Zifahamu nchi zilizopo chini ya Mfalme wa Uingereza

Muktasari:
- Ufalme wa Uingereza hauishii Uingereza tu bali zipo nchi 15 kwa ujumla zinazotambua Charles kama Mfalme wao.
Dar es Salaam. Ukiachana na nchi 56 za Jumuiya ya Madola unafahamu kwamba Mfalme Charles III ni kiongozi (Mfalme) wa nchi 15 ikiwemo Uingereza yenyewe.
Juzi Mfalme Charles III alitawazwa kuwa kiongozi wa Uingereza lakini ndiye Mfalme na mkuu wa nchi 14 huru zinazomtambua kama kiongozi wake.
Nchi hizo ni, Antigua na Barbuda, Australia, Bahamas, Belize, Kanada, Grenada, Jamaika, New Zealand, Papua New Guinea, Saint Kitts na Nevis, Saint Lucia, Saint Vincent na Grenadines, Visiwa vya Solomon, Tuvalu na Uingereza yenyewe.
Nchi hizi 14 zinazoitwa "Commonwealth Realms" zilikuwa sehemu ya Milki ya Uingereza, ambazo zilipata uhuru. Ndani yao kuna Gavana mkuu, sawa na Rais katika Jamhuri, ambaye ni mwakilishi wa Mfalme/Malkia katika kila taifa.
Mataifa haya mengi yakiwa ni visiwa yanapatikana Asia na Amerika, Antigua na Barbuda ni nchi huru ya Jumuiya ya Madola inayojumuisha visiwa vyake viwili. Inapatikana mahali ambapo bahari ya Atlantiki na Karibea hukutana, inaongozwa na Waziri Mkuu.
Australia, ikiwa ni nchi ya sita kwa ukubwa duniani ni sehemu ya Jumuiya ya Madola ikiwa chini ya Mfalme wa Uingereza. Inaongozwa na Waziri Mkuu kwa mfumo wa Bunge na Ufalme wa Shirikisho.
Bahamas ikiwa ni Jumuiya ya Madola ni nchi ya kisiwa ndani ya visiwa vya Lucayan vya West Indies katika bara la Amerika ya Kaskazini. Inaongozwa na Waziri mkuu.
Belize ni taifa lililo kwenye pwani ya Mashariki ya Amerika ya Kati, ni moja kati ya mataifa yanayoongozwa na Mfalme wa Uingereza.
Kanada ni nchi iliyoko Amerika Kaskazini ni nchi ya pili kwa ukubwa duniani kwa jumla ya eneo, na ukanda wa pwani mrefu zaidi ulimwenguni. Iko chini ya Mfalme Charles III, kiserikali inaongozwa na Waziri Mkuu.
Grenada ni nchi ya Karibiani inayojumuisha visiwa vidogo vinavyozunguka eneo lake ni moja ya nchi zilizochini ya Mfalme wa Uingereza. Inaongozwa na Waziri Mkuu.
Jamaika, taifa la visiwa vya Karibea, ni taifa lililochini ya Mfalme Charles, inaongozwa na Waziri Mkuu. New Zealand pia ni nchi ya kisiwa kusini magharibi mwa Bahari ya Pasifiki moja ya sehemu ya uongozi wa Mfalme.
Papua New Guinea, Kusini Magharibi mwa Pasifiki, inaongozwa na Waziri Mkuu huku Mfalme Charles akiwa ndio mkuu wa nchi hiyo. Saint Kitts na Nevis ni taifa la visiwa viwili lililo kati ya Bahari ya Atlantiki na Bahari ya Karibi lililochini ya Mfalme Charles huku likiongozwa na Waziri Mkuu.
Saint Lucia ni taifa la Kisiwa cha Karibea Mashariki katika bara la Amerika ya Kaskazini linaloongozwa na Waziri Mkuu aliye chini ya Mfalme wa sasa Charles III.
Vincent na Grenadines ni taifa la kusini mwa Karibea linalojumuisha kisiwa kikuu na msururu wa visiwa vidogo. Mfalme wa sasa wa taifa hili ni Mfalme Charles III.
Visiwa vya Solomon, taifa la mamia ya visiwa katika vinavyopatikana eneo la bahari ya Pasifiki ya Kusini, Solomon inaongozwa na Waziri Mkuu huku utawala ni mfumo wa serikali ambao mfalme ndiye mkuu wa nchi. Mfalme wa sasa tangu 8 Septemba 2022, Charles III.
Tuvalu, inalopatikana bahari ya Pasifiki ya Kusini, ni taifa huru la kisiwa ndani ya Jumuiya ya Madola ya Uingereza. Utawala wa kifalme wa Tuvalu ni mfumo wa serikali ambao Mfalme Charles III ndiye mkuu.
Mwisho ni Uingereza, inayoundwa na Scotland, Wales na Ireland ya Kaskazini, ni taifa la visiwa Kaskazini Magharibi mwa Ulaya. Mfalme wa sasa ni Mfalme Charles III, ambaye alipata kiti cha enzi mnamo 8 Septemba 2022, baada ya kifo cha mama yake, Malkia Elizabeth II.
Mamlaka ya Ufalme kwenye mataifa haya
Akiwa kama mkuu wa nchi Mfalme katika mataifa haya ana majukumu ya kikatiba, muhimu zaidi ni kuidhinisha Serikali mpya. Kulingana na nchi, anaweza kuidhinisha rasmi sheria, kuteua maofisa au kutoa heshima za serikali.
Katika maeneo yasiyo ya Uingereza, Mfalme huteua mwakilishi wa kifalme kutekeleza majukumu haya ambaye hujulikana kama Gavana Mkuu.
Katika hali ya kipekee taji la Mfalme (Mamlaka) pia lina kile kinachojulikana kama ‘mamlaka ya akiba’ au mamlaka ya kupindua matawi mengine ya serikali.
Hii imetokea mara chache tangu vita ya dunia ya pili, nchini Australia ambapo kulikuwa na mzozo wa kikatiba mwaka 1975, ambapo Gavana Mkuu alimfukuza kazi Waziri Mkuu.
Madhumuni ya Mfalme ni kutumika kama kiongozi asiyegemea upande wowote wa taifa, mwendelezo wa kikatiba, na mamlaka ya kimaadili. Aidha safari za kifalme katika maeneo ya Jumuiya ya Madola zimesaidia kuibua uaminifu katika nchi hizo.