Netanyahu amgomea Biden, adai anachofanya siyo sera binafsi

Rais wa Marekani, Joe Biden (kushoto) akiwa kwenye mazungumzo na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu. Picha na Mtandao

Muktasari:

  • Kauli ya Nentanyahu imekuja siku chache baada ya Biden kufanya mahojiano na kituo cha televisheni cha MSNBC cha Marekani,  kwamba waziri mkuu huyo anafanya kosa kubwa kwa kutofanya juhudi za kuwalinda raia wasio na hatia kwenye vita vya Gaza.

Jerusalem. Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amegomea onyo  la Rais Joe Biden wa Marekani la kumtaka asivuke mstari mwekundu kwa kuushambulia mji wa Rafah uliopo kusini mwa Ukanda wa Gaza, wenye wakimbizi wa Palestina zaidi ya 2.3 milioni.

Kauli ya Nentanyahu imekuja siku chache baada ya Biden kufanya mahojiano na kituo cha televisheni cha MSNBC cha Marekani, kwamba waziri mkuu huyo anafanya kosa kubwa kwa kutofanya juhudi za kuwalinda raia wasio na hatia kwenye vita vya Gaza. “Anaiumiza Israeli badala ya kuisaidia Israeli.” alisema Biden.

Majibu hayo ya Netanyahu yanaonyesha kuzidisha mzozo kati ya viongozi hao  wawili (Biden na Netanyahu) aliyatoa jana    Jumapili alipofanya mahojiano na vyombo vya habari vya Bild, televisheni ya Welt na Politico yaliyofanyika kwenye makazi yake yaliyopo Jerusalem. Marekani na Israeli ni washirika wa kihistoria.

“Kama Biden anamaanisha kuwa mimi natekeleza sera zangu binafsi tofauti na zile za wengi ambazo ni matakwa ya Waisraeli na kwamba hii inaumiza masilahi ya Israeli, basi amekosea katika mambo yote mawili,” alisema Netanyahu.

Netanyahu kwenye mahojiano hayo alisisitiza kuwa kipaumbele chake ni kuwalinda Waisraeli wasishambuliwe tena na kikundi cha wapiganaji wa Hamas kama ilivyotokea Oktoba 7, 2023.

Alipoulizwa kama ana dhamira ya kuushambulia mji wa Rafah, Netanyahu alijibu: “Tutakwenda  huko. Hatuwezi kuwaacha. Unajua, nina mstari mwekundu. Unajua mstari mwekundu ni nini? Ile Oktoba 7, 2023 isitokee tena. Isitokee tena,” alisema Netanyahu akirejeea mauaji yaliyofanywa na Hamas na kusababisha vifo wa Waisraeli zaidi ya 1,160.

Bila kutaja majina, Netanyahu alisema anaungwa mkono na viongozi kadhaa wa nchi za Kiarabu kwa kuendeleza vita dhidi ya wapiganaji wa Hamas.

“Wanaelewa na pia kukubali kimya kimya,” alisema Netanyahu na kuongeza kuwa: “Wanaelewa Hamas ni sehemu ya mhimili wa ugaidi wa Iran.”

Netanyahu pia alibashiri mapigano hayo yataisha katika kipindi cha chini ya mwezi. “Tumeharibu robo tatu ya ngome za mapigano za Hamas na tunakaribia kuimaliza ngome ya mwisho. Mapigano hayawezi kuchukua zaidi ya miezi miwili. Labda wiki sita au nne,” alisema.

Kuhusu idadi ya vifo vya Wapalestina, alitoa takwimu zake akisema wapiganaji 13,000 wa Palestina wameuawa huku akisema makadirio ya vifo vya raia ni 1 hadi 1.5 kwa kila mpiganaji na kwamba jumla ya vifo kwa raia na wapiganaji inafika zaidi ya 26,000.

Pia, alipinga hoja ya kusimamisha mapigano wakati wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, akisema anachotaka kuona ni kuachiwa kwa mateka wengine wa Israeli na kwamba bila kuachiwa mateka hakuna suala la kusimamisha mapigano wakati wa mfungo.

Netanyahu pia alisema hakuna uwezekano wa kuwapo Taifa la Palestina, hoja mabayo inapingwa na mataifa mbalimbali duniani.

“Msimamo wangu na ambao unaungwa mkono na Waisraeli wengi wanaosema baada ya kilichotokea Oktoba 7, 2023 hawataki kuona Taifa la Palestina.

“Wananchi wa Israeli pia wanaunga mkono msimamo wangu kwamba lazima kwa sauti kubwa tukatae jaribio la kuwepo Taifa la Palestina,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu maoni ya Ulaya kwamba  hakuwezi kupatikana amani bila kuwepo suluhisho la kuanzisha mataifa mawili, Netanyahu alijibu kuwa: “Ndiyo, wanasema hivyo. Lakini, hawaelewi sababu ya kukosa amani siyo Wapalestina kutokuwa na taifa. Ni kwa sababu Wayahudi wana taifa. Na kwa ukweli, Wapalestina hawajakubali  kulitambua taifa la Wayahudi.”

Netanyahu alipoelezwa kuhusiana na kufanya mabadiliko ya uongozi wa Palestina ikiwamo utamaduni wao, kiongozi huyo alisisitiza kuwa Israeli lazima iwe na udhibiti wa kiusalama kwenye mamlaka ya Kiarabu ya magharibi mwa Mto Jordan.

Kwenye mahojiano hayo Netanyahu alikuwa makini kumkosoa Biden pale alipoulizwa kama anamuunga mkono mgombea wa chama cha Republican Donald Trump akisema: “Kama kuna kitu cha mwisho naweza kufanya, basi ni kuingia kwenye medani za siasa za Marekani.”


Alichosema Biden

Kiongozi huyo wa Marekani kwenye mahojiano ya Jumamosi  na kituo cha televisheni cha MSNBC cha Marekani alionyesha kuchoshwa na ongezeko la idadi ya vifo vya Wapalestina huko Gaza vinavyotokana na mashambuli ya Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF).

Alisema mpango wa Israeli wa kuushambulia mji wa Rafah ambao ndio eneo pekee Wapalestina wamekimbilia huko kukwepa mashambuizi ya IDF, itakuwa kuvuka mstari mwekundu kwa Waziri Mkuu Netanyahu, lakini hatoiacha Israeli.

“Ninamfahamu Bibi kwa miaka 50 (Bibi ni jina la utani la Netanyahu). Israeli ina haki ya kujiinda kutokana na mashambullizi ya Hamas, lakini Netanyahu lazima, lazima, lazima awe mwangalifu kuzuia madhara kwa raia Gaza,” alisema Biden na kuongeza: “Anaiumiza Israeli badala ya kuisaidia kwa kuua raia. Hili ni kosa,” alisema Biden.

“Lakini, kuna mstari mwekundu kama atauvuka…,” alisema Biden bila kumalizia itakuwaje huo mstari ukivukwa na kungeza kuwa utawala wake hauwezi kuvumilia vifo vya Wapalestina zaidi 30,000.

Biden alimuonya Netanyahu kwamba asiifanye Gaza kama Marekani ilivyoivamia Iraq na Afghanistan (japokuwa mwanzoni alikosea na kuitaja Ukraine kwamba ndio Afghanistan).

“Haikuwa lazima, haikuwa lazima. Hii ilisababisha matatizo zaidi ya kuyaondoa, zaidi ya kuyatibu,” alisema Biden kuhusiana na matatizo yaliyotokea baada uvamizi wa Marekani katika nchi za Iraq na Afghanistan.

Alisema Israeli haitakiwi kuuvamia mji wa Rafah hadi iweke utaratibu wa kuwaokoa raia wasio na hatia waliokimbilia huko.

Biden alipoulizwa kuhusu mpango wake wa kusimamisha mapigano kama utafanyika kabla ya Waislamu kuanza mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, alijibu hilo linawezekana na hajakata tamaa.


Imeandikwa na Noor Shija.