Watano wauawa kwa kuchinjwa Kenya

Muktasari:
- Magaidi waliojitambulisha kama wanamgambo halisi wa Al-Shabaab katika vijiji vya Salama na juhudi Tarafa ya Mkunumbi, Kaunti ya Lamu wamewaua watu watano na kuteketeza nyumba zaidi ya tano nchini Kenya.
Kenya. Kikundi cha Al-Shabaab kimevamia vijiji viwili vya Salama na Juhudi vilivyopo katika Tarafa ya Mkunumbi, Kaunti ya Lamu na kuua watu watano na kuteketeza nyumba zaidi ya tano.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Taifa Leo, zimesema kuwa kuamkia Juni 24, 2023 majira ya saa moja na nusu jioni Magaidi waliojihami na silaha hatari kama bunduki, mapanga na visu waliingia katika vijiji hivyo wakiwashurutisha wakazi kutoka kwenye nyumba zao hasa wanaume na kuwachinja.
Inasemekana kuwa miongoni mwa waliouawa yupo mwanafunzi wa kidato cha tatu anayesoma Shule ya Sekondari Bakanja ililopo katika eneo la Mpeketoni, Barrack Hussain (19) aliyefika nyumbani kwao jioni ya siku hiyo kwa ajili ya likizo.
Akizungumza na Taifa Leo jana Jumapili Shangazi wa mwanafunzi aliyeuawa, Pamela Ogutu amesema magaidi hao walikuwa wamevaa sare zinazofanana na zile za polisi na jeshi, huku wengine wakiwa wamevaa fulana za rangi ya kijani na chini wakiwa wamefunga vikoi.
“Walipofika walituamuru tulale chini bila kupiga kelele na kujitambulisha kuwa wao ni wanamgambo halisi wa Al-Shabaab na wamekuja kutuua. Pia wametudokezea ujumbe wa kumfikishia rais wetu kuwa hawakuridhika na Serikali ya Kenya kufungua mpaka na kuachilia maofisa wa ulinzi kushambuli na kuua watu wao, baada ya hapo walimkaribia kijana Barrack Hussain na kumfunga kwa kamba miguuni na mikononi kisha wakamfunika uso na kumpiga risasi tumboni na baadaye kumchinja shingoni,” amesema Ogutu.
“Baada ya kumuua kijana wetu walituamuru sisi wanawake turudi ndani ya nyumba na walienda hadi kwenye stoo yangu ambapo waliiba vyakula, mbuzi, simu na fedha taslimu Sh1,040,000 kisha kuiteketeza stoo yangu,” ameongezea Ogutu.