Mjue Rais Geingob wa Namibia aliyefariki dunia
Muktasari:
- Rais Hage Geingob amefariki dunia kutokana na maradhi ya saratani yaliyokuwa yakimkabili, amefanyiwa upasuaji mara kadhaa katika jitihada za kuokoa uhai wake.
Windhoek. Wananchi wa Namibia na Afrika kwa ujumla wanaomboleza kifo cha Rais wa Namibia, Hage Geingob (82), kiongozi aliyejitoa kupigania nchi yake tangu wakati wa ujana wake.
Geingob, waziri mkuu aliyekaa muda mrefu zaidi nchini Namibia na Rais wa tatu, alikuwa mwanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi aliyegeuka kuwa mwanasiasa na tumaini katika Taifa hilo la kusini mwa Afrika.
Ameaga dunia mapema leo Jumapili Februari 4, 2024 katika hospitali moja iliyopo katika mji mkuu wa Windhoek ambako alikuwa akipata matibabu ya saratani.
Geingob aliyezaliwa kaskazini mwa Namibia mwaka 1941, alikuwa Rais wa kwanza wa Namibia kutoka nje ya kabila la Ovambo, ambalo ni la zaidi ya nusu ya wakazi wa nchi hiyo.
Alianza harakati dhidi ya utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini, nchi ambayo wakati huo iliitawala Namibia, tangu miaka yake ya awali ya shule kabla ya kufukuzwa nchini humo na kwenda uhamishoni.
Akiwa uhamishoni alikaa karibu miongo mitatu nchini Botswana na Marekani.
Kiongozi huyo mrefu na mwenye sauti nzito, alisoma katika Chuo Kikuu cha Fordham huko New York, Marekani na baadaye sana alipata shahada ya uzamivu (PhD) nchini Uingereza.
Akiwa Marekani, aliendelea kuwa mtetezi mkubwa wa uhuru wa Namibia, akiwakilisha vuguvugu la ukombozi wa ndani (Swapo), ambacho sasa ni chama tawala, katika Umoja wa Mataifa na kote Marekani.
Mapema miaka ya 1970, alianza kufanya kazi katika Umoja wa Mataifa katika masuala ya utawala.
Akionekana kama kiongozi mkuu, alirejea Namibia mwaka 1989, mwaka mmoja kabla ya uhuru wa nchi hiyo.
“Nilikumbatia ardhi ya Namibia baada ya miaka 27 uhamishoni. Nikikumbuka nyuma, safari ya kujenga Namibia mpya imekuwa ya manufaa,” alisema katika ukurasa wake wa X (Twitter) mwaka 2020, akiweka picha ya mdogo wake akibusu lami baada ya kutua nyumbani.
Swapo iliposhinda uchaguzi wa kwanza mwaka wa 1990, Geingob aliteuliwa kuwa waziri mkuu, nafasi aliyoshikilia kwa miaka 12 kabla ya kurejea mwaka 2012.
Mwaka 2014, chama kiliposhinda uchaguzi mwingine, Geingob akawa Rais.
Geingob aliyetambulika kwa kuzungumza kwa ukali akiwa na miwani yake mipana, kabla ya urais alishika nyadhifa mbalimbali za uwaziri na za ndani za chama.
Muhula wake wa kwanza kama Rais ulitiwa doa na mdororo wa uchumi, ukosefu mkubwa wa ajira na madai ya ufisadi.
Mwaka 2019, hati zilizochapishwa na WikiLeaks zilieleza kwamba maofisa wa Serikali walipokea rushwa kutoka kwa kampuni moja ya Iceland, ili waendelee na shughuli zao kwenye maeneo ya uvuvi ya Namibia.
Kashfa ya “kuoza kwa samaki” ilitishia matarajio ya Geingob kuwania muhula wa pili, huku mkuu huyo wa nchi pia akilaumiwa kwa kutoa kandarasi kwa kampuni za kigeni badala ya kampuni ya ndani.
Kura zake zilishuka kwa kiasi kikubwa mwaka 2019 hadi asilimia 56 kutoka asilimia 87 alizopata mwaka 2014.
Alipata na matatizo ya kiafya katika miaka ya baadaye, baada ya kufanyiwa upasuaji wa ubongo mwaka 2013 na upasuaji wa valvu za moyo nchini Afrika Kusini, Juni 2023.
Alikuwa shabiki mkubwa wa soka na alicheza mchezo huo akiwa kijana, jambo ambalo lilimpa jina la utani la “Danger Point”.
Alioa mara tatu katika maisha yake, mwaka 1967, 1993 na tena mwaka 2015 na ana watoto wengi. Mke wake wa mwisho, Monica Geingos ni mwanasheria na mfanyabiashara.