Rwanda kujenga kinu cha nyukilia kuzalisha umeme

Dar es Salaam. Serikali ya Rwanda inakusudia kujenga kinu cha nyuklia na kukifanyia majaribio ifikapo mwaka 2026, baada ya kuingia makubaliano na kampuni ya Dual Fluid Energy inayofanya kazi kutokea Canada na Ujerumani, kwa ajili ya ujenzi huo.
DW imeripoti kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Goetz Ruprecht, amewaambia waandishi wa habari mjini Kigali jana kuwa aina mpya ya vinu hivyo, vinaweza kutumiwa kuzalisha umeme, haidrojeni na mafuta yaliyosindikwa kwa gharama ndogo.
Waziri wa miundombinu wa Rwanda Ernest Nsabimana amesema matumizi ya nishati ya nyuklia yatatoa chanzo thabiti na cha kuaminika cha umeme, kupunguza utegemezi wa mafuta na kusaidia kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya nishati nchini humo.
Nsabimana amendelea kuwa kujumuisha nyuklia katika jumla ya vyanzo vya nishati kutapelekea kuwa na aina mbalimbali za vyanzo vya nishati, kuimarisha usalama wa nishati na kupunguza hatari ya uhaba wa usambazaji.
Mwaka 2019, Rwanda ilitia saini mkataba wa kuanzisha vinu vya nyuklia kwa ushirikiano na wakala wa nyuklia wa Urusi "Rosatom", jambo lililozusha upinzani mkali hasa kuhusu hatari zinazohusiana na masuala ya kiusalama.
Rais wa chama kikuu cha upinzani nchini humo cha ‘Democratic Green Party of Rwanda,’ Frank Habineza, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa makubaliano kati ya serikali na Kampuni ya Dual Fluid Energy, ni hatari na kwamba hayana tofauti kubwa na makubaliano ya mwaka 2019 kati ya serikali ya Kigali na wakala wa nyuklia kutoka Urusi.
Habineza amesisitiza: "Hakuna utafiti unaoweza kunishawishi kuwa kuna mahali katika nchi hii (Rwanda) ambapo kinu cha nyuklia kinaweza kujengwa bila kuyaweka maisha ya watu hatarini."
Bodi ya Nishati ya Atomiki ya Rwanda, ikishirikiana na Kampuni hiyo wamebainisha kuwa miradi yao ni salama na wala si tishio kwa watu au mazingira. Katika taarifa yao ya pamoja wameeleza: "Kinu chetu cha majaribio ni kifaa kidogo chenye chembechembe ndogo za mionzi. Kwa sababu hii, mradi huu si tishio kwa mazingira."
Taarifa hiyo imeendelea kuelezea kuwa: “Kwa mfano, hata ikitokea mlipuko kwenye kinu hicho au kwenye jengo lenyewe, basi ni kiwango kidogo mno cha mionzi ndicho kitakachotawanyika."
Afrika Kusini ndio nchi pekee barani Afrika iliyo na vinu vy nyuklia ambavyo vimekuwa vikifanya kazi kwa zaidi ya miaka 30 na kuzalisha megawati 1,860 za umeme, ikiwa ni sawa na karibu na asilimia 4 ya nishati yote inayozalishwa nchini humo.