Wanajeshi wa Marekani wamuua kiongozi mkuu Islamic State

Muktasari:

  • Wanajeshi wa Marekani waliovamia nchini Somalia, wamefanikiwa kumuuwa kiongozi mkuu wa kundi la kigaidi la Islamic State.

Dar es Salaam. Maafisa wa Marekani wamesema uvamizi wa kijeshi uliofanywa na taifa lao huko nchini Somalia ulioamriwa na Rais Joe Biden, wamefanikiwa kumuua kiongozi mkuu wa kikanda wa Kundi la Islamic State, Bilal al-Sudani.

Kulingana na kituo cha habari ‘AFP’ wameeleza kwamba, Sudan aliuawa wakati wa mapigano ya risasi baada ya wanajeshi wa Marekani kuteremka kwenye pango la milima kaskazini mwa Somalia wakitarajia kumkamata, kulingana na maofisa wa Marekani.

Takriban washirika 10 wa IS katika eneo la tukio waliuawa, lakini hakukuwa na majeruhi wa Marekani, maafisa walisema.

"Januari 25, kwa amri ya rais, Jeshi la Marekani lilifanya operesheni ya mashambulizi kaskazini mwa Somalia ambayo ilisababisha vifo vya wanachama kadhaa wa ISIS, akiwemo Bilal al-Sudani," Waziri wa Ulinzi Lloyd Austin alisema katika taarifa yake.

"Al-Sudani alikuwa na jukumu la kukuza uwepo wa ISIS unaokua barani Afrika na kufadhili shughuli za kikundi hicho kote ulimwenguni, pamoja na Afghanistan," Austin alisema.
Kutoka kwenye ngome yake ya milimani kaskazini mwa Somalia, alitoa na kuratibu ufadhili kwa matawi ya IS, sio tu barani Afrika bali pia Islamic-State.
Miaka kumi iliyopita, kabla hajajiunga na Islamic State, Sudani alihusika katika kuwasajili na kuwafunza wapiganaji wa vuguvugu la itikadi kali la al-Shabaab nchini Somalia.

Inaelezwa, operesheni hiyo ilikuwa imetayarishwa kwa muda wa miezi kadhaa, huku vikosi vya Marekani vikifanya mazoezi katika eneo lililojengwa ili kuigia eneo ambalo Wasudani walikuwa wamejificha.

"Rais Biden ameweka wazi kwamba tumejitolea kutafuta na kuondoa vitisho vya kigaidi kwa Marekani na kwa watu wa Marekani, popote walipo kujificha, bila kujali ni mbali kiasi gani," afisa huyo alisema.
Majeshi ya Marekani yamekuwa yakifanya kazi nchini Somalia kwa muda mrefu kwa uratibu na kwa niaba ya serikali, wengi wao wakifanya mashambulizi ya angani ili kuunga mkono vikosi rasmi vinavyopambana na waasi wa Shabaab.