Mwanaume auwa wanawe wawili kisa kuachwa na mke

Muktasari:

  • Mwanaume mmoja nchini Kenya amewaua watoto wake wawili kutokana na mgogoro wa kifamilia uliosababisha kuachwa na mke.

Kenya. Mwanamume mwenye miaka 28, Hillary Rono amekiri kuwaua wanawe wawili baada ya mke wake kuondoka nyumbani kutokana na ugomvi kati yao katika Kaunti ya Bomet nchini Kenya.

Rono ameripotiwa kuwaua watoto wake wavulana wenye umri wa miaka miwili na mitatu kwa kutumia panga kabla ya kujaribu kujiua kwa kunywa sumu Jumapili iliyopita.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ndogo ya Bomet ya Kati, Musa Omar amesema mshukiwa anahisiwa kufanya hivyo kama kulipiza kisasi baada ya mke wake kuondoka nyumbani.

Baada ya kunywa sumu, Rono alikwenda hadi nyumbani kwa wazazi wake ambako ni karibu na kwake, akiwaambia kuwa amewaua watoto wake pia yeye karibu atakufa.

Baba yake aliwaambia majirani ambao walikimbia na kumkamata kabla ya polisi kufika. Polisi waliondoa miili ya watoto hao na kupata kichupa kilichokuwa na sumu inayoaminika kunywewa na Rono.

Alipewa huduma ya kwanza katika kituo cha afya cha karibu kabla ya kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Longisa ambako anaendelea kupata matibabu.

Polisi waliambiwa kuwa mke wa mshukiwa aliondoka nyumbani wiki mbili zilizopita akihofia kuuawa na mumewe kutokana na migogoro ya kifamilia ambayo ilikuwepo kwa muda mrefu.