Mwili wa mchungaji uliokaa siku 579 kungojea afufuke, wazikwa

Muktasari:

  • Mwili wa Mchungaji Siva Moodley uliohifadhiwa Johannesburg tangu Agosti 15, 2021 alipokutwa na mauti umezikwa baada ya kusubiriwa afufuke kwa siku 579.

Dar es Salaam. Mhubiri ambaye alifariki dunia Agosti 2021 nchini Afrika Kusini na mwili wake kuendelea kuhifahiwa mochwari na kuombewa ili afufuke hatimaye amezikwa leo Jumamosi Machi 18, 2023.

Mwili wa Mchungaji Siva Moodley ulihifadhiwa kwa siku 579 licha ya juhudi za familia pamoja na ndugu hao kwenda mochwari kuuombea bila mafanikio.

Kipindi chote hicho akiwa mochwari, imeelezwa kuwa akaunti zake za Facebook na Twitter zilikuwa zinawekwa ujumbe mpya na matukio yanayoendelea kuonyesha zinatoka kwake.

Tovuti ya Tuko imeeleza kuwa mwili wa Mchungaji Siva Moodley ulihifadhiwa mochwari jijini Johannesburg tangu Agosti 15, 2021 alipokutwa na mauti.

Mwanzilishi huyo wa Kanisa la The Miracle Centre lililo kaskazini mwa Johannesburg aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 53 baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa jarida la OIL, familia ya Mooley na marafiki zake walikuwa wakitembelea mahali ulikohifadhiwa mwili huo kwa lengo la kumwombea ili afufuke.

Licha ya kusudio lao ndugu na familia kuendelea kuuhifadhi mwili huo, meneja wa eneo hilo walilohifadhi maiti, Martin du Toit aliwasilisha ombi katika mahakama ya Johannesburg akitaka ruhusa ili auzikwe au kuuchoma moto.

Tangu mchungaji huyo alipofariki, inaelezwa kwamba ibada zimekuwa zikiendelea katika kanisa lake, huku zikiendeshwa na mke wake anayeitwa Jessie pamoja na watoto wake wawili David na Kathryn Jade.

Ibada hizo huonyeshwa moja kwa moja kwenye mitandao ya kijamii. Hata hivyo hadi sasa inaelezwa kuwa kanisa hilo halijawatangazia tukio la kufariki dunia kwa mhubiri huyo wala hawajui yupo wapi.