Zuma apiga kura akishangiliwa na mamia ya wafuasi

Mwenyekiti wa chama cha uMkhonto we Sizwe (MK), Jacob Zuma akipiga kura
Muktasari:
- Zuma aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini na miongoni mwa wapigania uhuru wa taifa hilo, alijivua uanachama wa ANC Disemba 2023 na kuanzisha chama chake cha uMkhonto weSizwe (MK), akilenga kugombea urais.
Afrika Kusini. Mamia ya wafuasi wa Mwenyekiti wa chama cha uMkhonto we Sizwe (MK), Jacob Zuma wamelipuka kwa furaha kiongozi huyo alipowasili kupiga kura katika kijiji chake cha Nkandla.
Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Zuma mwenye umri wa miaka 82 aliwasalimu maofisa na kisha kuketi chini katika Shule ya Msingi ya Ntolwane akiwa amevaa fulana nyeupe yenye rangi za kijani na nyeusi za chama chake, ndipo wafuasi wake walipomshangilia huku wakiimba majina ya ukoo wake ‘Nxamala!’, ‘Msholozi!’
Baada ya kitambulisho chake kukaguliwa na dole gumba lake la kushoto kupakwa wino, alipewa karatasi tatu za kupigia kura.
Alizikagua kwa uangalifu, akatabasamu na kusema "kila kitu kiko sawa, naweza kuona uso wangu kwenye karatasi za kupigia kura,” amesema Zuma akinukuliwa na BBC.
Zuma alizuiwa kugombea uchaguzi na mahakama kuu ya Afrika Kusini siku tisa zilizopita baada ya Mahakama ya Kikatiba kuamua kwamba kifungo chake cha miezi 15 gerezani kwa kudharau mahakama kilimfanya asistahili kushiriki kwenye kinyang'anyiro hicho.
Hata hivyo, picha yake bado inaonekana kwenye karatasi za kupigia kura.
Baada ya kuingia kwenye kibanda cha kupigia kura, aliweka karatasi zote tatu za kupigia kura ndani ya sanduku na akaaga. Aliwasiliana kwa ufupi na wafuasi wake kabla ya kuondolewa haraka na walinzi wake.
Uchaguzi wachelewa kuanza
Awali kulikuwa na taarifa za ucheleweshaji wa kupiga kura katika vituo vingi nchini kote nyakati za asubuhi ya leo.
Taarifa zinaeleza kuwa katika jiji la sita kwa ukubwa nchini humo, Gqeberha, upigaji kura katika Shule ya Sekondari ya Cape Recife ulisimamishwa kutokana na mihuri ya masanduku mawili ya kura kuvunjika.
Masanduku hayo yalibeba karatasi za kura za waliopiga ‘kura maalumu’ mapema wiki hii, kwa kuwa wasingeweza kusafiri kwenda kituo chao cha kupigia kura leo.
Maofisa wa Tume Huru ya Uchaguzi (IEC) wamesema wanasikitika kwa ucheleweshaji huo, lakini wanataka mambo yafanyike kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo IEC imetoa taarifa ikisema wakati uchaguzi ulipotarajiwa kuanza, asilimia 93 ya vituo vya kupigia kura vilikuwa vimefunguliwa na vilivyobaki vilifunguliwa ndani ya saa moja.
Naibu Ofisa Mkuu wa uchaguzi, Masego Shiburi amesema ucheleweshaji ulisababishwa na kutokuwa na maofisa wa usalama wa kutosha kusindikiza vifaa.
Shiburi pia ameeleza changamoto ya mtandao wa intaneti ilivyoathiri skana zinazotumika katika vituo vya kupigia kura.
Skana hizo hutumika kukagua kitambulisho cha mpigakura, hivyo baadhi ya maofisa wa uchaguzi waliambiwa kukagua vitambulisho kwa mkono dhidi ya orodha ya wapigakura, jambo ambalo Shiburi amesema limesababisha ucheleweshaji mkubwa.
Taarifa pia zimesema kuwa maandamano ya jamii katika Eastern Cape na KwaZulu Natal pia yalichelewesha shughuli katika vituo vya kupigia kura 25, lakini upigaji kura sasa unaendelea, amesema.