UN yaendela kuibana Rwanda kuhusu M23

Wanajeshi wa Kikosi cha Waasi M23 wenye makazi yao katika kambi ya Rumangabo Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Picha na AFP

Muktasari:

  • UN yaendelea kuishutumu Rwanda kwa kuunga mkono kikundi cha waasi M23, wakieleza katika ripoti yao kwamba nchi hiyo bado inaendelea kukiunga mkono kikosi hicho kupitia uimarishaji wa wanajeshi na vifaa.

Kongo. Kwa mara nyingine tena, Umoja wa Mataifa UN umeishutumu Rwanda kwa kutoa msaada kwa waasi wa kundi la 'Mouvement du 23 mars' (M23) wanaopigana na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Kwa mujibu wa kituo cha habari ‘The EastAfrican’ wameeleza kwamba, ripoti mpya ya kundi la wataalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu DRC, inadai kuwa Rwanda inaunga mkono kikosi cha waasi M23 kupitia uimarishaji wa wanajeshi na vifaa.

Kwa upande mwingine, ripoti hiyo ya UN pia imeweka wazi majina ya makamanda wakuu watano wa Jeshi la Ulinzi la Rwanda kama waratibu.

Ripoti ya Juni 13, 2023 kwa Rais wa Baraza la Usalama la umoja huo inaonya kwamba kuzorota kwa uhusiano kati ya Kinshasa na Kigali kunaleta tishio la usalama katika eneo hilo.

Machi mwaka huu, DRC ilidai kuwa Rwanda ilituma vikosi vya kijeshi na vifaa kwa M23 nchini DRC.

Wakati Kigali inakanusha hili, ikiwa ni pamoja na kujibu maombi ya taarifa kutoka kwa wataalamu wa Umoja wa Mataifa walioandika ripoti hiyo, Umoja wa Ulaya na Marekani zimeitaka Rwanda kuacha kulisaidia kundi la waasi lililoidhinishwa na Umoja wa Mataifa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, matukio ya vurugu kubwa yameathiri majimbo matatu ya mashariki mwa DRC ambayo ni Kivu Kusini, Kivu Kaskazini na Ituri; yaliyosababishwa na mapigano kati ya M23 na Jeshi la Kongo (FARDC), na pande zote mbili zikilaumiana.

"Licha ya juhudi za nchi mbili, kikanda, na kimataifa za kupunguza mzozo unaohusiana na kundi hilo la 'Mouvement du 23 mars' (M23), bado limeendelea kupanua eneo lake na kuongeza mashambulizi," sehemu ya ripoti imesema.

Ofisi ya Mawasiliano ya Serikali ilibainisha jinsi maelezo ya usaidizi wa kifedha, silaha na bima ya kisiasa iliyotolewa kwa FDLR na Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na inathibitisha kwamba, pamoja na vikosi vingine haramu vya silaha, FDLR inapigana pamoja na jeshi la Kongo (FARDC) ambapo kwa  mara kadhaa katika mwaka uliopita walikua wanakiuka eneo la Rwanda.

Hata hivyo, majibu ya Rwanda dhidi ya shutuma ya jeshi lake hayamo kwenye ripoti hiyo.