Rais wa Namibia ataka uwazi katika chaguzi za Afrika

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na mgeni wake Rais Dkt.Hage Geingob wa Namibia ikulu jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

Amewaambia mabalozi kuwa wakati umefika kwa viongozi wa Afrika kuboresha mifumo yao katika kuendesha chaguzi sambamba na kutoa fursa kwa watu kufanya chaguzi za kidemokrasia.

Dar es Salaam. Rais wa Namibia Dkt Hage Geingob amesema nchi za Afrika zinapaswa kuweka mazingira ya uwazi katika chaguzi zake ili kuondoa manung’uniko baina ya wanasiasa na vyama vitakavyoshindwa.

Akizungumza na mabalozi mbalimbali wa Afrika leo jijini Dar es salaam, Dk Geingob amesema mazingira ya chaguzi yakiwa wazi na yenye uhuru na haki yataepusha wasiwasi kwa wanasiasa kuhisi wameibiwa hali aliyosema inaweza kusababisha machafuko.

Amewaambia mabalozi kuwa wakati umefika kwa viongozi wa Afrika kuboresha mifumo yao katika kuendesha chaguzi sambamba na kutoa fursa kwa watu kufanya chaguzi za kidemokrasia.

“Ni lazima chaguzi ziendeshwe katika mazingira ya uwazi na ukweli, hii itaondoa wasiwasi na kuepusha malalamiko ya hisia za kuwepo kwa udanganyifu kwa wale wanaoshindwa” amesema.

Akizungumzia uchaguzi mkuu ujao, rais huyo wa Namibia amesema Tanzania ni kisiwa cha amani na anayo imani kubwa kuwa uchaguzi wake utafanyika katika hali ya amani na vile vile utakuwa wa haki na huru.

Amewataka wanasiasa na wananchi wa Tanzania kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu na kwa washiriki wa nafasi mbalimbali kukubali kushindwa.