Sultan Qaboos wa Oman afariki dunia

Muscat. Sultani Qaboos bin Said wa Oman aliyeitawala nchi hiyo kwa karibu nusu karne amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 79.
Shirika la habari la taifa hilo limeripoti kuwa Qaboos ambaye amekuwa Sultan wa Oman tangu mwaka 1970 baada ya kumpindua baba yake, amekuwa mgonjwa kwa muda mrefu na inaaminika alikuwa akitibiwa saratani ya utumbo.
Kufuatia kifo chake serikali imetangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa na bendera zitapepea nusu mlingoti kwa siku 40.
Qaboos aliyepata elimu yake nchini Uingereza alifanya mageuzi makubwa nchini Oman, taifa ambalo wakati akichukua madaraka lilikuwa na shule tatu pekee na sheria kandamizi zilizopiga marufuku nishati ya umeme, redio, miwani na hata matumizi ya miavuli.
Chini ya utawala wake, Oman ilikuja kufahamika kuwa eneo linapendelewa zaidi na watalii na taifa kiungo kwenye eneo la mashariki ya kati likisaidia Marekani kuwaokoa wanadiplomasia wake waliokamatwa mateka nchini Iran na Yemen na hata kuwakaribisha maofisa wa Israeli wakati huohuo akipinga ukaliaji wa mabavu ardhi ya Wapalestina.
Nani anaweza kumrithi?
Kulingana na Katiba ya Oman, familia ya Sultani inapaswa kumtaja mrithi wa kiti hicho ndani ya muda wa siku tatu tangu kinapotangazwa kuwa wazi.
Iwapo familia itashindwa kuafikiana kuhusu jina la yule atakayechukua wadhifa huo, mtu aliyeteuliwa na Qaboos kupitia barua kwenda kwa familia yake ndiye atakuwa mrithi wa kiti cha usultani.
Katiba ya Oman imeainisha kuwa sultani anapaswa kuwa sehemu ya familia ya kifalme, muumini wa dini ya Kiislamu, mtu mzima, timamu na mtoto halali wa wazazi Waislamu wa Oman.
Wataalamu wa taratibu hizo wanasema kuna zaidi ya watu 80 wenye sifa za kumrithi Sultani Qaboos.
Asad bin Tariq mwenye umri wa miaka 65 ndiye anatajwa zaidi kuwa jina lake ndio limo kwenye bahasha ya Sultani baada ya kuteuliwa mwaka 2002 kuwa naibu waziri mkuu anayeshughulikia masuala ya kimataifa na mahusiano ya kigeni.
Hatua hiyo ilikuwa ni ujumbe wa wazi kuwa Qaboos alikuwa akimuunga mkono binamu yake huyo.
Wengine wanaoweza kupewa nafasi ni binamu wawili wa Sultan Qaboos, Haitham bin Tariq ambaye ni waziri wa utamaduni na Shihab bin Tariq aliyekuwa mshauri wa karibu wa Qaboos.
Wasiwasi uliopo
Hata hivyo, kifo cha Sultani Qaboos ambaye hakuwa na mke wala watoto hakutaja hadharani mrithi wake, kinaleta wasiwasi wa kutokea machafuko kwenye taifa hilo lenye raia milioni 4.6.