Mtoto wa Museveni kupeleka jeshi Urusi

Kiongozi wa Jeshi nchini Uganda Muhoozi Kainerugaba

Muktasari:

  • Baada ya tamko la kuivamia Nairobi, Kiongozi wa Jeshi nchini Uganda Muhoozi Kainerugaba ametoa tamko jingine la kutuma vikosi vya Jeshi nchini  Urusi endapo kutatokea tishio lolote la kiuslama nchini humo.

Dar es Salaam. Kiongozi wa Jeshi nchini Uganda, Muhoozi Kainerugaba ambaye ni mtoto wa Rais wa nchi hiyo, Yoweri Museveni, amesema atatuma vikosi vya Jeshi mjini Moscow nchini Urusi kulinda usalama endapo kutatokea tishio la kiuslama nchini humo.

"Nchi za Magharibi zinapoteza muda wake kwa propaganda zisizo na maana za Kiukreni, Uganda itatuma wanajeshi kuilinda Moscow kama kutatokea uvamizi nchini Urusi," aliandika kiongozi huyo ambaye ni mfuasi wa Rais wa Urusi, Vladmir Putin kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Pia kupitia mtandao huo, kuongozi huyo mkuu wa jeshi jana alitangaza kuanzisha chaneli ya runinga yenye chapa ya jina lake ‘MK’.

Kainerugaba mwenye umri wa miaka 48, hivi karibuni amekuwa akitumia mtandao wa Twitter kutoa matamko mbalimbali ambapo mwezi uliopita alieleza nia yake ya kugombea urais wa taifa lake mwaka 2026.

Mwezi Oktoba mwaka jana, Rais Museveni alieleza kwamba hataandika tenda mambo yanayohusu taifa hilo kwenye mitandao hasa baada ya tukio la mwanaye huyo kuonyesha nia ya kuivamia Nairobi.

Tamko la kiongozi huyo wa jeshi linakuja wakati tayari Uganda ilijiepusha na kura za Umoja wa Mataifa kuhusu mzozo wa Ukraine ambapo mazimio yalipitishwa kuitaka Urusi kuondoa vikosi vyake nchini Ukraine.

Julai mwaka jana wakati wa ziara ya Waziri wa mambo ya nje Urusi Sergei Lavrov, Kainerugaba alinukuliwa akisema “tutawezaje kuwa tofauti na mtu asiyetuchukia,” amesema.

Ameongeza kuwa Urusi imetoa msaada  mkubwa kwa nchi za Afrika  hasa katika kusaidia harakati za uhuru  kuwaondoa wakoloni.