‘Acheni kuwaadhibu watoto mkiwa na hasira’

New Content Item (1)
Hakimu Mkazi kutoka Mahakama ya Mwanzo ya Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, John Mugonya akizungumza wakati wa hafla ya utambulisho wa mradi wa upatikanaji haki unaoratibiwa na Shirika la Valuable and Determined Community Aid (VADECA) iliyofanyika katika ofisi za kata ya Butimba jijini humo. Picha na Anania Kajuni. 

Muktasari:

Machi 3 mwaka huu,  Jeshi la Polisi mkoani Mwanza lilitoa taarifa ya kumshikilia George Shaban (55) Mkazi wa Mahina mkoani humo kwa tuhuma za kumuua mtoto wake Emmanuel Shaban (14) baada ya kumshambulia kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili kwa kosa la kuchuma mahindi mawili kutoka kwenye shamba la jirani yake bila kuomba.

Mwanza. Wazazi nchini wametakiwa kuepuka kutoa adhabu kwa watoto wao wakiwa na hasira pindi wanapowakosea au kufanya kinyume na na matarajio yao ili kuepusha madhara mbalimbali ikiwemo vifo vya ghafla wakati wa kuwaadhibu.

Machi 3 mwaka huu,  Jeshi la Polisi mkoani Mwanza lilitoa taarifa ya kumshikilia, George Shaban (55) Mkazi wa Mahina mkoani humo kwa tuhuma za kumuua mtoto wake Emmanuel Shaban (14) baada ya kumshambulia kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili kwa kosa la kuchuma mahindi mawili kutoka kwenye shamba la jirani yake bila kuomba.

Akizungumza kwa njia ya simu na Mwananchi leo Ijumaa, Machi 24, 2023 Mratibu wa Shirika la Valuable and Determined Community Aid (VADECA) Wilaya ya Nyamagana, Fredy Kate amesema kutoa adhabu kwa mtoto ukiwa na hasira inaweza kupelekea kumwadhibu bila kuangalia mahali sahihi nakumsababishia madhara kama majeraha ya kudumu, ulemavu, makovu na hata kifo.

“Jamii au wazazi wafahamu kabisa kuwa unapomwadhibu mtoto kwa kutumia hisia au hasira unaweza kusababisha vitu ambavyo havikuwa matarajio yako kwahiyo  kumwadhibu mtoto kwa upendo ni njia nzuri zaidi,”

“Wewe kama mzazi unapokaa na kumtengenezea mazingira rafiki na ya upendo yanakufanya wewe kufikia kwa urahisi na wepesi mambo yake yanayomsibu kila siku kwenye michezo yake ya kutwa na inakurahishia wewe kujua kuwa leo mwanangu amekutana na nani, kitu gani kilikuwa cha kumdhuru na salama kwake,” amesema Kate

Akizungumza kwenye hafla ya utambulisho wa mradi wa upatikanaji haki ulioanza kutekelezwa Oktoba 2022 na shirika hilo, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo wilayani Nyamagana, John Mugonya ametoa wito kwa jamii na wadau mbalimbali kulitambua kundi la vijana na watoto wakiume kama kundi maalumu linalohitaji elimu ya ukatili.

"Katika dira yenu hii mna nia ya kuwasaidia watoto wa kike pamoja na wanawake lakini kuna kundi mmeliacha nyuma na linakumbana sana na ukatili na kundi hili ni vijana wakiume na lenyewe kwa sasa linaanza kuwa kundi maalumu na sisi tulio Mahakamani tunapata kesi nyingi sana zinazohusu watoto wa kiume,”amesema Mugonya.

Mwenyekiti wa Kampeni ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) wilaya ya Nyamagana, Ester Moris amesema wazazi wanatakiwa kuwa makini sana na kundi hilo na kujenga tabia ya kuwachunguza na kuwakagua watoto wao mara kwa mara ili kubaini kama wapo salama.

“Huko nyuma tulikuwa tumezoea ukatili ulikuwa unafanyika sana kwa wanawake na watoto wa kike lakini kwa sasa kidogo hali imebadilika kundi la vijana wetu wa kiume lipo kwenye hatari kubwa ya kukumbana na vitendo hivyo,”amesema Moris.

Akizungumzia mafanikio ya mradi huo, Mkurugenzi wa Shirika hilo wilaya ya Nyamagana, Samuel Lusesa amesema katika kipindi cha miezi sita ya mradi huo katika kata 13 za wilaya ya Nyamagana mkoani humo jumla ya watu 30,258 wamefikiwa na kupatiwa elimu ya msaada wa kisheria ambapo kati ya hao wanawake ni 16,058 na wanaume 14,200.

Pia katika kipindi hicho wamefanikiwa kutatua migogoro mbalimbali na kutoa rufaa kwa watu wasiopungua 237, wanawake wakiwa 119 na wanaume 118.