Watalii kutoka China kuwasiri nchini

Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki

Muktasari:

  • Tanzania inatarajia kupokea kundi la watalii kutoka nchini China Kesho Mei 12, 2023 ambao kwa muda wa wiki moja, wanatarajia kutembelea maeneo mbalimbali ya vivutio katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam na Zanzibar ndani ya wiki moja watakayotumia.

Dar es Salaam. Ujumbe wa watalii kutoka nchini China unatarajiwa kuwasili nchi Mei 12, 2023 kwa ajili ya ziara ya wiki moja huku wakilenga kutembelea maeneo mbalimbali yenye vivutio ikiwemo Zanzibar, Arusha, Mara na Dar es Salaam.

Mbali na kutembelea vivutio hivyo, kila eneo watakalofika watafanya vikao na wadau mbalimbali wa sekta ya utalii ikiwemo wamiliki wa hoteli na wasafirishaji watalii.

Ujumbe huo utajumuisha Kampuni 14 zinazoongoza katika kusafirisha watalii nchini China, vyombo sita vya habari kutoka Majimbo ya China pamoja watu wenye ushawishi nchini humo.

Akizungumzia ujio huo, Balozi wa Tanzania nchini China Mbelwa Kairuki amesema hii ni fursa kwa wadau wa utalii nchini kuandaa taarifa zao ili ziweze kuwasilishwa kwa kampuni hizo huku akishauri kuwa ikiwezekana ni vyema zikawa katika lugha ya kichina.

 "Pia ingekuwa ni vyema zaidi kama taarifa hizi zingewekwa katika mfumo wa soft copy ili muonekane mnaenda na wakati," amesema Kairuki.

Kwa mujibu wa Kairuki, ziara hiyo imeandaliwa na Ubalozi wa Tanzania kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii (TTB), Kamisheni ya Utalii Zanzibar na kufadhiliwa na Benki ya NMB na Shirika la Ndege la Tanzania.

Akizungumzia sehemu watakazotembelea, Kairuki alisema Mei 12 ujumbe huo utashukia katika uwanja wa Amani Abeid Karume na wakiwa Zanzibar watapata fursa ya kutembelea maeneo ya vivutio vya Utalii.

Mei 13 watakutana na wadau wengine wa utalii wa Zanzibar wamiliki hoteli na watoa huduma za utalii Zanzibar na  watakapomaliza Zanzibar Mei 17 watakwenda Arusha ambapo watatembelea, Ngorongoro, Tarangire na Serengeti kabla ya kufanya mkutano na wadau wa utalii katika siku inayofuata katika hoteli ya Grand Mellia.

"Mei 23 watalii hao watakwenda jijini Dar es Salaam ambapo miongoni mwa sehemu zitakazotembelea ni Stesheni ya Tazara ambayo ina historia katika mahusiano ya Tanzania na China," alisema Kairuki.