Wabunge waliosimama na Gachagua hawa hapa
Muktasari:
- Ni wabunge watano pekee kutoka Kaunti ya Murang’a waliojitenga na hoja ya kumtimua, wakisema itakuwa na athari kubwa za kijamii, kisiasa na kiuchumi katika eneo la Mlima Kenya.
Dar es Salaam. Wabunge 58 wa Bunge la Kitaifa la Kenya hawakutia saini hoja ya kumtimua Naibu Rais, Rigathi Gachagua iliyowasilishwa rasmi katika Bunge hilo, Jumanne Oktoba Mosi, 2024.
Haijabainika iwapo baadhi ya wabunge hao walikataa kutia saini hoja hiyo kwa sababu ya kutokuwemo ndani ya Bunge kwa sababu moja au nyingine au wanapinga kumrudisha Gachagua nyumbani.
Ni wabunge watano pekee kutoka Kaunti ya Murang’a waliojitenga na hoja ya kumtimua, wakisema itakuwa na athari kubwa za kijamii, kisiasa na kiuchumi katika eneo la Mlima Kenya.
Wabunge hao ni Wakili Edward Muriu (Gatanga), Mary Wamaua (Maragua), Peter Kihungi (Kangema), Joseph Muiotoro (Kigumo) na Chege Njuguna (Kandara).
“Ni wito wetu kama wabunge kutoka Kaunti ya Murang'a kuwaomba wenzetu kuwa waangalifu katika kushughulikia hoja hii kwa sababu maslahi ya taifa ni makubwa kuliko maslahi ya mtu binafsi,” wabunge hao walisema kwenye taarifa yao ya pamoja.
“Haitakuwa rahisi kama unavyofikiri, Gachagua kuondolewa kwake madarakani,” wamesema.
Ahukumiwa bila kusikilizwa
Wabunge hao walikashifu kile walichokitaja kama Bunge kumshtaki Gachagua bila kusikilizwa, kinyume na Katiba.
“Hoja ya kushtakiwa bungeni chini ya Kifungu cha 150 cha Katiba hakitoi fursa ya kujitetea tuhuma dhidi yake,” wabunge walisema kwenye taarifa hiyo ya pamoja.
Wabunge hao waliapa kupiga kura kupinga hoja hiyo.
Katika orodha ya waliopinga hoja ya kuondolewa madarakani ni Mbunge wa Kiharu, Ndindi Nyoro na Babu Owino wa Embakasi Mashariki kupitia chama cha Orange Democratic Movement (ODM).
Nyoro, ambaye aliwahi kupigiwa debe kuchukua nafasi ya Gachagua kama Naibu Rais, hakuwa miongoni mwa wabunge ambao majina yao yalisomwa katika ukumbi wa Bunge.
Owino hajaweka wazi kuiunga mknono serikali inayosimamiwa na Rais William Ruto na mwenzake wa ODM, Raila Odinga.
Jina lake halikuonekana kwenye orodha hiyo licha ya wabunge wengi washirika wa ODM kutia saini zao kuunga mkono.
John Kaguchia wa Mukurweini, ndiye mbunge pekee kutoka Kaunti ya Nyeri ambaye hakutia saini hoja hiyo, bali aliwataka Rais Ruto na Gachagua kumaliza tofauti zao.
Wasioridhishwa na msingi wa hoja
Mbunge wa Kitui ya Kati, Makali Mulu aliiambia Daily Nation kuwa chama chake cha Wiper hakiungi mkono hoja hiyo ya kumuondoa Gachagua madarakani.
“Sina hakika kuwa kuna sababu za kumshtaki Gachagua. Tutapinga hoja kama Wiper. Ikiwa ni kushtakiwa, Rais Ruto anafaa kurejeshwa nyumbani pia. Hakuna jambo ambalo Gachagua amefanya ambalo Rais hajafanya,” Dk Mulu ameliambia Nation.
Amerejelea kikao cha NEC cha Wiper Ijumaa iliyopita ambapo chama hicho kiliazimia kupinga hoja hiyo.
Wiper ina wabunge 25 katika Bunge la Kitaifa huku Chama cha Democratic Action Party of Kenya (DAP-K) kikiwa na watano.
Ili kumshtaki Naibu Rais, wanaomuunga mkono ni lazima wapate uungwaji mkono wa angalau wabunge 233. Ili kuwasilisha bungeni, ni saini 117 pekee zilizohitajika.
Timu ya Gachagua inapanga kufanya kazi na wabunge wa Jubilee, Wiper na DAP-K kukanusha hoja hiyo ya wabunge 233. Wakati wabunge 291 wakiwa wametia saini kuunga mkono hoja hiyo, huenda ikawa ni mwisho wa Gachagua, labda kama baadhi walio kwenye orodha hiyo inasemekana hawatajitokeza siku ya kupiga kura.
Ambao majina yao hayakuwa kwenye orodha hiyo ni pamoja na Babu Owino (Embakasi Mashariki), Ndindi Nyoro (Kiharu), Gathoni Wamuchomba (Githunguri), Makali Mulu (Kitui ya Kati), Robert Mbui (Kathiani), Benjamin Gathiru ( Embakasi ya Kati), James Gakuya (Embakasi Kaskazini), John Kaguchia (Mukurweini), Wakili Edward Muriu (Gatanga), Mary Wamaua (Maragua), Peter Kihungi (Kangema), Joseph Muiotoro (Kigumo), Chege Njuguna (Kandara), Amos Mwago (Starehe), Timothy Kipchumba (Marakwet Mashariki), Peter Salasya (Mumias Mashariki), Jayne Kihara (Naivasha), Njeri Maina (Mwakilishi wa Wanawake wa Kirinyaga), Samuel Gachobe (Subukia) na George Koimburi wa Juja.