Mtoto wa Rais wa zamani jela kwa ulanguzi wa dawa za kulevya

Malam Bacai Sanha Jr

Muktasari:

 Mtoto huyo wa Rais wa Guinea-Bissau alikanatwa Dar es Salaam, Tanzania mwaka 2022 na kurudishwa Marekani ambako alikuwa akikabiliwa na kesi ya kuingiza dawa za kulevya nchini humo

Marekani. Mtoto wa Rais wa zamani wa Guinea-Bissau amehukumiwa kifungo cha miaka sita na nusu jela kwa kuhusika katika biashara ya kimataifa ya ulanguzi wa dawa za kulevya aina ya heroini, Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya ya Marekani (DEA) ilitangaza Jumanne Machi 26, 2024.

"Malam Bacai Sanha Jr. hakuwa mlanguzi wa dawa za kulevya wa kawaida," amesema Douglas Williams, wakala maalumu anayesimamia Ofisi ya FBI, iliyoko Houston.

"Yeye ni mtoto wa Rais wa zamani wa Guinea-Bissau na alikuwa akisafirisha dawa za kulevya kwa sababu maalumu,  kufadhili mapinduzi," imesema taarifa ya mamlaka hiyo.

Sanha alikuwa kiongozi na mratibu wa ulanguzi wa dawa za kulevya aina ya heroini na alihusika katika uagizaji wake kutoka Ulaya hadi Marekani, kwa mujibu wa taarifa hiyo.

Alikamatwa pamoja na mshiriki mwenzake baada ya kuwasili Dar es Salaam, Tanzania Julai 2022. Hata hivyo, walirejeshwa Marekani muda mfupi baadaye.

Septemba 2023, Sanha alikubali makosa ya kula njama ya kusambaza kemikali zinazodhibitiwa kwa madhumuni ya kuingizwa nchini kinyume cha sheria," kwa mujibu wa taarifa ya Jumanne.

Alihukumiwa kifungo cha miezi 80 jela.

Guinea-Bissau imekuwa na historia ya mapinduzi ya kijeshi yaliyoingiliana na vipindi vya utawala wa kidemokrasia, ingawa viongozi waliochaguliwa waliweza kuhudumu kwa muhula kamili tangu nchi hiyo ilipopata uhuru kutoka kwa Ureno mwaka 1974.

Baba yake Sanha, Malam Bacai Sanha, awali aliwekwa madarakani na jeshi kama kiongozi wa muda mwaka 1999 kabla ya kushindwa katika uchaguzi mwaka uliofuata.

Alishinda urais katika uchaguzi wa mwaka 2009, lakini alifariki dunia alipokuwa akipatiwa matibabu mjini Paris, Ufaransa Januari 2012 kabla ya kumaliza muda wake.

Mwanaye, anayejulikana kama "Bacaizinho" nchini Guinea-Bissau, amehudumu katika majukumu tofauti serikalini, ikiwa ni pamoja na mshauri wa kiuchumi wa baba yake.