Aga Khan yazindua mafunzo ya magonjwa ya dharura

Mratibu wa Mradi wa huduma ya magonjwa ya dharura hospitali ya Aga Khan Dk Hussein Manji kulia akimuelekeza Balozi wa Poland Krzysztof Buzalski wa pili kutoka kushoto katika kituo cha Mafunzo ya magonjwa ya dharura kilichopo Upanga jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
- Hospitali ya Aga Khan imezindua kituo cha mafunzo ya dharura kwa ajili ya kuboresha huduma ya afya kwa upande wa dharura kilichogharimu Sh 182 milioni.
Dar es Salaam. Aga Khan Tanzania (AKHS) wamezindua kituo cha mafunzo ya magonjwa ya dharura na kukabidhi vifaa muhimu vya matibabu ya magonjwa hayo chini ya ufadhili wa mradi wa kuboresha huduma ya dharura nchini (IMECT).
Kituo hicho kimezinduliwa kwa ushirikiano wa sekta za umma na sekta binafsi na kufadhiliwa na Serikali ya Poland kupitia Polish Aid na kutekelezwa na kituo cha misaada cha Kimataifa cha Poland.
Akizungumza leo jijini Dar es salaam Februari 16, 2024 Daktari bingwa wa magonjwa ya dharura na Mratibu wa mradi wa huduma ya dharura, Dk Hussein Manji amesema Kituo kimejengwa na kukarabatiwa kwa gharama ya Sh 182 milioni kikiwa na vifaa vya kisasa vya kufundishia na kuweka kigezo kipya cha elimu ya huduma za dharura nchini.
Amesema katika kuimarisha miundombinu ya huduma ya afya nchini mradi wa IMECT umesambaza vifaa vyenye thamani ya Sh 641.3 milioni kwa vituo saba ambavyo ni Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala,Temeke na hospitali ya Wilaya ya Chanika na Nyamagana ya jijini Mwanza.
Vingine ni Hospitali ya Aga Khan , Dar es Salaam na Aga Khan ya Zanzibar na vituo vingine.
"Maboresho ya kudumu ya viwango vya huduma za daharura ni kuhakikisha kuwa wataalamu wa afya wa nchini wanakuwa na vifaa vya kutosha kuokoa maisha na kutoa huduma muhimu inapotakiwa,"amesema Dk Manji.
Mratibu wa magonjwa ya dharura hospitali ya Wilaya ya Nyamagana,jijini Mwanza, Dk Godfrey Kajumbura amesema tangu mradi huo kuanzishwa wameshafundisha wahudumu 60 kwa ajili ya kutoa huduma za dharura.
"Sisi ni wanufaika wa mradi huu na leo hii tunatapewa vifaa kwa ajili ya huduma za dharura na huu mradi utasaidia watu mbalimbali katika jiji la Mwanza,"amesema Kajumbura.
Amesema kwa kuwa mradi unaendela anaamini utafika kwenye mikoa mingine ikiwepo Mbeya.
Kwa upande wake balozi wa Poland Krzysztof Buzalski amesema anafuraha kubwa kwa kuwa na ushirikianao na Tanzania na hata Rais wake kutembelea nchini na kufika katika hospitali ya Aga Khan wiki iliyopita.
Amesema ushirikiano uliopo ni kuhakikisha wanaokoa maisha ya watanzania hususani kwa wale wanaopata ajali kuhakikisha wanapata huduma za dharura kwa haraka.
"Hii ni kuhakikisha namba ya watoa huduma ya dharura inaongezeka na kuwasaidia kuwaokoa waathirika wa ajali na maafa,"amesema Buzalski.
Naye ,Muwakilishi wa Mganga Mkuu mkoanwa Dar es Salaam Dk Guinini Kamba amesema kituo hicho cha mafunzo ni msaada katika mkoa huo kwa kuzingatiwa umuhimuh wa huduma wa magonjwa ya dharura.
"Tunatoa shukurani kwa wale wote waliofadhili kwani ni ukweli kwamba watakao nufaika na kituo hiki si watu binafsi bali hata watumishi wa umma kutokana na ushirikiano wa Serikali na Aga Khan,"amesema Dk Kamba.
Mradi wa IMECT ulizinduliwa Septemba 2022 kwa kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya nchini katika kozi za huduma za dharura na kuvipa vituo vifaa vinavyohitajika huku mradi ukilenga kufanya maboresho ya kudumu na kuhakikisha kuna kuwa na vifaa vya kutosha kuokoa maisha.