanzania imewafikia wanawake 194 ambapo mpaka mwishoni mwa mwaka huu wanatarajia kuwafikia wanawake  wafanyabiashara 500 wanaomiliki biashara zao na waajiriwa.

Mkuu wa kitengo cha biashara Ecobank Joyce Ndyetabura amesema kuna umuhimu kwa wafanyabiashara wanawake kutumia mifumo ya kibenki kwani walio wengi hawatumii mifumo yenye nidhamu kuhifadhi fedha za biashara.

Mkurugenzi wa Shirika la Tawido linalofanya utetezi wa haki za wanawake wasichana na watoto, ambaye pia ni  mfanyabiashara, Sofia Lugilahe amesema fursa hiyo ni muhimu kwa wanawake wafanyabiashara.

"Wanawake hatuna mali zisizohamishika hivyo tunakua waathirika wa kukosa msaada wa kifedha, hivyo elimu wanayoipata inasaidia kujua umuhimu wa kutumia mifumo ya kibenki, kuwekeza na kuwa na mali zisizohamishika na kupata elimu ya usimamizi wa fedha," amesema Lugilahe.

Vida Mndolwa kutoka Kampuni ya biashara ya wanawake NABW-Tz, amesema ni muhimu kwa wanawake kuzitumia fursa hizo ili waweze kukua kibiashara.