Papa aziangukia Israel, Palestina kumaliza tofauti zao

Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis
Muktasari:
- Kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis ametoa wito wa amani kufuatia mapigano yanayoendelea kati ya Israel na Palestina ambayo yamesababisha mamia ya watu kuuawa hadi sasa huku wengine maelfu kujeruhiwa.
Vatican. Kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis ametoa wito wa amani kufuatia mapigano yanayoendelea kati ya Israel na Palestina ambayo yamesababisha mamia ya watu kuuawa huku maelfu kujeruhiwa.
Papa ameyasema hayo leo Jumapili Oktoba 8, 2023 mbele ya umati wa waumini baaada ya sala ya Angelus iliyofanyika katika viwanja vya Kanisa la Mtakatifu Petro lililopo Vatican na kunukuliwa na Shirika la habari la AFP.
"Vita ni kushindwa. Vita vyote ni kushindwa. Tuombe kwa ajili ya amani Israel na Palestina," amesema Papa Francis na kuongeza…
"Ninafuatilia kwa wasiwasi na uchungu kile kinachotokea Israel. Ninaelezea mshikamano wangu na familia za wahasithiriwa.”
Papa ameongeza kuwa anawaombea wale wote ambao wanaishi katika nyakati hizi za uchungu.
"Mashambulio na silaha zikome, nakuomba. Ugaidi na vita havileti suluhu, bali ni vifo na mateso ya watu wengi wasio na hatia," alimalizia Papa.
Leo ni siku ya pili ya mapigano yaliyoanza jana baada ya kikundi cha wanamgambo cha Hamas kurusha makombora zaidi ya 5,000 nchini Israel na baadaye Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kutangaza vita kisha kujibu mashambulizi hayo yaliyopelekea mamia ya watu kuuawa.