Waandamanaji Kenya wamuua Ofisa wa polisi kwa jiwe

Maofisa wa Polisi nchini Kenya wakiwarushia waandamanaji gesi ya kutoa machozi kutawanya maandamano nchini humo.

Muktasari:

  • Kufuatia maandamano yanayoendelea nchini Kenya yakiongozwa na kiongozi wa Azimio la Umoja Raila Odinga, jana waandamanaji wamemuua ofisa wa polisi kwa jiwe.

Kenya. Ofisa wa Polisi kaunti ya Kisumu nchini Kenya, ameuwa kwa kupigwa na jiwe kifuani wakati wa maandamano nchini huo yaliyofanyika jana.

Ofisa huyo aliyetambulika kwa jina la Ben Oduor baada ya kupata dhoruba ya kupigwa na jiwe kifuani ilitushwa kwa manati, alikimbizwa Hospitali ya Aga Khan katika chumba maalumu cha wagonjwa mahututi na baada ya muda alipoteza maisha jana usiku.

Kamanda wa Polisi eneo la Nyanza nchini humo Noah Mwivanda amesema marehemu alirushiwa jiwe hilo kwa  manati ya kutengeneza wakati polisi wakikabiliana na waandamanaji.

“Maofisa wetu wapo kwenye msako mkali kuitafuta manati hiyo ambayo tumeitambua kama silaha mbaya,

Silaha hii ni mbaya hata kwa wanaotumia, tunamtaka yeyote anayemiliki au mtu mwenye taarifa za anayemiliki awasilishe taarifa hizo kituo cha polisi kilichopo karibu naye,” amesema.

Baadhi ya wanasiasa nchini Kenya akiwamo kiongozi wa Azimio  Raila Odinga wanaongoza maandamano  nchini humo wakishinikiza Serikali kutimiza matakwa kama vile kupunguzwa kwa gharama ya juu ya maisha na kuunda upya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Tayari mwili wa ofisa huyo umetolewa katika chumba  maalumu cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Aga Khan na wanaume wawili waashikiliwa kufuatia mauaji hayo na watakabiliwa na shtaka la mauaji.


Imeandaliwa na Baraka Loshilaa.