Wakenya wamsaka Jaji Mkuu, usaili waonyeshwa 'live'

Wakenya wamsaka Jaji Mkuu, usaili waonyeshwa 'live'

Muktasari:

  • Kenya imeanza kutafuta jaji mkuu mpya baada ya wa sasa kustaafu na kazi hiyo inafanywa kwa jopo maalum kusaili majaji tisa waliopita katika mchujo ili kupata majina matatu yatakayopelekwa kwa Rais Uhuru Kenyatta kwa ajili ya uteuzi.

Kenya imeanza kutafuta jaji mkuu mpya baada ya wa sasa kustaafu na kazi hiyo inafanywa kwa jopo maalum kusaili majaji tisa waliopita katika mchujo ili kupata majina matatu yatakayopelekwa kwa Rais Uhuru Kenyatta kwa ajili ya uteuzi.


Usaili huo, unafanywa kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Jaji David Maraga aliyestaafu, unaonyeshwa moja kwa moja na televisheni.


Katika jopo hilo yumo Naibu Jaji Mkuu, Philomena Mwilu, ambaye amekuwa akikaimu nafasi hiyo tangu Maraga alipostaafu mwezi Januari. Pia yumo makamu mwenyekiti wa Tume ya Huduma za KImahakama (JSC), Jaji Mohammed Abdullahi Warsame.


Mtu wa kwanza kuhojiwa jana Jumatatu alikuwa Jaji Said Juma Chitembwe.


"Kama nikiteuliwa, nitaanzia pale wengine walipoishia nikiwa na lengo pekee la kuboresha taasisi ili iwe vile inavyoweza kuwa, kwa mujibu wa dira yake," alisema Jaji Chitembwe mwanzoni mwa usaili huo.


Washindani wake ni Profesa Patricia Mbote, Jaji Martha Koome, Jaji Marete Njagi, Philip Murgor, Jaji Nduma Nderi, Fred Ngatia, Jaji William Ouko, Dk Wekesa Moni na Alice Yano.

Mgongano wa maslahi
Kuhusu ushiriki wa Jaji Mwilu, JSC haijaweka uzito katika suala la mgongano wa maslahi linalomuhusu mmoja wa wanaowania nafasi hiyo, uamuzi ulioruhusu usaili kuanza.


Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma wa zamani, Philip Murgor aliiandikia JSC akitaka Jaji Mwilu aondolewe katika usaili, akidai kuwa anaweza kuwa na upendeleo kwa mgombea mwingine wa nafasi hiyo, Fred Ngatia.


Katika barua yake, Murgor alidai kuwa Jaji Mwilu na Ngatia walishakuwa na uhusiano wa wakili na mteja zamani, na kwamba historia yao inaweza kusababisha upendeleo katika usaili.


Jopo hilo litakuwa likimuhoji mtu mmoja kwa siku na kwamba utafanyika nje katika jitihada za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.


Jaji Said Juma Chitembwe wa Mahakama Kuu alionekana kuwa na hisia jana Jumatatu na kulia wakati usaili ukiendelea.
Chitembwe alikuwa akijibu swali la Kamishna Evelyne Olwande wa Tume ya Huduma za Kimahakama (JSC) kuhusu haki ya dhamana kwa watuhumiwa.


Alionekana kuwa na hisia alipotumia uzoefu wake binafsi wakati aliposhtakiwa kwa ufisadi na mahakama ikachukua zaidi ya mwezi kuamua kama anastahili dhamana.


Alishtakiwa wakati akiwa katibu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), ambayo aliifanya kabla ya kuwa jaji.


"Ukipitia mchakato huu unaujua vizuri zaidi. Uzoefu binafsi ulihusu mimi na ofisa mtendaji mkuu wa NSSF kushtakiwa, baadaye wanasheria wawili wakaunganishwa katika kesi kwa lengo la kuichelewesha, walifungua kesi kusimamisha kusikilizwa kwa kesi," alisema Chitembwe kwa hisia.


Alisema kuwa bado hajaelewa sababu za ombi lake la dhamana kuchukua siku 30.


"Ni yule anayevaa kiatu ndiye anayekijua, lakini suala langu haliwezi kuwa mfano mbaya kwa sababu tulisikilizwa na mahakama ikaamua ndani ya mwaka mmoja kuwa hakukuwa na kesi ya kujibu."


Jaji huyo alisema Wakenya wengi wanaishia kukaa mahabusu siku nyingi wakati uamuzi wa kupata dhamana au kutopata linatakiwa liamuliwe haraka.


Alisema kuwa amejifunza kutokana na uzoefu kuwa kuna haja ya kuwasikiliza watuhumiwa kabla ya kutoa hukumu.
"Unapokuwa ofisa anayefanya uamuzi, unatakiwa uweze kumsikiliza mtu aliye mbele yako,” aliongeza.


Awali, jaji huyo alitakiwa na Jaji Philomena Mwilu kuieleza kamisheni baadhi ya mabadiliko ambayo anapanga kuyafanya.
Chitembwe alijibu kuwa hadhani kama kuna matatizo yoyote katika Mahakama ya Juu yanayohitaji kubadilishwa.